Tafuta

Vatican News
Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Thailand kuanzia tarehe 19-23 Novemba 2019: Inaongozwa na kauli mbiu "Mitume wa Kristo, Wamisionari Mitume" Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Thailand kuanzia tarehe 19-23 Novemba 2019: Inaongozwa na kauli mbiu "Mitume wa Kristo, Wamisionari Mitume"  (ANSA)

Hija ya Papa Francisko Thailand: Ujumbe kwa watu wa Mungu

Katika ulimwengu mamboleo ambamo watu wanaonja ukosefu wa amani, misigano, kinzani na utengano, mambo yanayo hatarisha umoja na mafungamano ya kijamii, utu na heshima ya mwanadamu, kuna haja kwa watu wote kushikamana ili kudumisha maendeleo ya kweli kwa ajili ya familia binadamu; kwa kukazia mshikamano katika haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 19-23 Novemba 2019 anafanya hija ya 32 ya kitume nchini Thailand inayoongozwa na kauli mbiu: “Mitume wa Kristo, Wamisionari Mitume”. Hija hii ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 350 tangu kuanzishwa kwa utume wa Vikarieti ya Siam kunako mwaka 1669. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kama sehemu ya maandalizi ya hija yake ya kitume nchini Thailand, anasema, anapenda kuchukua fursa hii kuwasalimia kwa moyo wa upendo, kwa kutambua utajiri mkubwa unaounda taifa la Thailand, ambalo limejishughulisha kikamilifu ili kuhakikisha kwamba, linajenga na kudumisha amani na utulivu, si tu kwa ajili ya wananchi wake, bali hata kwa Ukanda mzima wa Kusini Mashariki wa Bara la Asia.

Baba Mtakatifu anasema, katika ulimwengu mamboleo ambamo watu wanaonja ukosefu wa amani, misigano, kinzani na utengano, mambo yanayo hatarisha umoja na mafungamano ya kijamii, utu na heshima ya mwanadamu, kuna haja kwa watu wote wenye mapenzi mema kushikamana ili kudumisha maendeleo makubwa na ya kweli kwa ajili ya familia binadamu; kwa kukazia mshikamano katika haki pamoja na kuwawezesha watu kuishi kwa amani. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, katika hija yake ya kitume nchini humo, atapata nafasi ya kuungana na waamini wa Kanisa Katoliki, ili kuwaimarisha katika imani na kuwatia shime, ili waendelee kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya jamii nzima. Ni matumaini yake kuwa, ataweza kuimarisha mshikamano wa urafiki pamoja na Wabudha, ambao wamekuwa kweli ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha, kwa kujikita katika ujenzi wa jamii himilivu na yenye utulivu utambulisho makini wa familia ya Mungu nchini Thailand.

Baba Mtakatifu ana imani kwamba, hija yake ya kitume, itachangia kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini; ili kukuza uelewano, ushirikiano wa kidugu, lakini zaidi huduma kwa maskini na wahitaji zaidi sanjari na huduma ya amani. Huu ni wakati muafaka wa kujishughulisha zaidi na ujenzi wa amani. Baba Mtakatifu Francisko anatambua kwamba, kuna watu wanaoendelea kujisadaka ili kuhakikisha kwamba, hija yake ya kitume inafanikiwa. Kumbe, anapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru kwa dhati na kwamba, anawahifadhi wananchi wote wa Thailand katika “sakafu ya moyo wake” kwa njia ya sala. Anasali kwa ajili ya kuwaombea wao, familia na nchi yao. Anawaomba waendelee kumkumbuka na kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala na sadaka zao.

Papa Thailand: Ujumbe

 

 

15 November 2019, 13:43