Tafuta

Vatican News
Kituo cha "Rosario Livatino" kinahimizwa kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kituo cha "Rosario Livatino" kinahimizwa kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Dumisheni Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwa bahati mbaya sana, mwelekeo wa sasa ni kwa wanasheria kuona kwamba, wazee, walemavu na wagonjwa wanakabiliana mubashara na kifo, kwa madai kwamba, mtu anayo “haki ya kufa” badala ya kuendelea kuteseka kwa magonjwa na maumivu. Hiki ni kichume kabisa cha Injili ya uhai! Dhamiri nyofu iwaongoze watu kuamua kwa busara!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kituo cha Mafunzo cha "Rosario Livatino" kinamilikiwa na kuongozwa na Mahakimu kutoka nchini Italia wanaojihusisha na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; haki msingi za binadamu; uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu pamoja na haki ya mtu kuishi dhidi ya utamaduni wa kifo unaokumbatia sera za kifolaini pamoja na utoaji mimba. Kituo hiki ni sehemu ya kumbu kumbu endelevu ya Hakimu Rosario Angelo Livatino, ambaye, tarehe 21 Septemba 1990 akiwa na umri wa miaka thelathini na nane, alipigwa risasi na kuuwawa hapo hapo wakati akiwa njiani kuelekea kazini. Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 9 Mei 1993 wakati akitoa mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu kwa wale wote wanaojihusisha na kikundi cha uhalifu wa kimataifa cha Mafia, alimtaja hakimu Rosario Angelo Livatino kuwa ni “Shuhuda wa haki na imani thabiti.

Mchakato wa Jimbo kutaka kumtangaza kuwa Mwenyeheri umekamilika na kwamba, Mwanasheria huyu ni mfano bora wa kuigwa na wale wote waliopewa dhamana ya kuhakikisha kwamba, wanawajibika kikamilifu ili haki iweze kutendeka. Washutumiwa wapewe nafasi ya kujitetea ili kweli haki iweze kushika mkondo wake. Wawe ni mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yao ya kila siku, kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za kifo laini pamoja na utoaji mimba. Hii inatokana na ukweli kwamba, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kulindwa na kudumishwa. Kwa bahati mbaya sana, mwelekeo wa sasa ni kwa wanasheria kuona kwamba, wazee, walemavu na wagonjwa wanakabiliana mubashara na kifo, kwa madai kwamba, mtu anayo “haki ya kufa” badala ya kuendelea kuteseka kwa magonjwa na maumivu. Hiki ni kichume kabisa cha Injili ya uhai!

Hakimu Rosario Angelo Livatino, alikazia sana umuhimu wa wanasheria kufuata Katiba na Sheria za nchi lakini pia kwa kuongozwa na dhamiri nyofu, ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Haki inapaswa kutekelezwa kwa hekima, busara na unyenyekevu wa hali ya juu, daima utu wa mwanadamu ukipewa kipaumbele cha pekee. Dhamiri ni sheria mama iliyoandikwa katika moyo wa mwanadamu ili kujua jema linalopaswa kutendwa na uovu kuweza kuuepukwa. Hapa ni mahali patakatifu ambapo Mwenyezi Mungu anazungumza mubashara na waja wake. Mtumishi wa Mungu Livatino anasema kupanga ni kuchagua, ili kuweza kuchagua vyema, kuna haja kwa wanasheria kujenga urafiki na mafungamano ya dhati kabisa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala; kwa kuwapenda na kuwaheshimu watuhumiwa pamoja na wadau wa vyombo vya sheria kutambua kwamba, hata wao ni binadamu. Kumbe, wanaweza kujikuta hata wao wametumbukia katika udhaifu wa kibinadamu! Sheria ni msumemo!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni utajiri, amana na urithi mkubwa ambao Hakimu Rosario Angelo Livatino ameiachia nchi ya Italia. Kwa njia ya mwanga wa imani, Mahakimu wanaweza kutekeleza vyema dhamana na utume wao katika jamii, kwa kuonesha utii kwa Kanisa na Serikali katika ujumla wake. Utulivu ni fadhila inayowaunganisha watu ndani ya jamii. Mahakimu na Majaji wanahamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa utulivu wa kijamii, ili kudumisha mafungamano, utu na heshima ya binadamu. Katika utekelezaji wa majukumu yao, wajitahidi kufafanua sheria, taratibu na kanuni zinazoweza kutumika kila siku pamoja na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao.

Papa: Injili ya uhai

 

 

30 November 2019, 15:55