Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema, utekelezaji wa haki msingi wa wafungwa wa kivita kimataifa ni wajibu wa kimaadili kwa wadau wote! Papa Francisko asema, utekelezaji wa haki msingi wa wafungwa wa kivita kimataifa ni wajibu wa kimaadili kwa wadau wote!  (AFP or licensors)

Papa: Utekelezaji wa haki ya wafungwa ni wajibu wa kimaadili!

Wafungwa wa vita ni matokeo ya uvunjwaji wa haki msingi za binadamu, matumizi mabaya ya madaraka, mipasuko ya kijamii, dhuluma na mateso. Kuna watu wanaotekwa nyara na wengine kutoweka katika mazingira ya kutatanisha; kuna mauaji ya kikatili pamoja na dhuluma kwa wakleri na watawa; kuna ukosefu wa uhuru wa kuabudu na kidini sehemu mbali mbali za dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa tarehe 12 Agosti 2019,  imeadhimisha kumbu kumbu  ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Mkataba wa Kimataifa wa Geneva wa mwaka 1949. Mkataba huu ni chombo cha sheria kimataifa, kinachodhibiti  matumizi ya nguvu wakati wa vita, na kuhimiza umuhimu wa kuwalinda raia na wafungwa wakati wa vita. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, kumbu kumbu ya Miaka 70 ya Mkataba wa Kimataifa wa Geneva utazihamasisha nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutambua na kuthamini maisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu hata katika mazingira ya vita na mapambano ya silaha. Wadau wote wanatakiwa kuhakikisha kwamba wanaheshimu na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na haki ya kimataifa kuhusu utu wa binadamu. Hii ni dhamana ya kimaadili kulinda, kudumisha na kutetea utu, heshima na haki msingi za wafungwa wa vita. Hii ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko, wakati alipokuwa anazungumza na wahudumu wakatoliki wa maisha ya kiroho kwenye vikosi vya ulinzi na usalama, 130 kutoka katika nchi 70 pamoja na Maaskofu wa Majimbo ya Kijeshi, waliokuwa wanahudhuria kozi ya awamu ya tano kuhusu haki za kimataifa.

Kozi hii iliandaliwa na: Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu, Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu pamoja na Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki, kuanzia tarehe 29-31 Oktoba 2019 hapa mjini Roma. Kozi ya mwaka huu imejikita zaidi katika: Ukosefu wa uhuru wakati wa vita sanjari na Dhamana na utume wa wahudumu wa maisha ya kiroho kwenye vikosi vya ulinzi na usalama. Baba Mtakatifu anasema, watu wanapaswa kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano, kwa kuondolea mbali dhana ya uadui, kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu wana haki na utu sawa na kwamba, maisha ya binadamu ni matakatifu kwa sababu asili yake ni Mwenyezi Mungu. Wafungwa wa vita ni matokeo ya uvunjwaji wa haki msingi za binadamu, matumizi mabaya ya madaraka, mipasuko ya kijamii, dhuluma na mateso. Kuna watu wanaotekwa nyara na wengine kutoweka katika mazingira ya kutatanisha.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kuna mauaji ya kikatili pamoja na dhuluma kwa wakleri na watawa ambao wamejisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao, lakini wanateseka na hata kuuwawa kutokana na ukosefu wa uhuru wa kuabudu na kidini pamoja na maamuzi mbele yanayofumbatwa wakati mwingine kwenye dhana potofu ya utaifa kwa ajili ya “kujimwambafai”. Wote hawa wanakumbukwa na kuombewa na Baba Mtakatifu, ili hata siku moja, wasitindikiwe na imani na matumaini thabiti katika maisha yao. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kuwa, haki ya wafungwa kimataifa inakazia utu, heshima na haki msingi za wafungwa na kwamba, utekelezaji wake ni dhamana ya kimaadili na utu wema. Licha ya sababu mbali mbali zinazoweza kupelekea watu kufungwa gerezani, lakini bado: utu, heshima na haki zao msingi zinapaswa kuzingatiwa. Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa kulea na kukuza dhamiri nyofu kwa wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama na kwamba, hii ni dhamana na utume wa wahudumu wakatoliki wa maisha ya kiroho pamoja na Maaskofu wa Majimbo ya Kijeshi.

