Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anasema, waathirika wa majanga mbali mbali nchini Japana wanahitaji kuonjeshwa mshikamano wa huruma na upendo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, waathirika wa majanga mbali mbali nchini Japana wanahitaji kuonjeshwa mshikamano wa huruma na upendo. 

Hija ya Papa Francisko nchini Japan: Ujumbe kwa waathirika wa majanga nchini Japan

Ujenzi mpya wa maeneo yaliyoathirika unahitaji umoja na mshikamano, ili kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kuwajengea matumaini wale waliovunjika na kupondeka moyo. Miaka nane imeyoyoma na Japan imeshuhudia kwamba, inaweza kujenga umoja, mshikamano, uvumilivu na udumifu katika kukabiliana na changamoto mamboleo, kwa kuendelea kushikana mikono!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya kitume Baba Mtakatifu Francisko nchini Japan kuanzia tarehe 23 hadi 26 Novemba 2019 inaongozwa na kauli mbiu “Linda Maisha Yote”. Huu ni ujumbe unaowataka watu wa Mungu nchini Japan kusimama kidete kulinda: utu, haki na heshima ya binadamu dhidi ya vitisho vinavyohatarisha misingi ya amani na utulivu na hasa zaidi mapambano ya silaha. Kanisa Katoliki nchini Japan, mwaka 2019 linaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 470 tangu alipowasili nchini humo, Mtakatifu Francisko Xavier pamoja na wenzake na huo ukawa ni mwanzo wa kuenea kwa Ukristo nchini Japan. Kunako mwaka 1614 madhulumu dhidi ya Wakristo yakafumuka na kupamba moto kwa takribani miaka 260 na waamini wengi wakauwawa kikatili kwa ajili ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Japan inatambua fika madhara ya vita na matumizi ya silaha za atomiki; maafa makubwa ya tetemeko kubwa la ardhi na tsunami iliofuatia vilisababisha vifo vya watu zaidi ya 20,000 nchini Japan. Uharibifu uliosababishwa kwenye mtambo wa nyuklia wa Fukushima Daichi ulipelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao. Haya ni mambo ambayo bado yameacha kumbu kumbu hai katika maisha ya wananchi wa Japan. Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linasema kuna haja ya kujizatiti zaidi “Kulinda maisha yote”. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 25 Novemba 2019 amekutana na kuzungumza na wahanga wa tetemeko la ardhi, tsunami pamoja na waathirika wa mtambo wa nyuklia wa Fukushima Daichi, hadi leo hii kuna baadhi ya watu ambao hawajulikani waliko!

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kwa ajili ya kusali na kukaa katika ukimya; amesikiliza shuhuda za wahanga wa majanga haya matatu na kwamba, hawa ni watu ambao bado wanahitaji msaada wa hali na mali kutoka kwa Wasamaria wema. Zaidi ya watu 50, 000 wanaishi kwenye makazi ya muda. Mshikamano wa upendo uliooneshwa na watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwa ajili ya kuwasaidia waathirika unapaswa kuendelezwa, ili kuhakikisha kwamba, waathirika wanapata mahitaji yao msingi. Ujenzi mpya wa maeneo yaliyoathirika unahitaji umoja na mshikamano, ili kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kuwajengea matumaini wale waliovunjika na kupondeka moyo. Miaka nane imeyoyoma na Japan imeshuhudia kwamba, inaweza kujenga umoja, mshikamano, uvumilivu na udumifu katika kukabiliana na changamoto mamboleo, kwa kuendelea kushikana mikono na kusonga mbele hatua kwa hatua.

Huu ni mshikamano kwa ajili ya kizazi hiki na kile kijacho anasema Baba Mtakatifu Francisko. Kuna changamoto pevu zinazoendelea kuukumba ulimwengu mamboleo na hizi zinahitaji utashi wa kisiasa, mshikamano na mafao ya wengi yakipewa kipaumbele cha kwanza. Vita sehemu mbali mbali za dunia, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, baa la njaa na utapiamlo wa kutisha, athari za mtikisiko wa uchumi kitaifa na kimataifa pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi ni mambo ambayo utekelezaji wake unahitaji mshikamano, kwa kuwa na maamuzi bora zaidi ya matumizi ya rasilimali za dunia; kwa kujenga utamaduni wa kupambana na umaskini duniani ili kupunguza pengo kubwa kati ya maskini na matajiri duniani. Kuna haja ya kushikamana kwa pamoja kama familia ya binadamu, kwa kutambua kwamba, watu wanategemeana na kukamilishana.

Baba Mtakatifu anasema maafa yaliyosababishwa na mtambo wa nyuklia wa Fukushima Daiichi ni makubwa sana si tu katika masuala ya kisayansi na huduma ya tiba, bali pia ni changamoto katika ujenzi wa mafungamano ya kijamii, kwa kuwahakikishia wananchi usalama wa maisha yao na kwamba, matumizi ya nguvu za kinyuklia bado ni hatari sana kwa usalama wa maisha ya binadamu. Kuna kishawishi kikubwa cha kutaka kudhani kwamba, maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ndicho kipimo pekee cha maendeleo ya binadamu, lakini maendeleo haya yamekuwa pia na madhara yake makubwa katika maisha ya watu. Kumbe, kuna haja ya kufanya upembuzi yakinifu ili kuibua sera na mikakati itakayosaidia kulinda maisha, kudumisha umoja na mshikamano wa familia ya binadamu.

Mustakabali, ustawi na mafao ya wengi, ni mambo yanayotegemea maamuzi ya busara, uwajibikaji na utekelezaji wa pamoja; kwa kuheshimu na kuthamini  uhai wa binadamu pamoja na kuendelea kujizatiti katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Watu wote ni vyombo vya Mungu kwa ajili ya utunzaji bora wa mazingira na kwamba, kila mtu anapaswa kutumia vyema karama zake. Baba Mtakatifu anawakumbusha wananchi wa Iwate, Miyagi na Fukushima kwamba, bado hawajasahauliwa, kwani kuna watu bado wanaendelea kuguswa na mateso yao, hivyo wataendelea kunyoosha mkono wa udugu ili kuwasaidia. Huruma hii iwe ni chemchemi ya matumaini, utulivu na usalama kwa siku za usoni.

Papa: Wahanga

 

 

25 November 2019, 14:34