Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anaunga mkono juhudi zinazotekelezwa na mkutano wa "Normandy Format" ili Ukraine iweze kupata amani katika haki kwa ajili ya watu wake. Baba Mtakatifu Francisko anaunga mkono juhudi zinazotekelezwa na mkutano wa "Normandy Format" ili Ukraine iweze kupata amani katika haki kwa ajili ya watu wake.  (AFP or licensors)

Mkutano wa "Normandy Format": Amani katika haki nchini Ukraine!

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, mkutano huu utaweza kuibua suluhu ya amani ya kudumu. Baba Mtakatifu anasema, anawasindikiza kwa sala na sadaka yake na ametumia fursa hii kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuunga mkono juhudi hizi, ili kwa njia ya majadiliano ya kisiasa, amani katika haki iweze kupatikana nchini Ukraine na kati ya watu wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 8 Desemba 2019 amegusia kuhusu mkutano kati ya Rais Volodymyr Zelenskiy wa Ukraine, Rais Vladimir Putin wa Urussi pamoja na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani unaofanyika mjini Paris, Ufaransa Jumatatu, tarehe 9 Desemba 2019. Mkutano huu kitaalam unajulikana kama  “Normandy Format” yaani Umoja unaoziunganisha nchi za: Ufaransa, Ujerumani, Urussi na Ukraine, ulioundwa kunako tarehe 6 Juni 2014 ili kutafuta suluhu ya amani kwa vita inayoendelea huko Mashariki mwa nchi ya Ukraine. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, mkutano huu utaweza kuibua suluhu ya amani ya kudumu. Baba Mtakatifu anasema, anawasindikiza kwa sala na sadaka yake na ametumia fursa hii kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuunga mkono juhudi hizi, ili kwa njia ya majadiliano ya kisiasa, amani katika haki iweze kupatikana nchini Ukraine na kati ya watu wake.

Wakati huo huo, habari kutoka Ukraine zinasema kwamba, Rais Volodymyr Zelenskiy wa Ukraine, tarehe 5 Desemba 2019 amekutana na kuzungumza na viongozi pamoja na wawakilishi wa dini mbali mbali nchini humo ili kupata mawazo yao kuhusu mkutano wa “Normandy Format”. Kati ya mambo yaliyojitokeza katika mkutano huu ni umuhimu wa kuanza mchakato wa haki, amani na maridhiano unaofumbatwa katika majadiliano, ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Ukraine. Viongozi wa kidini wamesema ni jambo lisilokubalika kuona uhuru wa kidini ukisiginwa na waamini wakinyanyaswa na hata kuuwawa. Kuna umuhimu kwa Serikali kusimama kidete kulinda usalama wa raia na mali zao na kwamba, maisha ya binadamu ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Nyanyaso na mipasuko ya kidini inakinzana na utashi wa ujenzi wa umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii nchini Ukraine.

Makanisa yana mchango mkubwa katika mchakato wa ujenzi wa amani, umoja na mshikamano nchini Ukraine. Inasikitisha kuona kwamba, vita inayoendelea nchini Ukraine ni kwa ajili ya mafao ya mataifa ya kigeni ambayo yamewekeza nchini humo na yanaendelea kufaidika kwa gharama ya maisha na umaskini wa wananchi wa Ukraine. Umefika wakati kwa watu wa Mungu nchini Ukraine kusimama kidete kukataa kutumiwa na mataifa ya nje kwa mafao yao binafsi. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni katika hotuba yake elekezi kwa viongozi wa Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine alihimiza umuhimu wa sala na maisha ya kiroho kama chemchemi ya faraja kutoka kwa Mungu. Alilitaka Kanisa liendelee kuwa ni shuhuda wa matumaini ya Kikristo kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo; Kanisa lioneshe ukaribu kwa watu wa Mungu wanaoteseka na kwamba, kuna haja ya kuendelea kukazia dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa!

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, Ukraine katika kipindi cha miaka mitano iliyopita imejikuta ikitumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe; vita ambayo imepelekea wananchi wa kawaida kulipa gharama kubwa. Hii ni kampeni inayochochea vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kisiasa na hata kidini. Lakini katika yote haya, watambue kwamba, daima ameendelea kuwabeba na kuwahifadhi katika sakafu ya moyo wake kwa njia ya sala na sadaka yake ya kila siku. Katika shida na mahangaiko ya watu kutokana na vita pamoja na madhara yake, Kanisa linapaswa kuwa ni shuhuda wa matumaini ya Kikristo, msingi wa umoja, upendo na mshikamano wa dhati na kwamba, haya ni matumaini ambayo hayadanganyi kamwe! Watambue kwamba, wamehesabiwa haki, wamepatanishwa na kuokolewa na Mwenyezi Mungu. Katika dhidi na mahangaiko mbali mbali waendelee kuwa na matumaini, saburi na uthabiti wa moyo kwa njia ya Roho Mtakatifu. Matumaini ya Kikristo ni chemchemi ya ufufuko, maisha na mwanzo mpya! Katika shida, hali na mazingira magumu na hatarishi kama haya ya vita, waamini wajifunze daima kuwa karibu sana na Kristo Yesu, chemchemi ya matumaini yao.

Huu ni umoja, mshikamamo na mafungamano yanayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo na kusimikwa katika imani, historia na shuhuda mbali mbali zinazotolewa na watakatifu ambao ni majirani zao. Watu wa Mungu nchini Ukraine wamejifunza kulipa ubaya kwa wema! Hawa ni watu wenye ushupaji na ushujaa kwa Kikristo kama unavyobainishwa kwenye Heri za Mlimani, muhtasari wa Mafundisho Makuu ya Kristo Yesu kwa waja wake. Wamejifunza kuwapenda na kuwaombea adui zao, huku wakijichotea nguvu kutoka katika Fumbo la Msalaba. Ni watu ambao wameteseka, wakanyanyasika na kuuwawa kikatili, lakini hawa ndio waliovikwa taji ya ushindi kama mashuhuda wa Kristo Yesu, kwa kuandika kurasa chungu za imani, matunda ya mbegu ya matumaini ya Kikristo!

Papa: Ukraine

 

 

08 December 2019, 15:29