Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asikitishwa sana na mauaji ya kinyama nchini Burkina Faso, anawasihi wadau mbali mbali kujielekeza katika majadiliano ya kidini. Papa Francisko asikitishwa sana na mauaji ya kinyama nchini Burkina Faso, anawasihi wadau mbali mbali kujielekeza katika majadiliano ya kidini. 

Papa Francisko asikitishwa na mauaji nchini Burkina Faso

Baba Mtakatifu Francisko anawasihi viongozi wa Serikali, kidini na kiraia pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini Burkina faso kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha ari na moyo wa udugu wa kibinadamu, kwa kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini, ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Ujenzi wa udugu wa kibinadamu ni muhimu sana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya katekesi yake, ameyaelekeza mawazo yake nchini Burkina Faso ambako hivi karibuni kumekuwepo na mashambulizi ambayo yamepelekea zaidi ya watu 100 kupoteza maisha. Baba Mtakatifu anawaombea marehemu wote na kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo. Anawaombea pia wale wote waliojeruhiwa na wale ambao kwa sasa hawana makazi tena baada ya nyumba zao kubomolewa. Anawasihi viongozi wa Serikali, kidini na kiraia pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha ari na moyo wa udugu wa kibinadamu, kwa kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini, ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa mkwaju kati yake na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu ni mwaliko kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba, binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hati ya Udugu wa Kibinadamu inapata chimbuko lake katika mikutano elekezi iliyowasaidia waamini wa dini hizi mbili kushirikishana: furaha, majonzi, matamanio yao halali pamoja na changamoto mamboleo. Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini kwamba, wajitahidi kumwomba Roho Mtakatifu, ili awakirimie nguvu na ujasiri wa kuwa na ukarimu, hatimaye waweze kumfungulia Kristo Yesu malango ya maisha yao kwa kujenga na kudumisha umoja wa kidugu kama ushuhuda wa imani tendaji; matumaini na mapendo thabiti! Familia za Kikristo ziwe kweli ni mashuhuda wa Mungu ambaye ni Muumbaji na Mkombozi.

Nyumba na familia za Kikristo daima ziwe ni mahali pa kumwilisha fadhila ya upendo, kwa kusikiliza na kutafakari Neno la Mungu, ili kukuza na kudumisha imani, matumaini na Injili ya maisha mapya. Ukarimu wao, uwe ni cheche za ushuhuda wa Kikristo kwa watu mbali mbali wanaokutana nao. Ushuhuda huu ukite mizizi yake katika fadhila ya unyenyekevu pasi na kutafuta makuu. Baba Mtakatifu amewapongeza watu wa Mungu kutoka Jamhuri ya Watu wa Czech kwa kuadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 30 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipomtangaza Mwenyeheri Agnese kuwa Mtakatifu. Huu ni mwaliko wa kupyaisha ari na mwamko wa Kiinjili, kwa kuendelea kusimama kidete kulinda na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na ushuhuda wenye mvuto, ili watu wengi waweze kumfahamu, kumpenda na hatimaye, kumtumikia Mwenyezi Mungu. Huduma kwa maskini ni mfano bora wa kuigwa kama kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya upendo. Mwishoni mwa katekesi yake, Baba Mtakatifu Francisko amewaalika waamini kumkumbuka katika sala na sadaka zao, wakati huu anapojiandaa kwa ajili ya hija ya kitume nchini Thailand na Japan kuanzia tarehe 19-26 Novemba 2019.

Papa: Burkina Faso

 

13 November 2019, 15:50