Tafuta

Mfuko wa Pensheni wa Mawakili Italia, "Cassa Nazionale del Notariato" Unaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake! Mfuko wa Pensheni wa Mawakili Italia, "Cassa Nazionale del Notariato" Unaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake! 

Papa Francisko asema dumisheni haki na mshikamano wa upendo!

Huu ni mfuko ambao unawajibika kuwahudumia wanachama wake pamoja na familia zao, wanaopambana na hali pamoja na mazingira magumu ya maisha. Huduma hii inapaswa kuongozwa na kanuni ya umoja na mshikamano kati ya wanachama wake. Dhamana hii haina budi kutekelezwa kwa kusaidia kuwafunda mawakili vijana wanaoingia katika taaluma. Kwa hakika mwanzo ni mgumu

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Mfuko wa Pensheni kwa ajili ya Mawakili nchini Italia “Cassa nazionale del notariato” ulianzishwa kunako mwaka 1919 kwa ajili ya kuwahudumia mawakili waliokuwa wanakula pensheni baada ya kulitumikia taifa kwa sadaka na majitoleo, kwa ari na moyo mkuu. Wanachama wa mfuko huu wanahamasishwa kushikamana kwa dhati, wakati huu wanapoadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. Kwa bahati mbaya, walimwengu wanaanza kugubikwa na tabia ya uchoyo na ubinafsi, kiasi kwamba, upendo na mshikamano vinaonekana kana kwamba, havina nafasi tena katika vipaumbele vya maisha ya watu katika ulimwengu mamboleo. Mfuko wa Pensheni kwa ajili ya Mawakili nchini Italia unapaswa kujizatiti katika lengo na msingi wa kuanzishwa kwake, ili juhudi hizi ziweze kuungwa mkono pia na vijana wa kizazi kipya. Haki msingi za binadamu, utu na heshima yake ni mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika shughuli za Mfuko huu.

Kuna kundi la watu ambao kipato chao kimeshuka sana kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha. Kuna familia ambazo zinateseka na kuogelea kwenye dimbwi la umaskini wa hali na mali baada ya kuingia kwenye mfumo wa pensheni, kumbe, haki na upendo ni chanda na pete kwa ajili ya kuwahudumia wazee wanaokula pensheni. Hii ni sehemu ya changamoto zilizowasilishwa mbele ya Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Mfuko wa Pensheni kwa ajili ya Mawakili nchini Italia “Cassa nazionale del notariato”. Huu ni mfuko ambao unawajibika kuwahudumia wanachama wake pamoja na familia zao, wanaopambana na hali pamoja na mazingira magumu ya maisha. Huduma hii inapaswa kuongozwa na kanuni ya umoja na mshikamano kati ya wanachama wake. Dhamana hii haina budi kutekelezwa kwa kusaidia kuwafunda mawakili vijana wanaoingia katika taaluma. Mwanzoni wa kazi yao, ni wazi watapambana na changamoto mbali mbali sanjari na kuwa makini na hali pamoja namaisha magumu kwa familia za mawakili wazee.

Baba Mtakatifu anawasihi na kuwahimiza kujikita zaidi katika mchakato wa kujenga na kudumisha haki inayomwilishwa katika upendo na kamwe wasitumbukie kwenye kishawishi cha kutafuta faida kubwa, bali wakuze na kudumisha ari na mwamko wa huduma ya upendo, kwa kuzingati: sheria, kanuni na taratibu zilizopo, ili haki iweze kupewa kipaumbele cha pekee. Changamoto kubwa iliyoko mbele yao ni kuhakikisha kwamba, wanajenga mazingira yatakayoiwezesha jamii kusimikwa katika utu badala ya vitu kwa kutaka kupata faida kubwa. Mfuko ujenge utamaduni wa kuwasikiliza na kuwahudumia wanachama wake katika masuala ya kisheria, kiuchumi na kijamii. Ili wakili aweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake, hana budi kujizatiti kila siku katika misingi ya haki, uaminifu, ili kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wateja wake, daima fadhila ya upendo isaidie kufafanua mahusiano na mafungamano ya kijamii kati yao.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, walimwengu wanashuhudia kuzaliwa kwa ubinadamu (humanism) mpya unaomfanya mtu ajitambulishe kwanza kwa uwajibikaji wake mbele ya wenzake na mbele ya historia. Katika muktadha kama huu, wafanyakazi katika sekta mbali mbali wanahimizwa na Mama Kanisa kutoa huduma makini itakayosaidia ujenzi wa udugu wa haki, ili mwisho  wa siku waweze kujenga jamii mintarafu mpango wa Mungu unaozingatia kanuni maadili na utu wema. Tasnia ya mawakili ni tete sana kwa sababu ina umuhimu wake katika maisha na ustawi wa jamii husika. Ili kutekeleza vyema dhamana na wajibu huu kuna haja kwa wahusika kuzingatia kanuni zifuatazo: uhakika wa ujuzi, weledi na matumizi sahihi ya sayansi na teknolojia; ukweli, uwazi na uadilifu.

Baba Mtakatifu anasema, haya ni mambo msingi yanayoweza kuwasaidia mawakili kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao ndani ya jamii. Hizi ni tunu msingi katika utekelezaji wa majukumu ya mtu binafsi na kama kikundi cha mawakili. Katika shughuli zao wanahamasishwa kuwa kweli waaminifu katika kutoa tafsiri na utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa. Ili kuweza kuifanya kazi hii kwa: nidhamu, welezi na uwajibikaji kuna haja kwa mawakili kuendea kupyaisha ujuzi wao, kwa kuzingatia mafao, ustawi na maendeleo ya wengi. Mawakili wawe ni mfano bora kwa kuwa ni kimbilio la wanyonge; wawe ni mfano bora wa kuigwa kutokana na ushuhuda wa tunu msingi za maisha zinazobubujika kutoka katika Mfuko huu.

Papa: Mawakili

 

 

10 December 2019, 15:55