Tafuta

Vatican News
Katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Nicholaus wa Bari, Parokia ya Mtongani Jimbo kuu la Dar es Salaam inaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 20 ya uwepo wake! Katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Nicholaus wa Bari, Parokia ya Mtongani Jimbo kuu la Dar es Salaam inaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 20 ya uwepo wake!  (Vatican Media)

Kumbu kumbu ya Mt. Nicholaus: Parokia ya Mtongani, Miaka 20!

Tarehe 6 Desemba 2019 Kanisa linaadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Nicholaus wa Bari. Papa anawaalika waamini kuiga mfano wa fadhila na utakatifu wake wa maisha; kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi. Waamini wajitahidi daima kuutafuta Uso wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya waja wake. Huyu ndiye Emmanueli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake, Jumatano tarehe 4 Desemba 2019 kuhusu wosia uliotolewa na Mkatifu Paulo mtume kwa wazee wa Efeso, amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kupyaisha upendo wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Watambue kwamba, ndani mwake kuna “Amana ya Imani: “Fidei Depositum” wanayopaswa kwenda kujichotea. Wawe mstari wa mbele kuwaenzi mapadre wao kwa njia ya sala na sadaka zao, ili waweze kuwa kweli ni mashuhuda wa viongozi wanaokesha na kusali, ili kuwafunulia watu upendo na huruma ya Mungu. Amewashukuru na kuwapongeza wale wote wanaoendelea kumuenzi Mwenyeheri Popieluszko kutoka Poland, Padre mchapakazi, aliyeuwawa kikatiliki kutokana na utawala wa Kinazi. Ni shuhuda wa imani, upendo na matumaini kwa Kristo Yesu, hususan kwa waamini ambao wamepokwa utu, heshima, haki zao msingi pamoja na uhuru wa kuabudu.

Baba Mtakatifu amewakumbusha watu wa Mungu kutoka nchini Poland kwamba, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Majilio, waamini wataadhimisha Siku ya XX kwa ajili ya Kuombea na kuyasaidia Makanisa Hitaji kutoka Ulaya ya Mashariki. Hii ni siku ambayo waamini wanajinyima ili kuchangia katika mchakato wa uenezaji wa Habari Njema kwa nchi za Ulaya ya Mashariki, kama kielelezo cha moyo wa upendo na udugu wa kibinadamu. Ijumaa, tarehe 6 Desemba 2019 Mama Kanisa anaadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Nicholaus wa Bari. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuiga mfano wa fadhila na utakatifu wake wa maisha; kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Waamini wajitahidi daima kuutafuta Uso wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya waja wake. Mtakatifu Nicholaus wa Bari anaheshimiwa sana na Makanisa ya Mashariki kama Baba wa majadiliano ya kiekumene na masalia yake  yanahifadhiwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Nicholaus wa Bari, Jimbo kuu la Bari-Bintonto, Italia. Ibada ya kuabudu masalia haya inayotekelezwa na Wakristo ambao bado wamegawanyika ni changamoto ya kumwomba asaidie kuganga na kuponya kashfa ya utengano kati ya Wakristo wa Makanisa ya Mashariki na Magharibi. Kwa waamini wa Makanisa haya mawili kuendelea kuonesha Ibada kwa watakatifu hawa ni kielelezo cha utashi wa watu wa Mungu kutaka kuungana tena ili kukuza na kudumisha umoja, ushuhuda na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Itakumbukwa kwamba, Parokia ya Mtakatifu Nicholaus, Mtongani Kunduchi, Jimbo kuu la Dar es Salaam, tarehe 8 Desemba 2019 inaadhimisha Jubilei ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwake. Hii ni fursa ya kupyaisha tena na tena imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Papa: Mt. Nicholaus
04 December 2019, 15:48