Tafuta

Watumishi wa Altareni kutoka Ufaransa tarehe 24-28 Agosti 2020 wanatarajiwa kukutana mubashara na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Watumishi wa Altareni kutoka Ufaransa tarehe 24-28 Agosti 2020 wanatarajiwa kukutana mubashara na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. 

Watumisi wa Altareni kutoka Ufaransa kukutana na Papa Francisko 24-28/8/2020

Papa amewatumia ujumbe Watumishi wa Altareni kutoka Ufaransa kukutana na kusali pamoja naye mjini Vatican kuanzia tarehe 24-28 Agosti 2020. Tukio limeandaliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa. Baba Mtakatifu anawapongeza Watumishi wa Altare ambao wamebahatikia kumtumikia Yesu, wakati wa Ibada na Liturujia ya Kanisa, lakini zaidi wakati wa Ibada ya Misa Takatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Familia ni mahali pa kwanza kabisa pa kuwafunda watoto misingi ya imani, matumaini, mapendo, maadili, nidhamu na utu wema. Wazazi wanapaswa kuwaangalia watoto wao kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kuwaheshimu kama binadamu, walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wawafundishe kushika Amri za Mungu zinazomwilishwa katika upendo kwa Mungu na jirani. Wazazi wawe ni mashuhuda na vyombo vya: utu wema, heshima, uaminifu, msamaha, upendo na mshikamano wa dhati. Nyumbani pawe ni mahali ambapo watoto wanafundwa fadhila njema, ili waweze kukua na kukomaa: kiakili, kiimani, kimaadili na kiutu tayari kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake! Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amewatumia ujumbe kwa njia ya video Watumishi wa Altareni kutoka nchini Ufaransa kukutana na kusali pamoja naye mjini Vatican kuanzia tarehe 24-28 Agosti 2020. Tukio hili la aina yake, limeandaliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa.

Baba Mtakatifu anawapongeza na kuwashukuru Watumishi wa Altare ambao katika hija ya maisha yao, wamebahatika sana kuweza kumtumikia Kristo Yesu, wakati wa maadhimisho ya Ibada na Liturujia ya Kanisa, lakini zaidi wakati wa Ibada ya Misa Takatifu. Hii ni fursa murua ya kumpenda na kujishikamanisha naye kwa dhati. Baada ya maadhimisho ya Misa Takatifu, waamini wote wanaalikwa na kuhimizwa kuendelea kumpenda na kumtumikia Kristo Yesu katika uhalisia wa maisha kama kielelezo na ushuhuda wa imani tendaji. Waamini wakumbuke kwamba, huu ni utume ambao wameitiwa na wanapaswa kuutekeleza. Hii itakuwa ni fursa kwa Watumishi wa Altareni kufanya hija kwenye Makaburi ya Mitume Petro na Paulo, miamba wa imani, walioitwa na kutumwa na Kristo Yesu kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kiasi hata cha kuweza kuyamimina maisha yao. Ushuhuda wao wa imani, uwatie nguvu waamini kuendelea na kudumu katika utume wao wa maisha ya Kikristo, licha ya kinzani na “madongo” wanayoweza kukumbana nayo katika maisha yao au maswali tete na nguvu wanazohitaji kutekelezea wajibu huu.

Tangu wakati huu, Baba Mtakatifu anasema, watapata fursa ya kuweza kukutana mubashara pamoja na kufahamiana na vijana wengine kutoka sehemu mbali mbali za Ufaransa, wanaoshirikishana fadhila ya imani katika hija ya maisha yao. Baba Mtakatifu anawahimiza watumishi wa Altareni, kuwakaribisha vijana wenzao wanaotaka kuiga mfao wao, ili wote waweze kufanya hija mjini Roma, kwa sababu umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Baba Mtakatifu anawakumbusha kwamba, kuanzia tarehe 24-28 Agosti 2020 anawasubiri kwa hamu kabisa mjini Roma na anapenda kutumia fursa hii kuwasindikiza katika maandalizi yao kwa njia ya sala na sadaka yake. Anawaomba pia waendelee kumkumbuka kwa sala katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Papa: Watumishi wa Altare
13 November 2019, 15:33