Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano yaliyoandikwa kitabu na Gianni Valente anakiri kwamba, Kanisa bila Kristo Yesu, haliwezi kamwe kufua dafu! Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano yaliyoandikwa kitabu na Gianni Valente anakiri kwamba, Kanisa bila Kristo Yesu, haliwezi kamwe kufua dafu!  ( Hiata Anderson Flores | Rodrigo Souza Lopes Ernesto)

Papa Francisko asema, Kanisa bila Kristo Yesu halifui dafu!

Amri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kila kiumbe ni utume wa kimisionari na ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Bila kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, Kanisa litabaki kuwa kama “Chama cha Maisha ya kiroho” kinachoshindwa kutoa nafasi kwa Kristo Yesu ili kuendelea kukutana na waja wake, katika hija ya maisha yao ya ndani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wake wa kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” anasema, furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Yesu. Wale wanaoikubali zawadi yake ya ukombozi wanawekwa huru kuondokana na dhambi, uchungu, utupu wa ndani na upweke hasi. Pamoja na Kristo daima furaha inazaliwa upya. Wosia huu ni mwongozo wa maisha na utume wa Kanisa katika kutangaza na kushuhudia Furaha ya Injili katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu aliutangaza Mwezi Oktoba 2019, kuwa ni mwezi maalum uliotengwa na Mama Kanisa kwa ajili ya kuhamasisha ari na mwamko wa kimisionari duniani, kwa mwaka huu 2019, Kanisa linapoadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume "Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari.” Papa Benedikto XV katika Waraka huu, alifungua rasmi ukurasa mpya wa maisha na utume wa Kanisa mintarafu shughuli za kimisionari, kwa kulitaka Kanisa kuanzisha mchakato wa majiundo na malezi kwa ajili ya kuyategemeza Makanisa mahalia kwa rasilimali watu, yaani mihimili ya uinjilishaji! Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 umeongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa”: Kanisa la Kristo katika utume.”

Maadhimisho haya yamekwenda sanjari na maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, ambayo imekazia umuhimu wa: Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, wongofu wa kitamaduni unaojikita katika mchakato wa utamadunisho; wongofu wa kiekolojia; wongofu wa kijamii kwa kuheshimu utu na utambulisho wa watu mahalia. Na kwamba, wongofu wa kichungaji, uwawezeshe wananchi wa Ukanda wa Amazonia kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na  Gianni Valente kama sehemu ya hitimisho la Maadhimisho ya Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019; mahojiano ambayo yameandikiwa kitabu anakiri kwamba, bila ya uwepo wa Kristo Yesu, Kanisa haliwezi kufanya chochote kile. Haya ni mahojiano ya jinsi ambavyo waamini wanapaswa kuwa wamisionari katika ulimwengu mamboleo. Tangu mwanzo wa maisha yake kama kijana Baba Mtakatifu Francisko, alitamani sana kwenda nchini Japan ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, lakini hakufanikiwa hata mara moja, lakini hii ikawa ni sehemu ya mchakato wa kutoka katika ubinafsi wake ili kwenda kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa.

Hii ni amri kutoka kwa Kristo Yesu kwa wafuasi wake, kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kila kiumbe na kwamba, utume wa kimisionari ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Bila kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, Kanisa litabaki kuwa kama “Chama cha Maisha ya kiroho” kinachoshindwa kutoa nafasi kwa Kristo Yesu ili kuendelea kukutana na waja wake, katika hija ya maisha yao ya ndani. Kwa njia ya nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, Kanisa linahamasishwa kutoka na kuwaendea watu wake kwani Roho Mtakatifu ndiye mhusika mkuu wa mchakato wa uinjilishaji kama ilivyokuwa hata katika Kanisa la Mwanzo mintarafu Matendo ya Mitume. Kwa nguvu ya Roho Mtakatifu waamini wakaongezeka na Kanisa likaendelea kuimarika. Roho Mtakatifu ameendelea kuliongoza na kulisindikiza Kanisa katika maisha na utume wake. Akalisimamisha imara na thabiti wakati wa madhulumu kama ilivyokuwa wakati wa Mtakatifu Stefano, Shahidi wa kwanza kuyamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Damu ya mashuhuda wa imani sehemu mbali mbali za dunia, imekuwa ni mbegu ya Ukristo kama wanavyosema Mababa wa Kanisa. Wakristo waliobatizwa na kuimarishwa kwa Roho Mtakatifu wanapokea dhamana na utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sehemu mbali mbali za dunia.

