Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili ya 4 ya Kipindi cha Majilio amemtaja Mtakatifu Josefu, Baba mlishi wa Yesu kuwa ni mfano bora wa kuigwa na waamini. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili ya 4 ya Kipindi cha Majilio amemtaja Mtakatifu Josefu, Baba mlishi wa Yesu kuwa ni mfano bora wa kuigwa na waamini. 

Mtakatifu Yosefu, Mtu wa haki ni mfano bora wa kuigwa na waamini

Mtakatifu Yosefu alikuwa na imani thabiti kwa Bikira Maria ndiyo maana alikua ameamua kumchumbia! Hakuelewa kinagaubaga kile kilichokuwa kinaendelea katika maisha ya Bikira Maria, ndiyo maana akaamua kutafuta suluhu ya kudumu kwa kumwacha Bikira Maria bila ya kuleta kashfa. Alipokuwa bado anawaza jambo hilo, Malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto,! Usiogope Yosefu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili 4 ya Kipindi cha Majilio inamweka Mtakatifu Yosefu kuwaongoza waamini kwa mang’amuzi na historia yake katika kuadhimisha Fumbo la Umwilisho, Noeli, yaani kuzaliwa kwa Mtoto Yesu. Mtakatifu Yosefu hapewi uzito wa juu kabisa, lakini uzoefu wake unafumbata hekima ya maisha ya Kikristo. Bikira Maria, Mtakatifu Yosefu na Yohane Mbatizaji ndio wahusika wakuu wanaowekwa mbele ya macho ya waamini katika Kipindi cha Majilio na kati yao, Mtakatifu Yosefu ni kati ya wanyenyekevu. Yosefu mtu mwenye haki, hakufungua mdomo wake kuhubiri, wala kusema, daima alikuwa tayari kutimiza mapenzi ya Mungu katika maisha yake. Akajitahidi kuwa kweli ni Mwenyeheri kutokana na umaskini wake wa kiroho na hivyo kustahilishwa kuurithi Ufalme wa mbinguni. Mtakatifu Yosefu alikuwa ni maskini kwa sababu alijitahidi kuishi kwa kuzingatia mambo msingi katika maisha, akatoka jasho ili kuipatia familia yake mahitaji msingi.

Huu ni ufukara wa maisha ya kiroho unaomwezesha mwamini kujiaminisha na kumtegemea Mwenyezi Mungu peke yake. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 22 Desemba 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema, Injili ya Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Majilio inamweka mbele ya macho ya waamini, Mtakatifu Yosefu na Bikira Maria Maria,  aliyekuwa ameposwa na Yosefu. Lakini kabla hawajakaa pamoja kama mume na mke, alionekana kuwa mjamzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Yosefu, mumewe, kwa vile alikuwa mwadilifu, hakutaka kumwaibisha hadharani; hivyo alikusudia kumwacha kwa siri baada ya kupata mahangaiko makubwa moyoni mwake. Ni uamuzi ambayo ulilenga kulinda na kutunza: utu, heshima na sifa ya Bikira Maria, kwani alitambua fika matokeo yake, ikiwa kama angemshitaki Bikira Maria hadharani. Hatima yake, ilikuwa ni kifo kwa kupigwa mawe.

Lakini Mtakatifu Yosefu mtu wa haki, alikuwa na imani thabiti kwa Bikira Maria ndiyo maana alikua ameamua kumchumbia! Hakuelewa kinagaubaga kile kilichokuwa kinaendelea katika maisha ya Bikira Maria, ndiyo maana akaamua kutafuta suluhu ya kudumu kwa kumwacha Bikira Maria bila ya kuleta kashfa. Alipokuwa bado anawaza jambo hilo, Malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akamwambia, “Yosefu, mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, maana amekuwa mjamzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Atajifungua mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu, kwa kuwa yeye ndiye atakayewaokoa watu wake katika dhambi zao.”. (Mt. 1:20-21). Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, tangu wakati huo, Mtakatifu Yosefu akatii maneno ya Malaika wa Bwana, akajiaminisha na kumtegemea Mungu katika maisha yake kwa kukubali kupokea hali ambayo kibinadamu ni tete sana hata wakati mwingine si rahisi kuweza kueleweka anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Mtakatifu Yosefu kwa njia ya imani akafahamu kwamba, Mtoto atakayezaliwa na Bikira Maria ni Mwana wa Mungu na yeye amepewa dhamana na wajibu wa kuwa Baba mlishi wa Mtoto Yesu. Mfano wa Mtakatifu Yosefu, Baba mlishi wa Yesu katika unyenyekevu na imani yake, unawabidiisha waamini kuzama na kwenda mbele zaidi katika imani ili kukubali kushangazwa na mpango wa Mungu katika maisha yao, kwa kuwafungulia  mwelekeo na mwanga angavu zaidi wa maisha kumwelekea Kristo Yesu na Neno lake. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwa njia ya maombezi ya Mtakatifu Yosefu na Mchumba wake Bikira Maria, wawasaidie kuwa wasikivu wa Mtoto Yesu anayekuja, anayetaka watu wampokeee na kumweka kuwa ni kati ya sera na vipaumbele vya maisha yao.

Papa: Mtakatifu Yosefu
22 December 2019, 10:42