Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya watu wa Mungu kutoka DRC. Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya watu wa Mungu kutoka DRC. 

Papa Francisko aadhimisha Ibada ya Misa kwa watu wa Mungu DRC

Papa ameongoza Ibada ya Misa Takatifu: Kkusherehekea Jubilei ya Miaka 25 ya Umoja na Mshikamano wa watu wa Mungu kutoka DRC wanaoishi Roma na Italia. Kanisa limemkumbuka Mwenyeheri Sr. Marie Clementine Anwarite Nengapeta aliyeuwawa kikatili huko DRC kunako tarehe 1 Desemba 1964, lakini akawa tayari kuwasamehe watesi wake kwa kuwa walikuwa hawajui wanalolitenda!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Majilio ni mwanzo wa Mwaka mpya wa Kanisa na mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuanza hija ya kujiandaa kumpokea Kristo Yesu anayezaliwa tena katika maisha yao, ili hatimaye, aweze kuzima njaa na kiu ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mataifa. Waamini wanahamasishwa kukianza Kipindi cha Majilio kwa kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa na Maisha ya Sala yanayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa maskini na wahitaji zaidi. Kipindi hiki cha Majilio, Sehemu ya kwanza kuanzia tarehe 1-16 Desemba, Kanisa linatafakari kuhusu Ujio wa Pili wa Kristo Yesu, atakapokuja kuwahudumu wazima na wafu na wala ufalme wake hautakuwa na mwisho. Sehemu ya Pili ni Ujio wa Kristo Yesu katika Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipotwaa mwili na kukaa kati ya watu wake katika mambo yote akawa sawa na binadamu isipokuwa hakutenda dhambi!

Maadhimisho ya Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio, tarehe 1 Desemba 2019 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican yamepambwa kwa namna ya pekee na Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili kusherehekea Jubilei ya Miaka 25 ya Umoja na Mshikamano wa watu wa Mungu kutoka DRC wanaoishi Roma na Italia katika ujumla wake. Kanisa limemkumbuka Mwenyeheri Sr. Marie Clementine Anwarite Nengapeta aliyeuwawa kikatili huko DRC kunako tarehe 1 Desemba 1964, lakini akawa tayari kuwasamehe watesi wake kwa kuwa walikuwa hawajui wanalolitenda! Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amefafanua maana ya kipindi cha majilio, kinachoonesha ujio wa Masiha Mkombozi wa ulimwengu, chemchemi ya matumaini na faraja kwa watu wake wanao ogelea katika “patashika nguo kuchanika”! Katika Kipindi hiki cha mwanzo wa Mwaka wa Kanisa, waamini wakumbuke kwamba, daima Mwenyezi Mungu anataka kuambatana na ataendelea kuwa pamoja nao hadi utimilifu wa nyakati.

Na kwa njia hii, Masiha anakuwa kweli ni chemchemi ya furaha na faraja kwa waja wake. Neno wa Mungu amefanyika mwili kwa ajili ya watu wake na watu wa Mataifa kwa njia zao wenyewe watapanda kwenda kwenye mlima wa Bwana, Nyumbani mwa Bwana kwa sababu nyumbani mwake kuna nafasi tele kwa ajili ya wote na watu wote wanapata hifadhi katika Moyo wake Mtakatifu. Hiki ni kielelezo cha familia ya Mungu kutoka nchini DRC ambako wameacha nyumba, ndugu na jamaa, wakafanikiwa kuonja ukarimu na upendo wa Mungu hata kama bado wanakabiliana na changamoto mbali mbali za maisha. Lakini mbele ya Mwenyezi Mungu hakuna “Mgeni; Mtu wa kuja; Mnyamahanga wa Kyasaka” wote wanahesabika kuwa ni watoto wateule wa Mungu. Kanisa kimsingi ni nyumba ya Mungu na hapa waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanapaswa kujisikia kuwa wako nyumbani, ili kuweza kutembelea kwa umoja, upendo na mshikamano.

