Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Asema utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha za atomiki utafafanuliwa na kuingizwa kwenye Katekesimu ya Kanisa Katoliki kuwa ni kinyume cha maadili na utu wema. Papa Francisko: Asema utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha za atomiki utafafanuliwa na kuingizwa kwenye Katekesimu ya Kanisa Katoliki kuwa ni kinyume cha maadili na utu wema. 

Utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha za atomiki: Katekisimu

Papa amesema matumizi na hifadhi ya mabomu ya atomiki ni kinyume cha maadili na utu wema. Kanisa linapenda kufafanua jambo hili na kuliingiza katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki ambayo kimsingi ni muhtasari wa: Imani, Sakramenti, Maisha Adili na Sala. Kanisa Katoliki limefuta adhabu ya kifo katika mafundisho yake, ili kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 19-26 Novemba 2019 amefanya hija ya 32 ya kitume Barani Asia kwa kutembelea: Thailand na Japan, kama sehemu ya mchakato wa Kanisa wa kutaka kudumisha majadiliano ya kidini na kitamaduni ili kulinda: utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo, mafao ya wengi, haki na amani duniani na kwa namna ya pekee Barani Asia. Alipowasili mjini Roma, Jumanne jioni tarehe 26 Novemba 2019 amekwenda moja kwa moja kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma kusali na kumshukuru Bikira Maria kwa ulinzi na tunza yake ya kimama wakati wote wa hija yake ya kitume Barani Asia. Akiwa njiani kurejea mjini Vatican, Baba Mtakatifu amepata nafasi ya “kuchonga” na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake kutoka Japan. Amejibu kwa ufasaha maswali magumu na tete katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu Injili ya amani, utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Papa amesema matumizi na hifadhi ya mabomu ya atomiki ni kinyume cha maadili na utu wema. Kanisa linapenda kufafanua jambo hili na kuliingiza katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki ambayo kimsingi ni muhtasari wa: Imani, Sakramenti, Maisha Adili na Sala. Kanisa Katoliki limefuta adhabu ya kifo katika mafundisho yake, ili kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo na wala hakuna tena vita halali na ya haki. Fedha ya Kanisa ni kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Inapaswa kutumika kwa kuzingatia kanuni ya ukweli, uwazi, maadili na mafundisho ya Kanisa. Kashfa ya matumizi makubwa ya fedha ya Vatican katika uwekezaji kwenye miundombinu huko London nchini Uingereza, ni matokeo ya usimamizi na udhibiti bora zaidi wa masuala ya fedha unaoendelea kutekelezwa na Mamlaka ya Habari za Kifedha mjini Vatican, iliyoanzishwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2010 na kufanyiwa marekebisho na Papa Francisko kunako mwaka 2013.

AIF inapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake kuzingatia misingi ya: ukweli, uwazi na ushirikiano katika masuala ya fedha kimataifa! Baba Mtakatifu anasema, ana upendo wa dhati kwa familia ya Mungu nchini China na kwamba, anatamani kuwa iko siku, Mwenyezi Mungu akipenda ataweza kuitembelea China. Nchi nyingi za Amerika ya Kusini zimetumbukia katika vurugu, uvunjifu wa amani na utulivu na matokeo yake ni maafa makubwa kwa watu na mali zao. Amerika ya Kusini inawaka moto kwa sasa, lakini kuna haja ya kujikita katika majadiliano yanayosimiwa katika ukweli na uwazi, kwa kuzingatia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Baba Mtakatifu ametumia fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari kwa kuwashukuru kwa mchango wao mkubwa katika kuwajulisha watu wa Mungu kile kilichokuwa kinajiri huko Thailand na Japan, nchi mbili ambazo zinatofautiana sana. Wakati wote amekuwa pamoja nao katika utekelezaji wa majukumu yao.

Baba Mtakatifu akiwa nchini Japan amepata nafasi ya kutembelea miji ya Hiroshima na Nagasaki, mahali ambapo panawapatia watu fursa ya kujifunza kusimama na kutafakari; kufunga, kutubu na kusali ili kutoa nafasi ya hekima na busara ya Mungu kutenda kazi katika maisha ya waja wake. Nagasaki iliharibiwa sana na mashambulizi ya mabomu ya atomiki, lakini ukawa ni chemchemi ya ukristo na mashuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Wakristo wakadhulumiwa na kuteswa sana, lakini ushuhuda wao ukaacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za watu wa Mungu. Mjini Hiroshima, watu wanaonja madhara na ukatili wa silaha za atomiki dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mji wa Hiroshima ni mahali ambapo binadamu amejifunza ukatili mkubwa unaofumbatwa katika utamaduni wa kifo. Ni kutokana na muktadha huu, Baba Mtakatifu anasema bila kupepesapepesa macho kwamba, matumizi  na ulimbikizaji wa silaha za atomiki ni kinyume cha maadili na utu wema.

