Tafuta

Vatican News
Papa Francisko akiwa kwenye Madhabahu ya Mwenyeheri Nicolas Bunkerd Kitbamrung amekutana na kuzungumza na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC Papa Francisko akiwa kwenye Madhabahu ya Mwenyeheri Nicolas Bunkerd Kitbamrung amekutana na kuzungumza na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC  (Vatican Media)

Hija ya Papa Francisko Nchini Thailand: Ujumbe kwa Maaskofu Barani Asia, FABC

Papa Francisko katika hotuba yake amegusia kuhusu: Ushuhuda wa imani unaobubujika kutoka kwa wafiadini, Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa FABC, Nafasi ya Roho Mtakatifu katika mchakato wa uinjilishaji na umuhimu wa kukuza tasaufi maalum kwa ajili ya watu wa Mungu. Mwenyeheri Nicolas Bunkerd Kitbamrung, alisadaka maisha na utume wake kwa ajili ya ushuhuda!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 19-23 Novemba 2019 anafanya hija ya kitume nchini Thailand inayoongozwa na kauli mbiu: “Mitume wa Kristo, Wamisionari Mitume”. Hija hii ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 350 tangu kuanzishwa kwa utume wa Vikarieti ya Siam kunako mwaka 1669. Ijumaa, tarehe 22 Novemba 2019, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Thailand, mwenyeji wa mkutano huu. Mkutano huu umefanyika kwenye Madhabahu ya Mwenyeheri Nicolas Bunkerd Kitbamrung, Padre na mfiadini, huko Sampran, Jimbo kuu la Bangkok nchini Thailand. Kardinali Francis Xavier Kriengsak Kovithavanij, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bangkok, katika salam zake kwa Baba Mtakatifu amekumbushia kwamba, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC lililoanzishwa kunako mwaka 1972, kama matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

FABC kunako mwaka 2020 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake na kilele cha maadhimisho haya kitakuwa nchini Thailand kwa kuongozwa na kauli mbiu “FABC 2020: Safari ya Pamoja kama Watu wa Bara la Asia”. Hili ni Bara ambalo lina utajiri mkubwa wa dini mbali mbali, changamoto na mwaliko kwa Kanisa ni kuendeleza majadiliano ya kidini, mshikamano na uwajibikaji wa pamoja, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Asia. Ni matumaini ya Maaskofu kwamba, Jubilei hii itakoleza mchakato wa uinjilishaji Barani Asia na kuendeleza majadiliano ya kidini katika udugu na huduma kwa watu wa Mungu Barani Asia. Kanisa linataka kuwa ni chombo na shuhuda wa upatanisho haki na amani hasa katika Ukanda huu unaotambulikana kwa: vita, migogoro, biashara haramu ya binadamu na viungo vyake  pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Kanisa nchini Thailand linataka kutoa ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili, ili kuwawezesha waamini kuwa kweli ni mitume wamisionari nchini Thailand na kwa njia ya ushuhuda wa maisha, waweze kujenga na kudumisha umoja na mafungamano ya kitaifa!

