Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio mwaka 2019 anatembele Madhabahu ya Wafranciskani huko Greccio, Pango la kwanza la Noeli kutengenezwa na Mt. Francisko wa Assisi. Papa Francisko: Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio mwaka 2019 anatembele Madhabahu ya Wafranciskani huko Greccio, Pango la kwanza la Noeli kutengenezwa na Mt. Francisko wa Assisi. 

Papa Francisko: Kipindi cha Majilio: Madhabahu ya Greccio

Papa Francisko, Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio atakwenda kutembelea katika Madhabahu ya Wafranciskani huko Greccio, Rieti, Mkoani Lazio, Italia, ili kusali kwenye Pango la kwanza kabisa la Noeli lililotengenezwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi. Atatumia nafasi hii kuwaandikia waamini na watu wote wenye mapenzi mema maana ya Pango la Noeli katika maisha ya Wakristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kipindi cha Majilio ni muhtasari wa katekesi ya historia nzima ya kazi ya ukombozi iliyotekelezwa na Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Jumapili ya kwanza ya kipindi cha Majilio inaufungua rasmi Mwaka Mpya wa Kanisa, hija ya maisha ya imani, matumaini na mapendo; inayowakumbusha waamini, Fumbo la Umwilisho na Siku ya ile ya mwisho, Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu, kama waamini wanavyosali katika Kanuni ya Imani na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Na huu ndio ukamilifu wa kazi ya uumbaji.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano, tarehe 27 Novemba 2019 amesema, Jumapili ijayo tarehe 1 Desemba 2019, Kanisa litafungua Mwaka Mpya wa Kanisa kwa kwa kuadhimisha Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio. Baba Mtakatifu anasema, atatumia fursa hii kwenda kutembelea katika Madhabahu ya Wafranciskani huko Greccio, Rieti, Mkoani Lazio, Italia, ili kusali kwenye Pango la kwanza kabisa la Noeli lililotengenezwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi. Atatumia nafasi hii kuwaandikia waraka wa kitume waamini na watu wote wenye mapenzi mema maana ya Pango la Noeli katika maisha ya Wakristo. Baba Mtakatifu amewatakia waamini na watu wote wenye mapenzi mema maandalizi bora ya kiroho na kimwili, ili kuweza kuingia kikamilifu katika Kipindi cha Majilio, huku wakiwa na moyo unaosheheni matumaini na furaha kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii pia kuwaalika waamini na mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kumjalia neema na baraka hata akaweza kukamilisha hija yake ya kitume Barani Asia kwa kutembelea Thailand na Japan. Anawaomba waendelee kumkumbuka na kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Anawataka waamini kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu; kwa kushikamana kwa pamoja ili kulijenga na kulidumisha Kanisa. Bikira Maria, msaada wa Wakristo awasimamie na kuwalinda kwa tunza na ulinzi wake wa daima. Waamini wanakumbushwa kwamba, Kristo Yesu amewaahidia kwamba, ataendelea kuandamana nao hadi ukamilifu wa dahali. Huu ni mwaliko wa kusonga mbele kwa imani na matumaini, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa watu. Kristo anaendelea kuchakarika usiku na mchana akiwatafuta waja wake, ili apate kuwaokoa na kuwaonjesha huruma na upendo wake usiokuwa na kifani.

27 November 2019, 16:25