Haki ya wafungwa wa kivita kimataifa ipewe uzito wa pekee katika malezi na  majiundo ya wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama. Tena anawaalika wahudumu hawa kuwatembelea na kuwahudumia wafungwa mara kwa mara kama sehemu ya utekelezaji wa Habari Njema ya Wokovu. Wawasaidie kutambua na kutekeleza haki zao msingi kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu. Viongozi wa Kanisa katika vikosi vya ulinzi na usalama ni sehemu ya wahudumu wa watu wa Mungu na haki zao msingi. Utume huu unasaidia kujenga na kuimarisha fadhila ya upendo kwa watu kutoka katika: makabila, lugha, jamaa, tamaduni, dini na mataifa mbali mbali. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wanazuia watu kufungwa magerezani, dhamana na wajibu unaopaswa kutekelezwa kuanzia katika ngazi ya familia pamoja na jumuiya mbali mbali za Kikristo. Pili ni ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika ukweli, uwazi na urafiki, wema pamoja na kuheshimiana kwa dhati. Amana na utajiri wa maisha ya binadamu uwawezeshe watu wa Mataifa kujenga na kudumisha familia kubwa ya binadamu.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama ni wahudumu wa usalama na uhuru wa watu wa Mungu. Ni maneno yanayokita uzito wake katika tunu msingi za kiutu na maisha ya Kikristo. Baba Mtakatifu anakaza kwa kusema Vatican inaunga mkono kwa nguvu zote utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Geneva wa Mwaka 1949. Pale ambapo bado kuna haja ya kurekebishwa, parekebishwe hasa katika masuala ya kivita ndani ya nchi husika. Utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa na kudumishwa. Vaticana itaendelea kuchangia katika utekelezaji wa Mtakaba wa Geneva wa Mwaka 1949 katika uwanja wa Jumuiya ya Kimataifa, ili haki msingi za wafungwa ziweze kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote. Itakumbukwa kwamba, kama sehemu ya utekelezaji wa Mkataba huu, wanajeshi wakati wa vita: wanatakiwa kuwalinda raia na miundo mbinu ya kiraia hasa hospitali, shule, nyumba za ibada pamoja na kambi za wakimbizi. Lakini, Baba Mtakatifu Francisko kwa uchungu mkubwa ameonya kwamba,  vita pamoja na vitendo vya kigaidi ni maafa makubwa kwa binadamu.

Hizi ni dalili za kushindwa kwa binadamu. Mkataba wa Kimataifa wa Geneva wa mwaka 1949 pamoja na itifaki zilizoongezwa baadaye,  ni chombo cha sheria kimataifa kinachoratibu hali tete wakati wa vita vya nchi kavu kwa kuwalinda raia, kuwahudumia askari waliojeruhiwa pamoja na kuwalinda mateka wa vita. Hii ni sheria inayozingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu kimataifa. Mkataba wa kwanza ulijihusisha na mchakato wa kuwalinda askari waliojeruhiwa vitani. Mkataba wa pili, ukaongezwa ili kuwasaidia askari wa majini waliojeruhiwa vitani na meli zao kuharibiwa. Mkataba wa tatu ulikusudiwa kwa ajili ya kuwalinda mateka wa vita, kwa kuzingatia athari zilizojitokeza wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia pamoja na Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Kwamba, mateka wa vita watapaswa kuachiwa huru mara tu vita inapokoma. Mkataba wa Nne unahusu umuhimu wa kuwalinda na kuwasaidia raia wakati wa mapambano ya silaha; kwa kutenga maeneo maalum ambapo raia wanaweza kupata huduma bila upendeleo wowote ule. Kumbe, Mkataba wa Kimataifa wa Geneva wa mwaka 1949 umeridhiwa na Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na kwamba nchi zote zinawajibika kutekeleza yote yaliyobainishwa kwenye Mkataba huu.

Papa: Wafungwa wa Kivita

 

04 November 2019, 11:00