Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu amewataka waamini kuwa ni mashuhuda wa ukweli, haki, amani, upendo, ukweli na utakatifu. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu amewataka waamini kuwa ni mashuhuda wa ukweli, haki, amani, upendo, ukweli na utakatifu.  (Vatican Media)

Hija ya Papa Francisko nchini Japan: Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme

Baba Mtakatifu amepembua wokovu unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu aliyetundikwa Msalabani; Umuhimu wa waamini kuwa na ujasiri wa kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa kama walivyofanya Mashuhuda wa imani kutoka Japan. Imani ya Kanisa ni kwa ajili ya Mungu aliye hai na kwamba, Mlimani Kalvari, kimya cha mateso na mahangaiko ya watu kinaendelea kusikika!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Yesu Kristo ni Mfalme wa: Kweli, Uzima, Utakatifu, Neema, Haki, Amani na Mapendo. Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu ilianzishwa rasmi na Papa Pius XI, kunako tarehe 11 Novemba 1925 na kutangazwa katika Waraka wake wa kitume “Quas Primas”. Sherehe hii ni kilele cha kazi nzima ya ukombozi wa mwanadamu ambayo Kanisa limeadhimisha katika Mafumbo na Liturujia na kumkiri Kristo Yesu kuwa ni Mfalme wa ulimwengu pamoja na kuualika ulimwengu mzima kutambua kuwa hija ya maisha ya hapa duniani inahitimishwa katika ufalme wa Kristo Yesu aliye “Jana na leo, alfa na omega, mwanzo na mwisho. Baba Mtakatifu Francisko Jumapili tarehe 24 Novemba 2019 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu kwenye Uwanja wa Michezo wa “Baseball”, Nagasaki, nchini Japan, kama sehemu ya hija yake ya kitume nchini humo.

Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amepembua wokovu unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu aliyetundikwa Msalabani; Umuhimu wa waamini kuwa na ujasiri wa kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa kama walivyofanya Mashuhuda wa imani kutoka Japan. Imani ya Kanisa ni kwa ajili ya Mungu aliye hai na kwamba, Mlimani Kalvari, kimya cha mateso na mahangaiko ya watu kinaendelea kusikika! Liturujia ya Neno la Mungu na hasa Injili inaonesha jinsi ambavyo watu kadhaa walivyomkejeli Kristo Yesu pale Msalabani. Ni kelele na matusi kama haya ndiyo yaliyoamsha na kuwagusa watu kutoka katika undani wao, wakawa na huruma iliyochonga mwelekeo wa maisha yao. Yule mhalifu aliyekuwa ametungikwa Msalabani ndiye aliyethubutu kukiri imani yake kwa Yesu na kumwomba amkumbuke katika Ufalme wake. Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu ni fursa ya kukiri tena imani na kuendelea kujisadaka na kujiimarisha zaidi kwa kutambua kwamba, katika historia kuna kusimama na kuanguka; changamoto na mwaliko wa kujizatiti kuwasaidia na kuwahudumia maskini na wale wote wanaoteseka.

Japan katika historia yake imetikiswa sana majanga mbali mbali, lakini waamini wanataka kusimama kidete kukiri imani yao, kumlinda na kumsaidia Kristo Yesu, mtu wa mateso. Wanataka kumsindikiza katika Njia ya Msalaba, anapotengwa na kutelekezwa, ili kwa mara nyingine tena waweze kusikia sauti ya Kristo Yesu ikisema, “Leo hivi utakuwa pamoja nami peponi”. Mtakatifu Paulo Miki na wenzake walikuwa na ujasiri kiasi cha kuyamimina maisha yao, leo hii ushuhuda huu ni sehemu ya amana na utajiri wa maisha ya kiroho. Waamini nchini Japan wanataka kufuata nyayo zao ili kukiri kwa ujasiri kuhusu upendo wa Kristo Yesu uliobubujika kutoka pale Mlimani Kalvari, kwa kushinda kishawishi chuki na uhasama; uchoyo na ubinafsi; dharau na kutotimiza wajibu au ujana usiokuwa na mwelekeo sahihi unaovuruga matendo na maamuzi makini ya maisha. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanazungumzia msaada unaonuiwa kutolewa na Mama Kanisa kwa utendaji wa binadamu kwa njia ya Wakristo kwa kutambua kwamba, hawana uraia wa kudumu hapa duniani, kumbe hawapaswi kuzembea kutekeleza nyajibu zao za kidunia kwani imani yenyewe inawashurutisha zaidi kutekeleza, kadiri ya wito wa kila mmoja wao.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, imani ya Kanisa inakita mizizi yake kwa  Mungu mmoja anayetaka waja wake kupata ukamilifu wa maisha katika Ufalme wa Mungu. Wafuasi wamisionari wa Kristo wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa matumaini na chachu ya Ufalme wa Mungu katika medani mbali mbali za maisha. Wawe ni wahudumu wa maskini, wagonjwa na walemavu; watoto wanaoishi katika mazingira magumu; wakimbizi na wahamiaji, ili wote kwa pamoja waweze kufikia lengo la Ufalme wa mbinguni. Baba Mtakatifu asema kwamba, wote hawa ni Sakramenti hai za Kristo Mfalme; watu ambao Kristo Yesu amejifananisha nao. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa na ujasiri wa kutangaza na kushuhudia imani yao, ili kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu kama ilivyokuwa kwa yule mhalifu pale Msalabani. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kutambua maafa makubwa yaliyosababishwa na Vita Kuu ya Pili ya Dunia na kwa sasa kuna Vita Kuu ya Tatu inayoendelea kupigwana vipande vipande sehemu mbali mbali za dunia. Waamini wawe ni mashuhuda wa Ufalme wa Kristo unaosimikwa katika: kweli, uzima, utakatifu, neema, haki, amani na mapendo.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Joseph Takami, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Japan amemshukuru Baba Mtakatifu kwa uwepo wake nchini Japan kama mwaliko wa kufutilia mbali mashindanio ya utengenezaji wa silaha za kinyuklia, ili kudumisha amani. Iko siku ndoto hii itaweza kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Kati ya Mwaka 1614 hadi mwaka 1873 kuna wamisionari na waamini walei waliouwawa kikatili kama ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Leo hii waamini wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda wa imani kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya matendo; ili kupandikiza mbegu ya upendo kati ya watu wa Mataifa; kwa kuondokana na ubinafsi, ili kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili kupata furaha ya kweli katika maisha.

Papa: Kristo Mfalme
24 November 2019, 14:38