Kanisa linapaswa kuwa ni chombo na shuhuda wa furaha ya Injili, kwa njia ya mvuto wenye mashiko na wala si kwa kufanya wongofu wa shuruti. Hii ndiyo changamoto inayopaswa kutekelezwa na wamisionari katika maisha na utume wao. Watu waguswe na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hii ndiyo namna bora zaidi ya kudhihirisha kwa nje neema ya ndani kutoka kwa Roho Mtakatifu na kwamba, huruma ndiyo fadhila kubwa kushinda nyingine zote. Kwa hakika, bila ya Kristo Yesu, wafuasi wake, hawawezi kufua dafu! Kanisa linakua na kupanuka kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kimsingi wongofu wa shuruti unakinzana na ari na mwamko wa majadiliano ya kidini na kiekumene. Wongofu wa shuruti ni kitendo kinachowakosea haki wahusika kwa kuingilia uhuru na utashi wao. Baba Mtakatifu anaonya kwamba, hata leo hii, Kanisa lisipokuwa makini, linaweza kujikuta likitumbukia katika wongofu wa shuruti unaotekelezwa Parokiani, kwenye vyama vya kitume pamoja na kwenye Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume!

Habari Njema ya Wokovu inapaswa kutangazwa na kushuhudiwa kama cheche ya imani, matumaini na mapendo kwa watu wa Mungu, ili wote waweze kuokolewa. Huu ni mwaliko kwa viongozi wa Kanisa kuondoa vikwazo vinavyowazuia watu wa Mungu kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Watu wote wana uwezo wa kupokea na kukumbatia tunu msingi za Injili kama walivyoshuhudia hata Mababa wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Heri za Mlimani ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kama chemchemi ya kuyatakatifuza malimwengu, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Heri hizi zinakwenda sanjari na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama sehemu ya vinasaba na utambulisho wa Wakristo. Hii ni sehemu ya Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu anakaza kusema kwamba, Kanisa linawajibika kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili; kwa kusimama kidete katika wongofu wa kitamaduni unaothamini tamaduni, mila na desturi njema za watu mahalia. Kwa njia hii, Kanisa linapaswa pia kupambwa kwa tunu msingi kutoka katika tamaduni mbali mbali “Sposa ornata monilibus suis”.

Kuna uhusiano mkubwa sana kati utume na ushuhuda wa imani kama sehemu ya mchakato wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Ushuhuda wa imani ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu uliomiminwa ndani ya moyo wa mwamini, kiasi kwamba, yuko tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kushuhudia imani yake kwa Kristo na Kanisa lake. Kifo dini ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ushuhuda wa imani. Haya ndiyo yanayoendelea kushuhudiwa hata leo hii kwa Wakristo sehemu mbali mbali za dunia kuteswa, kudhulumiwa na hatimaye kuuwawa kikatili, kwa sababu ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, kila siku ya maisha yao, wanajitahidi kuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hata leo hii, kuna mambo makubwa na mazito yanayotekelezwa na wamisionari sehemu mbali mbali za dunia, lakini wao wenyewe hawayakumbuki tena, lakini Baba Mtakatifu anasema, waamini wanaendelea kuyakumbuka mambo haya na kwamba, yamehifadhiwa mahali pa salama machoni mwa Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kuendelea kujikita zaidi katika utekelezaji wa mambo makuu manne: Mosi, waamini wajitahidi kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Tafakari ya Neno la Mungu na Maisha ya Sala. Pili ni ushuhuda wa wamisionari watakatifu, wafiadini na waungama imani, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Tatu ni majiundo makini, endelevu na fungamani ya kimisionari kwa kujikita katika: Biblia, Katekesi, Tasaufi na Taalimungu. Nne, ni huduma ya upendo kama kielelezo cha Injili ya upendo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, kama kielelezo makini cha imani tendaji! Huu ni muda muafaka wa furaha ya Injili  kuendelea kutangazwa na kushuhudiwaa, Sakramenti za Kanisa kuadhimishwa na Wakristo kutoa ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake pamoja na kuendelea kujikita katika Tafakari ya Neno la Mungu, taa ya mapito ya watu wa Mungu hapa duniani.

Papa: Umisionari

 

05 November 2019, 15:17