Mafundisho haya yatafafanuliwa na hatimaye kuingizwa kwenye Katekisimu ya Kanisa Katoliki kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa familia ya binadamu. Pengine, kama alivyosema Einstein: Vita Kuu ya Nne ya Dunia watu watapigana kwa kutumia fimbo na mawe! Kuna mataifa ambayo yanachakata na kutengeneza silaha za kinyuklia, mengine yanahifadhi, hali inayotishia usalama na amani ya Jumuiya ya Kimataifa sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Usalama wa maisha ya binadamu na mazingira yake ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kabla ya kuanza kufikiria utengenezaji, usambazaji na ulimbikizaji wa nishati ya nyuklia. Usalama wa maisha na afya ya watu yazingatiwe sana! Baba Mtakatifu anasema, katika mazungumzo yake na Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe amegusia masuala mbali mbali ya kitaifa na kimataifa; kufurika kwa magereza na adhabu ya kifo nchini Japan.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ameridhia Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kufanya marekebisho kwenye Katekisimu ya Kanisa Katoliki, kifungu namba 2267 kinachozungumzia kuhusu adhabu ya kifo na tafsiri mpya inapaswa kuingizwa katika vipengele mbali mbali vya Katekisimu ya Kanisa Katoliki. Kanisa Katoliki limefuta adhabu ya kifo katika Mafundisho na Mapokeo yake kwa kukazia njia zinazotetea na kulinda maisha ya watu, amani na usalama wao dhidi ya adui; kwani hizi ni njia zinazodumisha utu, ustawi na mafao ya wengi. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inakazia kwamba, hatima na kiini chote cha mafundisho ya imani vinaelekezwa katika upendo ambao hauna kikomo. Iwe inaelekezwa kwa ajili ya ukweli wa imani au, matumaini au wajibu wa utendaji wa maadili, upendo wa Mungu utadumu daima.  Kanisa kwa kusoma alama za nyakati, linataka kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na uhai wa binadamu dhidi ya adhabu ya kifo inayokumbatia utamaduni wa kifo.

Mwenyezi Mungu anawapatia waja wake nafasi ya kutubu na kumwongokea, ili aweze kuwakirimia msamaha na kuwaonjesha tena huruma na upendo wake usiokuwa na kifani! Baba Mtakatifu anakaza kusema, adhabu ya kifo ni kinyume kabisa cha maadili na utu wema. Kuna haja pia ya kutafakari kuhusu utekelezaji wa adhabu ya kifungo cha maisha, kwani wafungwa wengi wanafia magerezani kutokana na magonjwa ya muda mrefu. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alikazia umuhimu wa wakuu wa Serikali kufutilia mbali adhabu ya kifo, ili kudumisha utu wa binadamu, amani na utulivu. Papa Francisko pia anasema adhabu ya kifo haikubaliki kwa sababu inadhuru haki na utu wa mtu. Haitoi nafasi ya mtu kujitetea mbele ya vyombo vya sheria. Kutokana na mwelekeo huu Kanisa linawataka viongozi wa Serikali kusimama kidete kulinda na kutetea uhai wa binadamu kama ambavyo inafafanuliwa kwenye kipengele cha 2265 na 2266 katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki.

Kuhusu Injili ya amani Baba Mtakatifu Francisko anasema, Vijana wanapaswa kujenga tabia ya kujiamini na kukabiliana na changamoto za maisha kwa ujasiri na busara, watambue nguvu na uzuri uliomo ndani mwao; udhaifu na mapungufu katika maisha na kwamba, kwa wale wanaotaka “kujimwambafai kwa kutumia mitandao ya kijamii wanadhani kwamba, kwa kufanya hivi wanakuwa ni watu muhimu sana katika jamii. Baba Mtakatifu anasema hiki ni kinyume chake kabisa kwani hawa ni watu waoga lakini wanataka kujitutumua kwa kutumia mitandao ya kijamii. Jukumu la kudhibiti unyanyasaji, uonevu na ubaguzi wa kimtandao ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na vijana wenyewe kwa kuunganisha nguvu zao huku wakisaidiwa na taasisi za elimu pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kusema “HAPANA” ili kuwaonesha kwamba, haya wanayotenda si mambo mazuri kwa jamii. Kuhusu kuandika Wosia wa Kitume mintarafu amani, bado kuna njia ndefu inayomtaka kusali na kutafakari ili hatimaye, kupata njia ya kutokea.

