Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawaambia wachumi na wajasiriamali vijana kutoka Ufaransa katika sera na mikakati yao ya kiuchumi kuzingatia wongofu wa kiekolojia Papa Francisko anawaambia wachumi na wajasiriamali vijana kutoka Ufaransa katika sera na mikakati yao ya kiuchumi kuzingatia wongofu wa kiekolojia  (Vatican Media)

Papa Francisko: Wongofu wa kiekolojia ni muhimu!

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, waamini walei wanashiriki: Ufalme, Ukuhani na Unabii wa Kristo katika maisha yao, kumbe wanapaswa kuchangia kwa bidii matendo yao ili mema yaliyoumbwa yasitawishwe kwa kazi ya binadamu, kwa ufundi na maarifa kwa ajili ya mafao ya watu wengi zaidi kadiri ya mpango wa Uumbaji na mwanga wa Neno la Mungu. Wongofu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wachumi na wajasiriamali vijana kutoka nchini Ufaransa kuanzia tarehe 1-3 Desemba 2019 wamekuwa wakifanya “hija kwa ajili ya mafao ya wengi jijini Roma”. Hii imekuwa ni fursa kwa vijana hawa kuzama zaidi katika wito wao mintarafu mwanga wa Mafundisho Jamii ya Kanisa. Kundi hili la vijana limepata nafasi ya kusikiliza hotuba kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican pamoja na Mama Elizabeth Beton-Delègue, Balozi wa Ufaransa mjini Vatican. Kwa ufupi vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele kufuata mifano bora ya maisha kutoka kwa watakatifu na wafiadini, waliosadaka maisha yao kwa ajili ya Mungu, Kanisa na jirani! Watakatifu ni wadhambi waliotubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu; wakasimama kidete: Kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake. Ni watu waliokuwa na furaha ya kweli iliyokuwa inabubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Vijana wanahamasishwa na Mama Kanisa kujikita katika malezi ya awali na endelevu kwa kutumia mwongozo uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko: DOCAT: Yaani “Kitabu cha Mkusanyiko wa Mafundisho Jamii ya Kanisa, tayari kuyatangaza na kuyashuhudia katika vipaumbele vya maisha na utume wao! Huu ni muhtasari wa mafundisho Jamii ya Kanisa kutoka kwa Papa Leo XIII “Rerum Novarum” yaani “Mambo Mapya” msingi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayofumbatwa katika: Haki msingi, utu na heshima ya binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, hadi katika Mafundisho ya Papa Francisko: “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” na “Amoris laetitia” yaani “Furaha katika upendo ndani ya familia”. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 2 Desemba 2019 amekutana na kuzungumza na Wachumi na wajasiriamali vijana kutoka nchini Ufaransa. Katika hotuba yake, amewataka vijana kujikita katika wongofu wa kiekolojia, ili kuwa tayari kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote sanjari na kilio cha maskini wanaotumbukizwa katika mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo, bila kusahau umaskini wa hali na kipato.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa ni mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo na shughuli mbali mbali wanazotekeleza kama sehemu ya taaluma zao. Vijana waendelee kuchota utajiri wa mafundisho yanayobubujika kutoka katika Injili, kwa kutambua kwamba, wana wajibika katika kutoa maamuzi kuhusiana na masuala ya kijamii na kiuchumi; mambo yanayoweza kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa siku za usoni. Changamoto kubwa kwa wachumi na wajasiriamali ni kuweka uwiano bora kati ya sheria na kanuni soko na utanadawazi mintarafu mwanga na tunu msingi za Kiinjili, ili kuwa kweli ni mashuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Waamini walei wanashiriki: Ufalme, Ukuhani na Unabii wa Kristo katika maisha yao, kumbe wanapaswa kuchangia kwa bidii matendo yao ili mema yaliyoumbwa yasitawishwe kwa kazi ya binadamu, kwa ufundi na maarifa kwa ajili ya mafao ya watu wengi zaidi kadiri ya mpango wa Uumbaji na mwanga wa Neno la Mungu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema,  mema hayo yagawanyike kati ya watu kwa haki, yasaidie mchakato wa kukuza na kudumisha maendeleo fungamani ya binadamu katika uhuru wa kibinadamu na wa Kikristo.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, “hija kwa ajili ya mafao ya wengi jijini Roma” itawasaidia kufanya mang’amuzi ili kutambua na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Si rahisi sana kuweza kufanya mageuzi, kwani kuna wakati ushuhuda wao unaweza kuwagharimu maisha kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro na Paulo, Miamba ya imani. Katika ulimwengu mamboleo nguvu ya fedha inatawala, lakini vijana kwa kujiaminisha chini ya ulinzi na uongozi wa Roho Mtakatifu wanaweza kuwa kweli ni mitume wamisionari, changamoto ni kuendelea kujipyaisha kila wakati na wala wasidumae hata kidogo. Baba Mtakatifu anawataka vijana hawa kuwa makini daima wanapofanya maamuzi kwa ajili ya vitega uchumi, familia na jamii inayowazunguka kwa kuzingatia misingi ya haki jamii, ujira unaokidhi mahitaji msingi ya wafanyakazi pamoja na kuwaundia wafanyakazi mazingira bora zaidi ya kazi, bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema ni wajibu wa dhamiri ya waamini iliyokwisha kuundwa ipasavyo, kuiandika sheria ya Kimungu katika maisha ya mji wa duniani. Nao kutoka kwa makuhani, watarajie kupewa mwanga na nguvu ya kiroho. Lakini wasifikiri kuwa wachungaji wao ni daima mabingwa kuhusu mambo haya kiasi kwamba, wakati wowote wana majibu kwa kila suala linalojitokeza; wala huo si wajibu wa kichungaji. Bali waamini walei wenyewe washike nyajibu zao, katika mwanga wa hekima ya Kikristo, na wazingatie kwa heshima mafundisho ya Mamlaka funzi ya Kanisa. Utekelezaji wa Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote” ni sehemu ya mbinu mkakati wa utunzaji bora wa mazingira na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kusikiliza na kujibu sauti ya vijana wanaotaka kuona sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira kutokana na athari zake kuendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Kuna haja ya kubadili mtindo wa maisha na mahusiano pamoja na wafanyakazi wao, ili kujenga utamaduni mpya katika ulimwengu wa wafanyakazi. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kufanya wongofu wa kiekolojia unaokita mizizi yake katika uhalisia wa maisha ya watu. Wongofu huu unakwenda sanjari na wongofu wa maisha ya kiroho, kwa kukazia ubora wa maisha unaofumbata unabii na tafakari ili kufurahia maisha bila kumezwa na malimwengu. Vijana wajitahidi kujinyima na kujisadaka katika maisha kwa kuwa ni watu wa kiasi, ili waweze kupata amani na furaha ya kweli katika maisha, kwa kumshukuru Mungu kwa kila jambo.

Papa: Vijana: Ufaransa
03 December 2019, 15:48