Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko asema, wongofu wa dhati ni neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko asema, wongofu wa dhati ni neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Wongofu wa dhati ni matunda ya neema ya Mungu

Wongofu wa dhati ni matunda ya neema ya Mwenyezi Mungu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, maana Kristo Yesu alikufa kwa ajili ya watu wote na wito halisi wa binadamu ndio mmoja, ule wa kimungu. Kwa hiyo lazima waamini wawe na wazo kwamba Roho Mtakatifu anawajalia watu wote uwezekano wa kushiriki fumbo la kipasaka, kwa jinsi anavyoijua Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano ni Mama ya Makanisa yote ulimwenguni na kichwa cha Makanisa yote ya Jimbo kuu la Roma, lililowekwa wakfu na Papa Silvester kunako tarehe 9 Novemba mwaka 324. Haya ni matunda ya uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu, sehemu ya haki msingi za binadamu, uliotolewa kwa Wakristo kuabudu kadiri ya dini na imani yao na Mfalme Costantino kunako mwaka 313. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya Kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, aliwashukuru na kuwapongeza watu wa Mungu wanaoishi na kufanya shughuli zao mjini Roma na kwamba, siri ya mafanikio na upyaisho wa maisha yao ni mambo yanayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, chemchemi ya maisha mapya! Mwenyezi Mungu yuko tayari kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wote wamwombao kwa dhati.

Kumbe, ni wajibu na dhamana ya Kanisa la Roma kuwafariji na kuwatia moyo wale wote wanaosetwa na kukandamizwa kwenye kongwa la umaskini na utumwa wa dhambi kwa kwa njia ya uinjilishaji mpya. Huu ni mchakato wa ushuhuda wa maisha unaokita mizizi yake katika majadiliano kwa kuwashirikisha jirani zao ile furaha ya Injili baada ya kuutafakari upendo wa Mungu katika maisha yao. Wawe tayari kusikiliza na kujibu kilio cha maskini wa Jimbo kuu la Roma. Baba Mtakatifu amewataka wakleri wote wa Jimbo kuu la Roma kujenga na kusimika maisha na utume wao katika msingi uliokwisha kuwekwa yaani, Yesu Kristo. Wawe mstari wa mbele kuimarisha jumuiya ya waamini kwa kusikiliza Neno la Mungu; kwa kuwasaidia kupambanua vishawishi vya malimwengu, ili wawe tayari kuvikwepa na wala wasikubali kutumbukia katika ahadi hewa katika maisha, zinazoweza kuwakanganya. Waamini wawe imara katika imani kwa kuzamisha mizizi ya maisha yao ndani ya Kanisa Takatifu.

Wakleri wawe mstari wa mbele kulilinda Kanisa dhidi ya hatari za “Mbwa mwitu na walaghai”, kwa kujiaminisha kwenye hekima ya Mungu inayobubujika kutoka katika Injili ya Kristo. Hakuna njia ya mkato katika maisha ya kiroho kwani kwa wale wanaotaka kupitia njia hii, matokeo ya maporomoko ya maisha ya kiroho! Baba Mtakatifu anawataka wakleri kuendelea kuimarisha imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; wawe karibu sana na watu wa Mungu kwa njia ya ukarimu na unyenyekevu wa moyo, upendeleo na huduma makini kwa maskini; wawe ni mapango hifadhi ya furaha na majonzi ya watu wa Mungu. Waachane na ushabiki wa vyama vya kisiasa kwa kujikita zaidi katika kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Wawe na busara ya kusoma alama za nyakati ili kung’amua changamoto mamboleo na kuzipatia majibu muafaka, daima wakiwa na matumaini ya kutekeleza mambo makuu katika maisha yao. Wakleri wafarijike na kufurahia uhusiano na mafungamano ya dhati na Kristo Yesu katika maisha yao ya kila siku.

Baba Mtakatifu anakitaka Kikosi kazi cha utekelezaji wa shughuli za kichungaji Jimbo kuu la Roma, waliopewa dhamana na kutumwa kwenda kutekeleza sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa Jimbo kuu la Roma katika kipindi cha Mwaka 2019-2020, wahakikishe kwamba, Injili ya Kristo inakuwa ni dira na mwongozo wa maisha yao, ili kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya waamini. Waige mfano wa watakatifu na mashuhuda wa imani waliojiweka chini ya nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu na wakafanikiwa kutafsiri na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Waamini watambue kwamba, nyumba ya Mungu yaani Kanisa ni mahali patakatifu panapomkutanisha Mwenyezi Mungu na waja wake, ni nyumba ya sala na ibada inayopaswa kutakaswa kila wakati, ili kuwawezesha watu wa Mungu kutambua wito na dhamana yao katika mchakato mzima wa kazi ya ukombozi kama ilivyokuwa kwa Waisraeli.

Kristo Yesu ni Hekalu lililoshuka kutoka mbinguni, likaharibiwa kwa njia ya mateso na kifo cha aibu, lakini likasimama tena imara baada ya siku tatu, kwa njia ya Ufufuko kutoka kwa wafu! Kikosi kazi cha Jimbo kuu la Roma kina dhamana na wajibu wa kusaidia utekelezaji wa shughuli za kichungaji, kwa kuibua sera na mipango itakayosaidia kukutana na waamini ambao kutokana na sababu mbali mbali wamekuwa nje kabisa na huruma na upendo wa Kristo Yesu na Kanisa lake. Watu wote wafahamu kwamba, Kristo Yesu anataka kupyaisha maisha yao kwani uwepo wa dhambi unamfanya Kristo Yesu kuwa mbali na watu waja wake na matokeo yake nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu ndani mwao inanyauka na kukauka na hata kupotea kabisa! Yesu anahitaji siku tatu tu, kuweza kulisimamisha Hekalu lake katika maisha ya waamini. Kwa hakika hakuna mtu ambaye amelaaniwa na kutupiliwa mbali na huruma pamoja na upendo wa Mungu. Daima Mwenyezi Mungu anatoa fursa kwa waja wake wanaohitaji kufahamu ukweli, wema na uzuri kwa kutoa nafasi katika mchakato wa uinjilishaji.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, uinjilishaji ni shughuli pevu, kwani njiani wanaweza kukutana na watu wasiojali na wenye shingo ngumu, daima wakumbuke kwamba, Mwenyezi Mungu anahitaji siku tatu tu, ili kuweza kumfufua Kristo Yesu katika nyoyo za waamini wake. Wongofu wa dhati ni matunda ya neema ya Mwenyezi Mungu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, maana Kristo Yesu alikufa kwa ajili ya watu wote na wito halisi wa binadamu ndio mmoja, ule wa kimungu. Kwa hiyo lazima waamini wawe na wazo kwamba Roho Mtakatifu anawajalia watu wote uwezekano wa kushiriki fumbo la kipasaka, kwa jinsi anavyoijua Mungu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, yote haya yataweza kumwilishwa katika mchakato wa uinjilishaji, ili watu wa Mungu waweze kukua na kukomaa katika imani inayobubujika kutoka kwenye Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, daima wakiwa wanawaka wivu kwa ajili ya nyumba ya Mungu.

Papa: Kutabaruku Kanisa
10 November 2019, 12:17