Tafuta

Vatican News
Papa Francisko amemtumia Patriaki Bartolomeo wa kwanza ujumbe wa matashi mema wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Andrea, Mtume. Papa Francisko amemtumia Patriaki Bartolomeo wa kwanza ujumbe wa matashi mema wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Andrea, Mtume. 

Ujumbe wa Papa Francisko: Siku kuu ya Mtakatifu Andrea, Mtume!

Wakristo hawana sababu msingi ya kuendelea kutengana. Hii ni changamoto iliyotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 30 Novemba 1979 na inapaswa kujibiwa na waamini kwa kupyaisha mielekeo pamoja na matendo yao. Majadiliano ya kiekumene yamwilishwe katika uhalisia wa maisha ya waamini, kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja katika Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Vatican ukiongozwa na Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo, tarehe 30 Novemba 2019, umeshiriki katika maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Andrea Mtume, inayopewa kipaumbele cha pekee na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol kama msimamizi wa Kanisa hilo. Liturujia Takatifu imeongozwa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza na ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya ukasomwa na  Kardinali Kurt Koch ambaye pia ameshiriki katika mazungumzo na Tume ya Sinodi ya Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol pamoja na Kanisa Katoliki. Mtakatifu Andrea ndiye aliyeitwa wa kwanza na Kristo Yesu na hatimaye, kumshikirisha wito huu ndugu yake Petro, wote wawili wakajisadaka kwa ajili ya kutangaza na kuhubiri Habari Njema ya Wokovu! Ushiriki wa Vatican katika maadhimisho haya kila mwaka ni sehemu ya utamaduni wa Makanisa haya mawili, kama kielelezo cha umoja na chachu ya kusonga mbele katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kuvunjilia mbali uhasama, kinzani na ukimya uliotawala kati ya Makanisa haya mawili kwa miongo kadhaa iliyopita.

Roho Mtakatifu chemchemi ya umoja, ndiye aliyewawezesha kuanza tena mchakato wa majadiliano ya udugu na upendo. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake amewatakia matashi mema. Baraka na neema kutoka mbinguni katika maadhimisho ya Siku kuu hii; kumbu kumbu ya Miaka 48 ya Tume ya Pamoja ya Kitaalimungu Kimataifa kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox; Mchakato wa majadiliano ya kiekumene katika ujenzi wa umoja, urafiki na udugu. Baba Mtakatifu katika salam zake, amewatakia heri na baraka tele waamini wote walioshiriki katika Liturujia Takatifu ya kumtukuza Mwenyezi Mungu na kumtakasa mwanadamu na kwamba, kwa pamoja wamepania kusonga mbele na mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili siku moja Wakristo wa Makanisa ya Mashariki na Magharibi waweze kuungana na kuwa wamoja! Tume ya Pamoja ya Kitaalimungu Kimataifa kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox inaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 48 tangu kuundwa na hatimaye, kuzinduliwa kwake na Mtakatifu Yohane Paulo II pamoja na Patriaki Dimitrios wa kwanza katika kumbu kumbu ya Siku kuu ya Mtakatifu Andrea, Mtume.

Katika kipindi cha miaka yote hii, Tume hii imepiga hatua kubwa na kwamba, ana matumaini makubwa kwa siku za mbeleni. Kwa heshima na taadhima amemkumbuka Askofu mkuu Stylianos ambaye kwa miaka mingi alikuwa ni Mwenyekiti mwenza wa Tume hii kutoka katika Kanisa la Kiorthodox, ambaye hivi karibuni, ametangulia mbele ya haki ili kuungana na wale ambao wamejiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Wakristo hawana sababu msingi ya kuendelea kutengana. Hii ni changamoto iliyotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 30 Novemba 1979. Changamoto hii inapaswa kujibiwa na waamini kwa kupyaisha mielekeo pamoja na matendo yao. Ikumbukwe kwamba, mchakato wa ujenzi wa umoja wa Wakristo si tu kwamba, unakita mizizi yake katika majadiliano ya kitaalimungu bali pia unapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini, kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja katika Kristo Yesu.

Wakristo wanapaswa kuonesha na kushuhudia uaminifu kwa Neno la Mungu, kwa kupendana kama kielelezo makini cha maisha ya Kikristo. Wakristo wanakumbushwa kwamba, upendo ni matunda ya Roho Mtakatifu anayewaongoza na kuwapatia dira. Ujirani mwema ushuhudiwe pia katika maisha ya sala kwa waamini kuombeana na kusali kwa pamoja. Uhusiano na udugu wao wa Kikristo anasema Baba Mtakatifu Francisko unapaswa kukua na kukomaa kwa kuendelea kuwa watiifu kwa Kristo Yesu, Mfufuka aliyewaita na kuwatuma wafuasi wake kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, huku wakizamisha ushuhuda wao katika huduma kwa maskini na wahitaji zaidi, jambo ambalo linatekelezwa kwa pamoja na Makanisa haya mawili. Baba Mtakatifu anaendelea kuhimiza majadiliano ya upendo na maisha kwa kushirikishana sera na mikakati ya maisha ya kiroho, kichungaji, kitamaduni pamoja na utekelezaji wa miradi ya huduma. Baba Mtakatifu anahitimisha salam na matashi mema kwa waamini wa Kanisa la Kiorthodox katika maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Andrea Mtume kama kielelezo cha furaha inayobubujika kutoka katika undani wa maisha yake.

Papa: Mt. Andrea
30 November 2019, 16:36