Mwaliko wa kwenda nyumbani kwa Bwana unapaswa kupokelewa kwa mikono miwili na wala si kama walivyofanya wakati wa Nuhu, watu wakashindwa kusoma alama za nyakati na matokeo yake wakaangamia kwa gharika kuu. Hii inatokana na ukweli kwamba, watu waligeuza mchakato wa maisha ya kila siku ili kukidhi mahitaji yao msingi kiasi cha kutumbukia katika ulaji wa kupindukia na kusahau kukesha ili kumngojea Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, ulaji wa kupindukia pamoja na kutopea katika malimwengu ni “Virusi” vinavyowashambuliwa sana watu wa Mungu, kiasi cha kujitafuta wao wenyewe na hivyo kumsahau Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao. Kwa bahati mbaya watu wanazama sana katika ubinafsi wao na kusahau jirani wanaoendelea kubisha hodi, kiasi kwamba, wanaonekana kuwa kama kero. Zote hizi ni dalili za ubinafsi na mambo hatari sana kwa imani. Ikumbukwe kwamba, hatari ya kweli si maadui wakubwa, chuki na dhuluma mbali mbali.

Adui mkubwa wa imani ni ulaji wa kupindukia, usioguswa na mahangaiko wala kilio cha jirani. Vitu vinapewa uzito wa kwanza badala ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Leo hii nyumba zimejaa vitu, lakini hakuna watoto, kielelezo cha kipindi cha ukame wa watoto Barani Ulaya. Watu wanao muda kibao wa “kujinafsi na kujibovusha” lakini hawana hata kidogo muda kwa ajili ya Mungu na jirani zao. Kutokana na watu kupenda na kuthamini sana vitu na matokeo yake, husuda, wivu na kijicho vimeingia ulimwenguni. Mambo kama haya, anasema Baba Mtakatifu yanatishia amani na usalama wa watu wa Mungu kwa sababu kamwe mwanadamu hawezi kutosheleza tamaa zake. Uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka yamekuwa ni chanzo cha vita, ghasia na uvunjifu wa haki na amani. Liturujia la Neno la Mungu Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Majilio inawaalika waamini kukesha, ili wasitumbukie katika usingizi na Mwenyezi Mungu akawakuta wakiwa wamelala.

Kukesha anasema Baba Mtakatifu ni sehemu ya mchakato wa kushinda vishawishi, kwa kujenga matumaini sanjari na kutambua kwamba, iko siku Mwenyezi Mungu atakuja tu! Lakini ikumbukwe kwamba sala na matendo ya huruma yanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee wakati huu wa kipindi cha Majilio, chemchemi ya matumaini na furaha ya kweli katika maisha ya waamini. Baba Mtakatifu anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumfungulia Mungu na jirani zao malango ya maisha yao, ili aweze kuwakirimia amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, iwafikirishe watu wa Mungu kutoka DRC, jinsi ambavyo amani inatishiwa kutokana na uwepo wa vita. Leo hii eneo la Mashariki mwa DRC na hasa huko Beni na Minembwe hali ni mbaya sana kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo inachochewa kwa kiasi kikubwa na mahasimu kutoka nje ya DRC.

Hii ni vita inayoendeshwa na watu wanaotaka utajiri wa haraka haraka na faida kubwa kutokana na biashara ya silaha duniani! Utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa watu hawa kwao si mambo ya kuzingatiwa. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko amemkumbuka Mwenyeheri Sr. Marie- Clementine Anwarite Nengapeta maana yake “utajiri si mali kitu” aliyezaliwa kunako tarehe 29 Desemba 1939 huko Wamba, nchini DRC. Kunako mwaka 1959 akajiunga na Shirika la Watawa wa Familia Takatifu. Na kunako mwaka 1964 kutokana na chuki dhidi ya imani akauwawa kikatili tarehe 1 Desemba 1964. Huyu alikiwa ni mtawa wa shoka aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini DRC kiasi kwamba, akawa ni chemchemi ya furaha na matumaini ya maisha mapya! Wakati akiwa kufani anasema Baba Mtakatifu Francisko akawasamehe watesi na wauaji wake kwani walikuwa wanatenda yote haya bila kufahamu.

Baba Mtakatifu anawaaomba watu wa Mungu kikimbilia ulinzi na maombezi ya Mwenyeheri Sr. Marie- Clementine Anwarite Nengapeta awaombee upendo ambao ni Mungu mwenyewe. Kwa msaada wa nchi jirani, DRC isikubali kuwa ni soko la silaha kwa ajili ya vita na machafuko. Matumaini yao kwa siku za mbeleni yajengeke kwenye utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana. Umefika wakati wa kuongoa uchumi unaofumbatwa katika biashara haramu ya silaha kwa kujielekeza katika uchumi fungamani unaosimikwa katika msingi wa amani! Mwenye masiko na asikie!

Papa: Misa DRC

 

01 December 2019, 15:43