Tafuta

Vatican News
Kanisa Katoliki linaunga mkono jitihada za Mpango wa Chakula Duniani za kupambana na ukosefu wa usalama na uhakika wa chakula duniani. Kanisa Katoliki linaunga mkono jitihada za Mpango wa Chakula Duniani za kupambana na ukosefu wa usalama na uhakika wa chakula duniani.  (ANSA)

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani 2019

Baba Mtakatifu anapenda kuihakikishia Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, kwamba, Kanisa Katoliki linaunga mkono na linapenda kushirikiana na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, ili kuhakikisha kwamba, haki ya watu wote kupata chakula bora na chenye lishe endelevu kinapatikana kwa watu wote. Maskini wapewe kipaumbele! Baa la Njaa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Francisko anasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuibua mbinu mkakati wa kupambana na baa la njaa na utapiamlo duniani, ikiwa ni pamoja na kukuza utamaduni wa kuhifadhi chakula, ili kiweze kutumika na watu wanaoteseka kwa baa la njaa duniani. Uharibifu wa chakula duniani unaendelea kuwa ni kikwazo kikubwa cha kupambana na ukosefu wa usalama na uhakika wa chakula duniani. Hali hii haina budi kwenda sanjari na mchakato wa kuondokana na ubinafsi, uchoyo na hali ya kutojali inayoshuhudiwa katika matumizi mabaya ya chakula duniani. Katika muktadha huu, itakuwa ni vigumu kwa Jumuiya ya Kimataifa kuweza kufikia Malengo yaliyobainishwa kwenye Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, Cop21 uliofanyika mjini Paris, nchini Ufaransa, mwaka 2015 sanjari na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Utekelezaji wa dhamana hii anasema Baba Mtakatifu ni wajibu wa watu wote bila ubaguzi.

Vyombo vya mawasiliano ya jamii vina wajibu wa kuelimisha na kuragibisha kuhusu umuhimu wa kutunza chakula ili kukidhi mahitaji ya watu wengi zaidi. Mapambano dhidi ya baa la njaa yanapaswa kuvaliwa njuga na watu wote wa Mungu, kwani njaa inaendelea kusigina utu, heshima na haki msingi za binadamu, hasa miongoni mwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu aliomwandikia Bwana David Beasley Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP., na Bodi ya Wakurugenzi katika mkutano wao wa pili wa kawaida wa Mwaka uliofunguliwa Jumatatu, tarehe 18 Novemba na unatarajiwa kuhitimishwa tarehe 21 Novemba 2019. Hivi karibuni, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, limeanzisha kampeni maalum ya utunzaji wa chakula, ili kuokoa maisha ya watu sanjari na kusaidia mchakato wa maendeleo fungamani, kwa kuwa na uhakika na usalama wa chakula kwa watu wengi zaidi.

Baba Mtakatifu anawaalika watu wote wenye mapenzi mema kuunganisha nguvu zao, kwa kufanya mabadiliko katika mtindo wa maisha kwa kukipatia chakula umuhimu unaostahili; kwa kuangalia uzalishaji unaotolewa na Dunia Mama na athari zake katika maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu anapenda kuihakikishia Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, kwamba, Kanisa Katoliki linaunga mkono na linapenda kushirikiana na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, ili kuhakikisha kwamba, haki ya watu wote kupata chakula bora na chenye lishe endelevu kinapatikana kwa watu wote. Baba Mtakatifu anasema, kampeni hii isaidie kuwapatia chakula watu wanaoathirika kutokana na ukosefu wa chakula na lishe bora. Kampeni hii inapaswa kupewa kipaumbele katika sera na maamuzi ya kiuchumi; amani, ustawi na maendeleo ya wengi; kama njia ya kufahamiana, msingi thabiti wa maendeleo fungamani ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu anawaombea ili kwamba, sadaka na majitoleo yao yasaidie kuleta ari na mwamko mpya wa kujenga dunia mpya inayosimikwa katika udugu, haki na amani. Wachunguzi wa mambo wanasema,  Bwana Beasley anaonesha utashi wa kisiasa wa kuweza kufikia lengo la kutokomeza njaa duniani kadiri ya mpango mkakati wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030.

Papa: WFP 2019

 

18 November 2019, 14:41