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC, amegusia ushuhuda wa imani unaobubujika kutoka kwa wafiadini, Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa FABC, Nafasi ya Roho Mtakatifu katika mchakato wa uinjilishaji unaofumbatwa katika wongofu na utangazaji wa Neno la Mungu pamoja na umuhimu wa kukuza tasaufi maalum kwa ajili ya watu wa Mungu. Mwenyeheri Nicolas Bunkerd Kitbamrung, Padre na mfiadini alisadaka maisha na utume wake kwa ajili ya ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili, akainjilisha na kufundisha katekesi, leo hii matunda ya kazi na utume wake yameenea nchini Thailand. Hii ni changamoto kwa Makanisa mahalia Barani Asia kujikita zaidi na zaidi katika mchakato wa uinjilishaji wa kina. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC ni mwaliko wa kutembelea tena “Madhabahu” ya maisha na utume wa wamisionari, tayari kujikita katika mchakato wa uinjilishaji, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Iwe ni fursa ya kupyaisha ari na mwamko wa uinjilishaji, ili watu waonje na kuguswa na upendo wa Kristo Yesu. Majadiliano ya kitamaduni, kiekumene na kidini ni muhimu sana katika kukabiliana na changamoto ya umaskini na unyonyaji katika ngazi mbali mbali. Biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; biashara ya binadamu na viungo vyake sanjari na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo ni mambo ambayo yanaendelea kusigina utu, heshima na haki msingi za binadamu, bila kusahau wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji na ukosefu wa haki jamii unaojionesha kwa pengo kubwa kati ya maskini na matajiri Barani Asia. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu Barani Asia kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa ujasiri, furaha, ari na moyo mkuu, kwa kuzingatia mambo msingi na kuendelea kujifunza kutoka kwa watakatifu waliotangulia mbele za haki, daima Kanisa liendelee kusoma alama za nyakati ili kujenga miundo mbinu itakayorahisisha mchakato wa uinjilishaji.

Kanisa daima linapaswa kuwa aminifu kwa utume wake kama chombo cha sala na uinjilishaji sanjari na kuendelea kujiaminisha kwa Roho Mtakatifu katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaotoa mwanga mpya wa kuweza kufikisha Neno la Yesu kwenye roho za watu ndani kabisa ya miji na tamaduni za watu. Roho Mtakatifu bado anaendelea kuliongoza Kanisa ili kukutana na watu, tamaduni na mazingira mbali mbali. Jambo la msingi hapa anasema Baba Mtakatifu Francisko ni mchakato wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili Barani Asia, kwa sababu maisha ya binadamu wote yana thamani kubwa mbele ya Kristo Yesu. Injili ni zawadi inayoshirikishwa kwa watu pamoja na kuguswa na mahangaiko yao ya ndani. Uinjilishaji mpya unakwenda sanjari na toba na wongofu wa ndani, kwa sababu Kanisa ni chombo cha kuinjilisha, lakini pia linapaswa kuinjilishwa kama alivyowahi kusema Mtakatifu Paulo VI. Kanisa ni Jumuiya ya waamini wenye imani, matumaini na mapendo, wanaopaswa kuwasikiliza na kuwapenda jirani zao. Hapa Kanisa linapaswa kuongoka na kutangaza Habari Njema ya Wokovu ili kushuhudia wito na utume wake kwa njia ya unyenyekevu na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Kanisa halina budi kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa maneno lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Ikumbukwe kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhusika mkuu wa uinjilishaji, ili kutangaza mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Viongozi wa Kanisa ni wahudumu wa Neno na Mafumbo ya Kanisa; dhamana inayotekelezwa kwa upole na ukarimu; kwa kusikiliza na kuheshimu utu wao; kwa kuwathamini na kuwajengea uwezo waamini walei, ili waweze kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Mchakato wa majadiliano ya kitamaduni ulenge kuwakutanisha watu na Kristo Mfufuka na kwamba, Mwenyezi Mungu bado anaendelea kutenda kazi kati ya waja wake. Baba Mtakatifu Francisko anawataka Maaskofu kuwa karibu na wakleri wao, kwa sababu wao ni majirani zao wa karibu zaidi. Wawasikilize na kuwatia shime, wale waliolegea na kukata tamaa; wawatafute na kuwasaidia wale walikengeuka na kumezwa na malimwengu. Maaskofu kwa Mapadre wao wajitahidi kuwa ni Mababa na ndugu na wala si kama meneja au hakimu.

Maaskofu wajenge mazingira ya kuaminiana, majadiliano na uvumilivu kama ambavyo Kristo Yesu anavyowavumilia hata wao katika maisha na utume wao. Maaskofu waendelee kumtegemea na kumtumainia Kristo Mfufuka, chemchemi ya maisha mapya. Waendelee kusafiri kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu yuko daima pamoja nao, anawaalika kutambua uwepo wake kwa kuumega mkate.

Papa: FABC

 

22 November 2019, 16:07