Tafuta

Vatican News
Papa Francisko, Ijumaa tarehe 8 Novemba 2019 amekutana na kuzungumza na wawakilishi wa Jeshi la Wokovu na kukazia umuhimu wa ushuhuda wa utakatifu wa maisha katika huduma. Papa Francisko, Ijumaa tarehe 8 Novemba 2019 amekutana na kuzungumza na wawakilishi wa Jeshi la Wokovu na kukazia umuhimu wa ushuhuda wa utakatifu wa maisha katika huduma.  (Vatican Media)

Papa Francisko na Wawakilishi wa Jeshi la Wokovu: Utakatifu!

Leo hii, ulimwengu mamboleo umegubikwa na “blanketi” la: Uchoyo na ubinafsi; kinzani na migawanyiko ya kila aina. Kumbe, harufu ya sadaka na majitoleo ni chachu yenye mvuto unaofungua akili na nyoyo za watu ili kung’amua maana ya maisha ya mwanadamu hapa ulimwenguni. Papa amewashukuru wafuasi wa Jeshi la Wokovu kwa huduma mbali mbali wanazoendelea kutoa mjini Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jeshi la Wokovu limekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hiki ni kielelezo makini cha ushuhuda upendo na utii unaobubujika kutoka kwenye amri upendo kwa jirani, kama ushuhuda ya kwamba, kweli wamekuwa ni wanafunzi wake Kristo Yesu, wakiwa na upendo wao kwa wao! Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na wawakilishi wa Jeshi la Wokovu, waliomtembelea mjini Vatican, Ijumaa, tarehe 8 Novemba 2019. Baba Mtakatifu anasema, malezi na majiundo yake katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene ni urithi kutoka kwa Bibi yake, aliyemfundisha miaka kadhaa iliyopita. Hawa ni wazee waliokuwa wanajituma na kujisadaka kwa ajili ya maskini na wanyonge katika jamii, kiasi kwamba, matendo yao yalikuwa na mvuto mkubwa kwa watu. Jambo la msingi linalopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza ni wito wa utakatifu wa maisha ya Kikristo unaovuka mipaka ya madhehebu.

Huu ni utakatifu unaokumbatiwa katika wema, mshikamano sanjari na uponyaji unaogusa undani wa mtu, kiasi cha kushuhudia kwamba, kwa kweli hawa wamekuwa ni wanafunzi wa Kristo Yesu. Katika muktadha huu, Wakatoliki la Jeshi la Wokovu, wanapaswa kuendelea kushirikiana, kusaidiana huku wakiheshimiana. Lengo ni kuwawezesha wafuasi wa Kristo kuwa ni chachu ya sadaka na huduma ya upendo yenye mguso na mashiko. Vijana wana kiu na hamu ya kuona na kushuhudia chachu ya upendo katika uhalisia wa maisha yao. Leo hii, ulimwengu mamboleo umegubikwa na “blanketi” la: Uchoyo na ubinafsi; kinzani na migawanyiko ya kila aina. Kumbe, harufu ya sadaka na majitoleo ni chachu yenye mvuto unaofungua akili na nyoyo za watu ili kung’amua maana ya maisha ya mwanadamu hapa ulimwenguni. Baba Mtakatifu Francisko kama Askofu wa Jimbo la Roma, amewashukuru na kuwapongeza wafuasi wa Jeshi la Wokovu kwa huduma mbali mbali wanazoendelea kutoa kwa watu wa Mungu, mjini Roma, hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu anawapongeza kwa kusimama kidete kupambana kufa na kupona dhidi ya biashara binadamu na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Anawaombea ili kweli Mwenyezi Mungu aweze kubariki jitihada hizi zinazopania kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewasihi wajumbe hawa, kuendelea kusindikizana katika sala; kwa kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja, ili kutangaza na kushuhudia upendo wa Mungu kwa njia ya huduma makini inayofumbatwa kwenye mshikamano wa dhati!

Papa: Jeshi la Wokovu

 

08 November 2019, 15:33