Tafuta

Vatican News
Waamini wa Kanisa la Mukacheco, Madhehebu ya Bizantina linaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 30 tangu lilipojitokeza hadharani kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Waamini wa Kanisa la Mukacheco, Madhehebu ya Bizantina linaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 30 tangu lilipojitokeza hadharani kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.  (Vatican Media)

Kumbu kumbu ya Miaka 30 ya maisha ya hadhara ya Kanisa la Mukachevo, Ukraine

Miaka 30 tangu Kanisa la Mukachevo lilipotoka mafichoni na kuanza kuonekana hadharini ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kanisa la Mukachevo ni Mama wa mashuhuda wengi wa imani, ambao wamethubutu kuyamimina maisha yao kama kielelezo cha uaminifu wao kwa Kristo, Kanisa Katoliki na kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro! Ushuhuda!

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Familia ya Mungu kutoka nchini Ukraine kutoka kwenye Madhehebu ya Kibizantina imekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 11 Desemba 2019 kama sehemu ya maadhimisho ya Kumbukumbu ya Miaka 30 tangu Kanisa la Mukachevo lilipotoka mafichoni na kuanza kuonekana hadharini ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Baba Mtakatifu ameungana na waamini hawa kumshukuru Mungu aliyelikomboa Kanisa lao baada ya dhuluma za miaka mingi kutoka katika utawala wa Urussi. Kanisa la Mukachevo ni Mama wa mashuhuda wengi wa imani, ambao wamethubutu kuyamimina maisha yao kama kielelezo cha uaminifu wao kwa Kristo, Kanisa Katoliki na kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa namna ya pekee, Kanisa linamkumbuka Mwenyeheri Askofu Teodor Romza ambaye katika kipindi cha giza, nyanyaso na madhulumu makubwa alifanikiwa kuwangoza watu wa Mungu, akishuhudia hekima ya Kiinjili na ujasiri wa kiimani, daima akajitahidi kufuata mfano wa Kristo Yesu, Mchungaji mwema, aliyejisadaka na kuyamimina maisha yake kwa ajili ya Kondoo wake.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru wazazi na walezi ambao katika maisha na utume wao, wameendelea kusimama kidete kutangaza, kushuhudia na kurithisha imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao. Huu ni ushuhuda wa imani thabiti, hai na Katoliki. Baba Mtakatifu anawashukuru waamini hawa kwa ushuhuda wao, changamoto na mwaliko wa kuendelea kupyaisha imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Wajenge ari na moyo wa kutaka kukutana na kuzungumza na Kristo Yesu kila wakati bila kuchoka. Kila mwamini anaitwa na kuhamasishwa kujichotea furaha ya kweli kwa kukutana na Kristo Yesu katika safari ya maisha yake. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewatakia maandalizi mema na hatimaye, maadhimisho ya Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2019. Mtoto Yesu azaliwe tena nyoyoni mwao!

Papa: Ukraine

 

 

11 December 2019, 15:55