Tafuta

Papa Francisko anaitaka Jumuiya ya Wakristo nchini Japan kusimama kidete kutangaza, kushuhudia na kuhudumia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Papa Francisko anaitaka Jumuiya ya Wakristo nchini Japan kusimama kidete kutangaza, kushuhudia na kuhudumia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! 

Hija ya Papa Francisko nchini Japan: Mashuhuda wa Injili ya uhai

Nia ya Ibada ya Misa Takatifu: Kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, ametafakari kuhusu Heri za Mlimani na upweke hasi unaopelekea watu kukosa furaha na amani; waamini watambue kwamba, maisha ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, Jumuiya ya waamini inapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtindo wa maisha bora ya Mkristo unafumbatwa katika Heri Nane za Mlimani, muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake! Heri za mlimani ni utambulisho  wa Kristo Yesu na ni utambulisho wa Mkristo. Heri za Mlimani ndiyo faraja ya Roho Mtakatifu kwa wale ambao wamekombolewa na kuweka mioyo yao wazi kwa ajili ya kupokea neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kiasi kwamba, wako huru kabisa. Kuna baadhi ya waamini wanajigamba kuwa ni Wakristo kweli kweli, lakini ukiangalia mtindo wa maisha na mwenendo wao ni kinyume kabisa cha mafundisho ya Kristo! Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Japan kuanzia tarehe 23 hadi 26 Novemba 2019 inaongozwa na kauli mbiu “Linda Maisha Yote”. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 25 Novemba 2019 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Tokyo nchini Japan. Nia ya Ibada ya Misa Takatifu ni kwa ajili ya kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, ametafakari kuhusu Heri za Mlimani na upweke hasi unaopelekea watu kukosa furaha na amani; waamini watambue kwamba, maisha ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, Jumuiya ya waamini inapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha maisha. Baba Mtakatifu anasema, Heri za Mlimani ni mwaliko kwa waamini kufuata njia na kuanza kupanda kwenda mlimani, mahali ambapo Mwenyezi Mungu anajifunua mbele ya waja wake. Ni mahali pa kusikiliza kwa utulivu, ili kupata ujumbe wa matumaini, tayari kukutana na maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni katika muktadha huu, waamini wanatambua kwamba wamekirimiwa uhuru wa kutambua kwamba, wao ni watoto wateule wa Mungu. Wakati mwingine, uhuru na utambuzi huu unapekenyuliwa na mashindano yasiyokuwa na tija wala mvuto; kwa kujikita zaidi katika shughuli za uzalishaji na ulaji zinazowapatia utambulisho wao, kiasi cha kushindwa kutambua mambo msingi yanayowazunguka katika maisha.

Hapa watu wanaongozwa na nguvu na kanuni za soko kwamba, kila kitu kinaweza kuzalishwa, kununuliwa au hata kutupiliwa mbali, mambo yanayoushtua moyo! Japan ni nchi ambayo imeendelea sana kiuchumi. Lakini kwa bahati mbaya kuwa wimbi kubwa la watu ambao hawafahamu tena maana ya maisha, kiasi cha kujikuta wanaogelea katika upweke hasi. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la makazi, shule na ukuaji wa jumuiya, lakini tunu msingi zinazowaunganisha watu katika mazingira kama haya zinaendelea kumong’onyoka kila kukicha, kiasi cha watu kubaki wakiwa wamechanganyikiwa na hatimaye, kutumbukia katika upweke hasi. Maandiko Matakatifu yanatoa angalisho kwa waamini kushinda fadhaa na wasi wasi kwa kusumbukia maisha yao kwa mambo mbali mbali kwa sababu kesho itajisumbukia yenyewe. Huu ni mwaliko wa kutekeleza nyajibu na kuendelea kuwajibika barabara; kwa kuwa na vipaumbele katika maisha, yaani kuutafuta kwanza Ufalme wa Mungu na mengine yote watayapata kwa ziada.

Angalisho hapa ni kutokutafuta malimwengu kwa gharama zote, kiasi cha kuhatarisha maisha, hali ambayo inaweza kuwatumbukiza katika hali ya kukosa furaha na hatimaye kuzama katika upweke hasi, hali inayokwamisha mchakato wa maendeleo ya kweli. Baba Mtakatifu anawataka watu wa Mungu nchini Japan kutambua kwamba, maisha ni zawadi adhimu kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayofumbata uzuri na wema unaopaswa kushirikishwa na kutolewa sadaka kwa ajili ya wengine; kwa kutunza mazingira, ambayo yana uhusiano wa pekee katika mchakato unaopania kudumisha udugu wa kibinadamu, haki na uaminifu kwa wengine. Baba Mtakatifu Francisko anaitaka Jumuiya ya Wakristo kujizatiti kikamilifu kulinda, kudumisha na kushuhudia tunu msingi za maisha ya binadamu kwa kuwa ni watu wa shukrani, wenye huruma, wakarimu na wenye uwezo wa kusikiliza kwa ukamilifu. Waamini wajitahidi kupokea zawadi ya maisha kwa unyoofu kwa kutambua kwamba, zawadi hii ni tete sana.

Jumuiya ya Wakristo ijifunze kutambua kwamba, si kila kitu kimefikia ukamilifu wake, lakini kinapaswa kupendwa na kuheshimiwa. Walemavu, wafungwa na wagonjwa ni watu wanaopaswa kupendwa, kama alivyofanya Kristo Yesu kwa kuwasamehe dhambi zao, akawaponya na kuwapatia mahitaji yao msingi. Wakristo wajifunze kusamehe na kusahau. Jumuiya za Kikristo zinapaswa kuwa kama Hospitali iliyoko kwenye uwanja wa mapambano, tayari kupokea na kutibu majeraha; sanjari na kutoa fursa ya msamaha na upatanisho, kwa kuendelea kumwilisha huruma na upendo wa Mungu katika uhalisia wa maisha ya watu. Wakristo nchini Japan wawe ni chachu ya unabii katika jamii, tayari kusimama kidete kulinda na kuhudumia Injili ya uhai!

Askofu mkuu Tarcisio Isao Kikuchi wa Jimbo kuu la Tokyo nchini Japan amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwahimiza kusimama kidete kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kulinda mazingira nyumba ya wote pamoja na kuendeleza utu, heshima na haki msingi za binadamu, kwa kuondokana na upweke hasi. Baba Mtakatifu amekuwa kweli ni shuhuda wa mchakato wa uponyaji, upendo na matumaini kwa Mwenyezi Mungu. Sasa wako tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, cheche za upendo na huruma ya Mungu inayoganga na kuponya!

 

25 November 2019, 15:35