Tafuta

Papa Francisko anazitaka asasi za kiraia zenye mwelekeo wa Kikatoliki kujizatiti kuyafahamu Mafundisho Jamii ya Kanisa ili kuchangia zaidi ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Papa Francisko anazitaka asasi za kiraia zenye mwelekeo wa Kikatoliki kujizatiti kuyafahamu Mafundisho Jamii ya Kanisa ili kuchangia zaidi ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. 

Papa Francisko: Asasi za kiraia za Kikatoliki: Mafundisho Jamii ya Kanisa ni muhimu!

Jukwaa la IV la Asasi za Kiraia zenye mwelekeo wa Kikatoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia, tarehe 7 Desemba 2019 zimekutana mjini Vatican ili kutafakari kwa pamoja tema zinazohusiana na mafungamani ya kijamii, ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa jamii jumuishi, ili hata maskini na wanyonge katika jamii waweze kujisikia kuwa wako nyumbani:Muhimu ni: Majiundo, Ujasiri na Umoja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 7 Deseamba 2019 amekutana na kuzungumza na wajumbe waliokuwa wanashiriki katika Jukwaa la IV la Asasi za Kiraia zenye mwelekeo wa Kikatoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kutafakari kwa pamoja tema zinazohusiana na mafungamani ya kijamii, ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa jamii jumuishi, ili hata maskini na wanyonge katika jamii waweze kujisikia kuwa wako nyumbani. Huu ni uzoefu na mang’amuzi yanayotekelezwa kwa kuzingatia mazingira ya mahali ya nchi wanamotoka pamoja na mazingira ya kimataifa katika ujumla wake. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amekazia umuhimu wa asasi hizi kujikita katika majiundo; pili ni watu kupata mahitaji yao msingi na hatimaye, ni kutekeleza sera na mikakati hii kwa kushikamana kwa pamoja kama timu  mmoja. Baba Mtakatifu anasema, wajumbe wengi kati yao ni watu ambao wanashiriki kwa hali na mali katika majadiliano kuhusu: haki msingi za binadamu, maboresho ya hali ya maisha, makazi, elimu, maendeleo fungamani, matatizo na fursa mbali mbali wanazoweza kutumia kama kielelezo makini kinachoonesha mahusiano kati ya Kanisa na Ulimwengu, pamoja na Kanisa linaloishi na kutenda kazi pamoja na walimwengu.

Katika muktadha kama huu, Kanisa linaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa njia ya ushirikiano na taasisi za kimataifa. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanafafanua vizuri zaidi kuhusu ushirikiano wa Wakristo katika taasisi za kimataifa katika mchakato wa ujenzi wa amani na udugu wa kibinadamu. Ndiyo maana taasisi kama hizi hazina budi kuimarishwa ili kuongeza idadi ya wanachama wake wenye malezi mazuri; kwa kutoa msaada na kuratibu nguvu zake kwa namna inayofaa. Kwa sababu mafanikio katika utendaji na majadiliano ni mambo yanayodai ushirikiano wa pamoja ili kufanya kazi kama timu mmoja! Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa malezi utakaowawezesha wanachama wao kutoa ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kama chachu ya majadiliano ili kuweza kupata tafakari yenye mwelekeo chanya kuhusu utu wa binadamu.

Haya ni mambo yanayohitaji imani na hali ya mtu kujiamini kwa kutambua kwamba, wao hapa duniani ni vyombo ambavyo Mwenyezi Mungu anavitumia kwa ajili ya kutekeleza mpango wake katika maisha ya mwanadamu! Kumbe ufanisi katika muktadha huu si kitu kinachopewa kipaumbele cha kwanza. Kwa upande wa pili wa shilingi, kunahitajika majiundo makini ya kitaalam, kisayansi na kiutu ili kuweza kujadili changamoto hizi katika mwono wa Kikristo. Ni katika muktadha huu, Mafundisho Jamii ya Kanisa yanatoa: sheria, kanuni na taratibu zinazopaswa kufuatwa ili kutoa huduma bora zaidi kwa binadamu. Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe wa Jukwaa la IV la Asasi za Kiraia zenye mwelekeo wa Kikatoliki kuhakikisha kwamba, wanakuwa na uelewa mpana zaidi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuyafanyia tafsiri katika utekelezaji wa miradi yao. Mafunzo na elimu makini ni njia muafaka ya kuweza kukabiliana na changamoto changamani za kijamii na kisiasa; mambo yanayopewa kipaumbele cha pekee na Mama Kanisa kwa wakati huu.

Ni kutokana na changamoto hii, Baba Mtakatifu anasema, ameamua kuunga mkono ujenzi wa  ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya elimu, kama sehemu ya mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Anatanabaisha athari za mwendokasi katika mchakato wa elimu; umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu; matumizi sahihi ya rasilimali watu sanjari na umuhimu wa kujisadaka kwa ajili ya huduma makini katika jamii. Lengo la mchakato huu ni kuhakikisha kwamba, elimu inasaidia kuwaandaa watu katika kukuza na kudumisha misingi ya haki na amani; kwa watu kupokeana jinsi walivyo pamoja na ujenzi wa mshikamano wa kimataifa, sanjari na utunzaji bora wa mazingira. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, ili kuweza kufikia malengo hayo, wanapaswa kujiamini na kuhakikisha kwamba, wanatumia kikamilifu karama, elimu na ujuzi wao kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Huu ni utajiri na amana ya Kanisa kwani Mwenyezi Mungu anaweza kuwajaza kila neema kwa wingi ili wao wakiwa na riziki ya kutosha waweze kuonesha ukarimu ili wapate kuzidi sana kwa kila tendo jema. Baba Mtakatifu anawataka wajumbe hawa kuratibu shughuli zao kwa njia ya umoja na mshikamano unaowawezesha kutekeleza majukumu haya kama timu. Hii ndiyo ile dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inayoliwezesha Kanisa kutekeleza utume wake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Jukwaa hili linapaswa kuwa ni mfano bora wa kuigwa, kwa kuunganisha nguvu katika utekelezaji wa miradi sehemu mbali mbali za dunia, huku wakishirikiana na viongozi wa Makanisa mahalia pamoja na wawakilishi wa Vatican katika nchi husika. Mwelekeo huu utakuwa ni chachu ya Injili, mwanga na nguvu kama ilivyokuwa kwa Wakristo wa Kanisa la  mwanzo. Jumuiya ya Kimataifa ina kiu ya majadiliano na ushirikiano ili kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu, daima utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza. Wajumbe watambue kwamba, Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro wanahitaji na kuthamini kazi, juhudi na ushuhuda wao katika Jumuiya ya Kimataifa.

Papa: Asasi za Kikatoliki
07 December 2019, 15:58