Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawashukuru na kuwapongeza wafanyakazi katika sekta ya afya nchini Thailand, kwa kuendeleza na kudumisha matendo ya huruma kwa wagonjwa! Papa Francisko anawashukuru na kuwapongeza wafanyakazi katika sekta ya afya nchini Thailand, kwa kuendeleza na kudumisha matendo ya huruma kwa wagonjwa!  (Vatican Media)

Hija ya Papa Francisko Thailand: Ujumbe kwa wahudumu wa afya

Wafanyakazi katika sekta ya afya wanatekeleza kwa dhati kabisa matendo ya huruma kwa kujitosa kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa, ili kukumbatia Injili ya uhai, wa wagonjwa wote wanaowasili kitengo cha dharura, ili kuwatibu na kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu, kwa kuheshimu utu wao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Muhimu: Utu wa mgonjwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kama kielelezo cha huruma, upendo na mshikamano na wagonjwa pamoja na wale wote wanaoteseka kiroho na kimwili, Baba Mtakatifu Francisko Alhamis tarehe 21 Novemba 2019 ametembelea Hospitali ya St. Louis iliyoanzishwa kunako mwaka 1898 kama kielelezo cha huruma na uwepo endelevu wa Mungu kati ua waja wake. Hii ni huduma ambayo Kanisa linatoa kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Thailand, shukrani kwa wale wote wanaojisadaka usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba, wagonjwa wanapata tiba muafaka na kuwasaidia kumtafakari Mwenyezi Mungu anayejitaabisha kuwaganga na kuwainua tena watu wake. Kauli mbiu inayoongoza huduma hospitalini hapa ni “Ubi caritas, Deus ibi est” yaani “Palipo na upendo, hapo Mungu yupo”, kielelezo makini cha ushuhuda wa wafuasi wamisionari, ambao wameendelea kuwa waaminifu kwa amri ya Kristo na siku ya hukumu watapata faraja kwani kadiri ya walivyomtendea mmojawapo na hao ndugu zake Yesu walio wadogo, wamemtendea Kristo mwenyewe.

Baba Mtakatifu anasema, wafanyakazi katika sekta ya afya ni wafuasi wamisionari, ambao mahusiano yao ya huduma yanakuza udugu wa kimuujiza na kitaamuli. Huu ni udugu wa upendo wenye uwezo wa kuona ukuu wa utakatifu wa jirani, kwa kumwona Mwenyezi Mungu  katika kila mwanadamu, kwa kuvumilia maudhi; kwa kuufungua moyo ili kuupokea upendo wa Kimungu pamoja na kutafuta furaha ya wengine, kama anavyofanya Baba yao wa mbinguni. Wafanyakazi katika sekta ya afya wanatekeleza kwa dhati kabisa matendo ya huruma kwa kujisadaka na kujitosa kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa, ili kukumbatia Injili ya uhai wa wagonjwa wote wanaowasili kitengo cha dharura, ili kuwatibu na kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu, kwa kuheshimu utu wao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mchakato wa uponyaji unapaswa kutazamwa kama njia makini ya kuremrejeshea tena mgonjwa utu na heshima yake.

Wafanyakazi katika sekta ya afya, wajitahidi kuwaita wagonjwa kwa majina yao, ingawa kuna changamoto na ugumu wake, ndiyo maana wafanyakazi katika sekta ya afya wanapaswa kusindikizwa na kuungwa mkono. Huduma ya uponyaji inapaswa kutekelezwa na wanajumuiya wote, kila mtu kadiri ya wito na nafasi yake, kama ushuhuda wa huruma ya Mungu. Hospitali ya St. Louis iliyoanzishwa kunako mwaka 1898, mwaka huu wa 2019 inaadhimisha kumbu kumbu ya takribani miaka 120 tangu kuanzishwa kwake. Imekuwa ni chemchemi ya faraja na uponyaji wa magonjwa mbali mbali; kimbilio la waliokuwa pweke katika maisha na kwamba, huu ni muda muafaka wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani, kwa ajili ya utume wa Kanisa, ili kweli liweze kuwa na ujasiri wa kuwakirimia wagonjwa upedo wa Kristo Yesu unaoganga na kuponya. Baada ya mkutano wake na wafanyakazi katika sekta ya afya, Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kuwatembelea na kuwasalimia wagonjwa na walemavu, ili kuwapatia matumaini ya kuweza kusonga mbele kwa imani katika shida na mahangaiko yao.

Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alionja shida na mahangaiko ya wagonjwa, Kanisa linataka kujiunga naye ili kumuunga mkono katika safari ya huduma. Baba Mtakatifu anawaalika waamini katika shida, udhaifu na mahangaiko yao ya kibinadamu, wakimbilie hifadhi kutoka katika Madonda Matakatifu ya Yesu. Kuna wakati wanaonja mkate wa machungu na maji ya mateso, lakini watambue kwamba, ingawa Bwana atawapatia chakula cha shida na maji ya msiba, lakini Mwenyezi Mungu ataendelea kuandamana nao katika huduma yao!

Papa: Wagonjwa
21 November 2019, 16:08