Tafuta

Vatican News
Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu mwaka 2019 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake na Mtakatifu Paulo VI Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu mwaka 2019 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake na Mtakatifu Paulo VI  (Vatican Media)

Jubilei ya Miaka 50 ya Baraza la Kipapa: Wenyeheri na Watakatifu

Baba Mtakatifu Francisko anasema utakatifu ni ushuhuda unaobubujika kutoka katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Watakatifu ni kielelezo angavu cha mwanga wa Injili ambayo imemwilishwa katika uhalisia wa maisha kiasi cha kuonesha ukaribu wake. Utakatifu wa maisha ndio mwanga halisi wa Kanisa, dira na mwongozo wa watu wa Mungu waliokombolewa. Ni kipaumbele cha Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu lilianzishwa kunako tarehe 8 Mei 1969 na Mtakatifu Paulo VI kwa kuanzisha Mabaraza mawili ya Kipapa, yaani Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu pamoja na Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa. Akatenga rasilimali fedha na watu kwa kusoma alama za nyakati pamoja na kujibu shida na changamoto mbali mbali zilizokuwa zinajitokeza ndani ya Makanisa mahalia. Katika kipindi cha Miaka 50 Baraza hili limeandika wasifu na tunu msingi za maisha ya kiroho, kielelezo na mfano bora wa kuishi tunu msingi za maisha ya Kikristo. Kanisa limeweza kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, ushuhuda kwamba, utakatifu wa maisha ni jambo linalowezekana.

Watakatifu kimsingi ni wadhambi waliotubu na kumwongokea Mungu katika hija ya maisha yao ya kila siku; walianguka lakini wakathubu kusimama tena kwa neema ya Mungu na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Watakatifu ni mashuhuda wa amini wa Neno la Mungu ambalo limemwilishwa katika historia na liko karibu na mazingira ya watu. Utakatifu ni ushuhuda unaobubujika kutoka katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Hii ni changamoto kwa waamini kuangalia na kupima mifano mbali mbali ya utakatifu wa maisha, ili kutambua mpango wa Mungu katika maisha na kujitahidi kuumwilisha. Watakatifu ni kielelezo angavu cha mwanga wa Injili ambayo imemwilishwa katika uhalisia wa maisha kiasi cha kuonesha ukaribu wake. Utakatifu wa maisha ndio mwanga halisi wa Kanisa, dira na mwongozo wa watu wa Mungu waliokombolewa.

Huu ni muhtasari wa hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 12 Desemba 2012 kwa wajumbe wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Baraza limekuwa likitekeleza dhamana na wajibu wake kwa umakini mkubwa, ili kuwa na uhakika kwa njia ya chunguzi za kisayansi ili hatimaye, kutoa hukumu ya kweli kuhusu: ushuhuda wa imani, fadhila za kishujaa, sadaka ya maisha pamoja na miujiza iliyosadikiwa kutendeka. Haya ni mambo tete yanayopaswa kuzingatiwa kisheria pamoja na matamanio halali ya watu wa Mungu wanaojiaminisha kwa sala na maombezi ya watakatifu, kielelezo na mfano bora wa kuigwa. Ni wajibu wa Baraza kuhakikisha kwamba, linaondoa ndago zote za mashaka kama ambavyo dhamana hii ilivyotekelezwa na Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa katika kipindi cha karne nne.

Wajibu huu unapaswa kuendelezwa na kudumishwa kwa kujikita katika: dhamiri nyofu na huru; kwa kuondokana na maamuzi mbele; kwa kutenganisha majukumu ya wahusika kwa kutambua kwamba, hatima ya mchakato mzima ni ushuhuda wa utukufu wa Mungu na mafao ya maisha ya kiroho kwa upande wa Kanisa, daima ukweli ukizingatiwa kama sehemu ya utimilifu wa Injili. Watoa hoja “Postulatori” watambue kwamba, wanapaswa kujiweka katika huduma ya ukweli kwa kushirikiana na Vatican mintarafu sheria, kanuni na taratibu husika. Hii ni kazi ya maisha ya kiroho inayotekelezwa kwa kuzingatia unyeti wa Kiinjili na kanuni maadili. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru wajumbe wote kwa huduma makini wanayoitoa kwa ajili ya Kanisa, kwa kutambua kwamba, utakatifu wa maisha ni wito kwa kila mwamini mbatizwa. Hii ni chachu ya maisha na utume wa Kanisa na ni kati ya vipaumbele vyake.

Itakumbukwa kwamba,  hivi karibuni Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, limetoa chapisho la nne la Prospero Lambertini, kwa heshima ya Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti  mstaafuwa Baraza hilo kwa miaka kumi, na ambaye mnamo tarehe 8 Juni 2018 katimiza miaka 80 ya kuzaliwa. Prospero Lambertini ambaye baadae alikuwa Baba Mtakatifu, tangu 1740 – 1758, na kubeba jina la Benedikto XIV, aliandika sana juu ya mchakato wa kutangaza waamini wenyeheri ama watakatifu ndani ya Kanisa. Chapisho lililotolewa sasa limeitwa “De servorum Dei beatificatione et beatorum canonizatione”, yaani Watumishi wa Mungu kutangazwa wenyeheri na wenyeheri kutangazwa watakatifu. Sehemu ya kwanza ya chapisho hilo la Prospero Lambertini lililotafsiriwa kwa lugha ya kiitalia, imejikita zaidi katika masuala ya miujiza. Lambertini, na baadae Papa Benedikto XIV aliamini kwamba Kanisa, na kwa namna ya pekee Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu linafanya kwa uangalifu na umakini mkubwa utambuaji wa matukio kuwa ni miujiza inayotokea kwa maombezi ya watumishi wa Mungu ama wenyeheri.

Pili, chapisho linaonesha umuhimu wa nafasi ya madaktari na watendaji wataalamu wa afya kuthibitisha miujiza hiyo, hasa kuhusu ukubwa wa ugonjwa na uponyaji wake kimuujiza. Mwishoni chapisho linazungumzia uponyaji wa kipekee kabisa wa viwete na wasioweza kutembea. Sehemu hii inasimulia pia mfano wa mtoto wa miaka minne ambaye tangu kuzaliwa hakuwahi kutembea mbali ya juhudi ya tiba zilizofanyika. Kisha akiwa na umri wa miaka mine alipelekwa kwenye nyumba ya kitawa aliyokuwa akiishi Mt. Theresa wa Avila. Siku ya mwisho ya Novena mtoto huyo alipona na akaanza kutembea. Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu limetoa chapisho hili kwa heshima ya Kardinali Angelo Amato, kwa kazi nzuri aliyoifanya akiwa mwanataalimungu ndani ya Kanisa, na kwa namna ya pekee akiwa Mwenyekiti wa Baraza hilo kwa miaka kumi.

Katika kipindi hicho, wametangazwa watakatifu 100, na wenyeheri 1233, kati yao ni pamoja na Yohane Paulo II, Yohane XXIII, Mama Theresa wa Calcutta, watoto Francisko na Yasinta waliotokewa na Bikira Maria kule Fatma, Ureno, na tarehe 14 Oktoba 2018, walitangazwa Paolo VI na Oscar Romero miamba wa imani ya Kanisa, waliopambana na changamoto katika maisha na utume wao, sasa Kanisa limewavika kilemba cha heshima na utakatifu wa maisha!

Papa: Baraza Miaka 50

 

12 December 2019, 17:14