Tafuta

Vatican News
Itifaki ya Montreal ya Mwaka 1987 ni mkataba wa kimataifa unaodhibiti uzalishaji na usambazaji wa bidhaa zenye kemikali zinazomong'onyoa tabaka la hewa ya ozoni angani. Itifaki ya Montreal ya Mwaka 1987 ni mkataba wa kimataifa unaodhibiti uzalishaji na usambazaji wa bidhaa zenye kemikali zinazomong'onyoa tabaka la hewa ya ozoni angani.  (2019 Getty Images)

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Mkutano wa Itifaki ya Montreal 1987

Itifaki ya Montreal ya Mwaka 1987 inapaswa kuzingatia: Ushirikiano wa Jumuiya ya Kimataifa katika medani mbali mbali za maisha: Umuhimu wa ustawi, maendeleo na mafao ya kizazi cha sasa na kile kijacho. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunza kudhibiti matumizi ya teknolojia, kwa kuyaelekeza katika mchakato wa maendeleo fungamani kwa kuzingatia utu na mafao ya kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Itifaki ya Montreal ya Mwaka 1987 “Montreal Protocol of 1987” ni Mkataba wa Kimataifa ulioridhiwa na Jumuiya ya Kimataifa ili kudhibiti uzalishaji na usambazaji wa bidhaa zenye kemikali zinazomong’onyoa tabaka la hewa ya ozoni angani,  ambayo ni muhimu sana katika kudhibiti kiwango cha mionzi ya jua inayotua ardhini. Ozoni ni hewa iliyoko kwenye angahewa ya juu, takribani kilometa 10 hadi 50 juu ya ardhi. Kazi yake kubwa ni kuchuja sehemu kubwa ya mnururisho wa mionzi kama “Ultraviolet B” isifike kwenye uso wa dunia. Itifaki hii pamoja na mambo mengine inapania kuhamasisha ushirikiano wa Jumuiya ya Kimataifa katika kuratibu shughuli mbali mbali za binadamu zinazotishia kuharibu tabaka la hewa ya ozoni angani na hivyo kuchochea kuongezeka kwa joto duniani. Itifaki imepata mafanikio makubwa katika Jumuiya ya Kimataifa kama sehemu ya mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwa kudhibiti uzalishaji wa hewa ya ukaa ambayo ina madhara makubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Itifaki imekuwa ikiboreshwa mara kwa mara kuendana na tafiti mbali mbali za sayansi na maendeleo ya teknolojia na kwa mara ya mwisho maboresho hayo yalifanyika mjini Kigali, Rwanda, kunako mwaka 2016. Takwimu zinaonesha kwamba,  kuna nchi 197 ambazo zimeridhia Itifaki ya Montreal ya Mwaka 1987 na Sudan ya Kusini ni nchi ya mwisho kuridhia Itifaki hii kunako mwaka 2012. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, amewatumia ujumbe washiriki wa Mkutano wa 31 wa Itifaki ya Montreal ya Mwaka 1987 kwa kutambua kwamba, Itifaki hii imekuwa na mchango mkubwa katika kudhibiti uchafuzi wa mazingira pamoja na kuhamasisha sera na mikakati ya maendeleo fungamani ya binadamu. Miaka thelathini na moja, imeyoyoma tangu wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa walipokutana huko Vienna, Austria, tarehe 22 Machi 1985 na kutia saini makubaliano yaliyojikita katika mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa. Tafiti za kisayansi zinaonesha kwamba, tabaka la ozoni linaendelea kumong’onyoka.

Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuzingatia mambo makuu yafuatayo: Ushirikiano wa Jumuiya ya Kimataifa katika medani mbali mbali za maisha; Changamoto ya kitamaduni inapaswa kushughulikiwa kwa kuzingatia pia kanuni maadili ndiyo maana Vatican pia imeonesha nia ya kuridhia itifaki hii. Jumuiya ya Kimataifa ielekeze sera na mikakati yote kwa kutambua kwamba, ni sehemu ya ekolojia fungamani katika maendeleo ya mwanadamu. Tangu Itifaki ya Montreal ya Mwaka 1987 ilipopitishwa na Jumuiya ya Kimataifa, mambo yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa zaidi, mosi ni ushirikiano wa Jumuiya ya Kimataifa katika medani mbali mbali za maisha yaani: wanasayansi, wanasiasa, wachumi, wazalishaji viwandani pamoja na raia katika ujumla wao. Ushirikiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa yanaweza kuleta mafanikio makubwa katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwa kuwajibika pamoja na kudumisha umoja na mshikamano, muhimu kwa ustawi, maendeleo na mafao ya kizazi cha sasa na kile kijacho.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunza kudhibiti matumizi ya teknolojia, kwa kuyaelekeza katika mchakato wa maendeleo fungamani kwa kuzingatia utu na mafao ya kijamii. Ingawa katika historia zama za viwanda zinaonekana kuwa ni zama ambazo hazikuwajibika kuhusiana na mazingira, hata hivyo kuna kila sababu ya kuleta matumaini kwa karne ya ishirini na moja, ili binadamu akumbukwe kwa kujifunga kibwebwe kupambana na uharibifu wa mazingira. Changamoto ya kitamaduni inapaswa kushughulikiwa kwa kuzingatia pia kanuni maadili, majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kusikilizana, ili kujenga umoja na mshikamano unaofumbatwa katika kipaji cha ubunifu, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Dunia mama! Maboresho ya Itifaki ya Montreal ya Mwaka 2016 yaliyofanyika mjini Kigali, nchini Rwanda yanapania kudhibiti uzalishaji wa kemikali ambazo zitaendelea kumong’onyoa tabaka la hewa ya ozoni angani. Vatican imeonesha nia ya kutaka kuridhia Itifaki ya Montreal ili kuendelea kuchangia katika wajibu wake wa kimaadili katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, matatizo na changamoto mbali mbali za utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote zinaingiliana. Kuna uhusiano wa karibu kati ya ongezeko la joto duniani na kumong’onyoka kwa tabaka la hewa ya ozoni angani. Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kujielekeza zaidi katika sera na mikakati ya maendeleo fungamani ya binadamu. Elimu makini haina budi kutolewa kwenye vituo vya elimu na utamaduni, mahali wanapoandaliwa wanasiasa, wanasayansi na raia, ili hatimaye, waweze kuwajibika barabara katika maamuzi yao. Ustawi, mafao ya wengi sanjari na maendeleo fungamani yasaidie kuleta maboresho makubwa katika maisha ya watu. Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa washiriki wa Mkutano wa 31 wa Itifaki ya Montreal ya Mwaka 1987 kwa kuhimiza majadiliano yanayopania kuiwajibisha Jumuiya ya Kimataifa katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yanapaswa kuzingatia pia kanuni maadili na utu wema kwa kuwa na uelewa mpana zaidi na kwamba, maendeleo fungamani ya binadamu ni muhimu sana.

Papa: Itifaki ya Montreal 1987

 

07 November 2019, 13:07