Mfumo wa demokrasia unaotumika kwenye Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa njia ya “Kura ya Veto” inadumaza ukuaji wa usalama na amani duniani. Jambo ambalo linapaswa kuvaliwa njuga ni Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, uzalishaji na usambazaji wa silaha unapigwa rufuku, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na umoja na udugu wa kibinadamu. Changamoto mbali mbali zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa zinapaswa kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya majadiliano na wala si kwa mtutu wa bunduki. Jumuiya ya Kimataifa bado haijafikia ukomavu mkubwa mintarafu amani duniani “Si vis pacem para bellum”. Kuna unafiki mkubwa kwa nchi na makampuni mbali mbali ya kitaifa na kimataifa yanayozungumzia kuhusu amani duniani, lakini wao hao hao ndio watengenezaji na wasambazaji wakuu wa silaha za kivita.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, kile ambacho kinaonekana kuwa ni Kashfa ya matumizi makubwa ya fedha ya Vatican katika uwekezaji kwenye miundombinu huko London nchini Uingereza, ni matokeo ya usimamizi na udhibiti bora zaidi wa masuala ya fedha unaoendelea kutekelezwa na Mamlaka ya Habari za Kifedha mjini Vatican, AIF, iliyoanzishwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2010 na kufanyiwa marekebisho na Papa Francisko kunako mwaka 2013. Kashfa hii imegunduliwa na wahusika wa ndani kwa sababu ya mfumo thabiti ambao unafanya kazi barabara. Baba Mtakatifu anasema, taratibu, sheria na kanuni zote zilizingatiwa na vyombo vya ulinzi na usalama, vikaomba kibali cha kufanya upekuzi kwa watuhumiwa, ili kubaini ikiwa kama uwekezaji huu ulikuwa umechafuliwa kwa harufu ya rushwa na ufisadi, ili sheria iweze kushika mkondo wake. Hadi sasa watu watano wanatuhumiwa kujihusisha na rushwa! Jambo hili linasikitisha sana kwa sababu linatendeka mjini Vatican.

Usimamizi wa fedha za Kanisa katika: ukweli, uwazi, uadilifu na weledi ni kati ya mambo yanayoendelea kupewa msukumo wa pekee na Baba Mtakatifu Francisko ili kweli rasilimali fedha iweze kutumika kiaminifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kumekuwepo na maendeleo makubwa ambayo yametekelezwa na Mamlaka ya Habari za Kifedha mjini Vatican, AIF. Leo hii Benki Kuu ya Vatican, IOR inaweza kujiendesha kibiashara kama Benki nyingine zilizoko nchini Italia. Mamlaka hii imetia sahihi itifaki ya ushirikiano na vikosi vya inteligensia ya kifedha na nchi kadhaa duniani ili kuweza kubadilishana taarifa; jambo ambalo limeonesha mafanikio makubwa katika upatikanaji wa taarifa muhimu kuhusu masuala ya kifedha Mfumo wa kudhibiti dalili za fedha haramu umeimarishwa zaidi. AIF kunako mwaka 2013 imejiunga na kuwa ni mwanachama wa Kundi la Egmont.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, alipohisi harufu ya rushwa katika ule uwekezaji, aliomba ushauri wa kiufundi ili kushughulikia kesi hii, ili ukweli uweze kujulikana na haki kutawala. Dr. René Brüelhart, Rais wa Baraza la Mamlaka ya Habari za Kifedha Vatican, AIF, amemaliza muda wake, hakumwongozea tena mkataba, ili kutoa nafasi kwa vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi ili kubainisha ukweli wa mambo. Kesi hii itaendelea kufuatiliwa na Moneyval kwa ukaribu zaidi. Utawala wa sheria, taratibu na kanuni za uongozi hazina budi kufuatwa na kutekelezwa na wote, ili haki iweze kushika mkondo wake. Baba Mtakatifu anasema, ni kawaida kutuma salam, matashi mema na baraka kwa wakuu wa Serikali na nchi mbali mbali wakati, Khalifa wa Mtakatifu Petro anapopitia juu ya anga za nchi zao. Demokrasia ni changamoto inayoendelea kuzikumba nchi nyingi duani si tu zile zinazoendelea hata zile ambazo zimeendelea kama Ufaransa, Hispania.

Dhamana na utume wa Vatican katika muktadha wa masuala kama haya ni kukazia: majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ndio ujumbe hata kwa nchi ya Hong Kong ambayo kwa siku za hivi karibuni, imetumbukia katika hali tete ya kisiasa. Baba Mtakatifu anasema, anawapenda watu wa Mungu nchini China na anatamani kwamba, iko siku Mwenyezi Mungu akipenda ataweza kutembelea Peking, nchini China. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, nchi nyingi za Amerika ya Kusini zinakabiliwa na hali tete sana ya kisiasa, kiasi cha kutishia misingi ya haki, amani, usalama, ustawi na maendeleo ya wengi. Brazil, Bolivia na Chile kwa sasa zinakabiliana na hali ngumu ya kisiasa baada ya kutumbukia katika kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Jambo la msingi ni kujenga na kuimarisha misingi ya haki, amani na demokrasia shirikishi. Kwa mfano kesi ya Venezuela, Vatican imekuwa daima mstari wa mbele  kuhamasisha majadiliano katika ukweli na uwazi.

Baba Mtakatifu amewakumbusha waandishi wa habari kwamba, katika maswali yao wamegusia kidogo sana kuhusu amana na utajiri wa watu wa Mungu nchini Thailand. Amewapongeza waandishi wa habari ambao wameendelea kuchangia katika mchakato wa kuragibisha mapambano dhidi ya biashara ya binadamu na viungo vyake sanjari na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo.

Papa: Waandishi wa Habari

 

27 November 2019, 18:10