Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anasema mashuhuda wa imani nchini Japan ni chachu ya uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu Francisko anasema mashuhuda wa imani nchini Japan ni chachu ya uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.  (Vatican Media)

Hija ya Papa Francisko nchini Japan: Mashuhuda wa imani Nagasaki

Baba Mtakatifu anasema amekwenda kutoa heshima zake kwa Mashuhuda wa imani, lakini pia kama alama ya shukrani kwa wamisionari wa kwanza na Mashuhuda wa imani kutoka Japan ambao aliwahi kusikia umaarufu wao, uliomtia shime katika maisha yake kama Myesuit. Sadaka yao kamwe haitaweza kusahaulika, kwani ni wao sasa wamekuwa ni chachu ya uinjilishaji mpya nchini Japan.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru wale wote waliojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili nchini Japan; wakajitahidi kuwahudumia watu wa Mungu kwa huruma na upendo, kiasi hata cha kubahatika kuwa na wafiadini kama Mtakatifu Paulo Mikki na wenzake na Mwenyeheri Justo Takayama Ukon, baada ya majaribu makubwa hatimaye, wakayamimina maisha yao kama ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Sadaka ya maisha yao ilisaidia kupyaisha imani miongoni mwa Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo nchini Japan, zikakua na kukomaa na hatimaye, kuzaa matunda ya Kanisa kuendelea kushamiri nchini Japan. Baba Mtakatifu, Jumapili tarehe 24 Novemba 2019 amepata nafasi ya kutembelea na kutoa heshima zake kwenye Mnara wa Kumbu kumbu ya Mashahidi wa Nagasaki walioyamimina maisha yao hapo tarehe 5 Februari 1597. Huu ni mnara unaong’aa na kuangaza ushindi wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Huu ni mnara ambao umeandikwa Heri za Mlimani kwa damu ya Mashuhuda wa imani waliokuwa wamejazwa nguvu ya Roho Mtakatifu, kiasi cha kuwa huru dhidi ya ubinafsi, manung’uniko na kiburi. Hapa ni mahali ambapo mwanga wa Injili ya upendo umeng’aa dhidi ya upanga mkali wa madhulumu! Ni mnara unaotangaza Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, kiasi kwamba, damu ya mashuhuda wa imani sasa imekuwa ni mbegu ya maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, na hivyo kuwaimarisha waamini katika imani, ili hatimaye, waweze kujisadaka bila ya kujibakiza kama wamisionari mitume wanaoweza kusimama kidete kulinda na kutetea maisha kwa njia ya ushuhuda wa huduma kwa wahitaji zaidi! Kwa unyenyekevu mkubwa Baba Mtakatifu anasema amekwenda kutoa heshima zake kwa Mashuhuda wa imani, lakini pia kama alama ya shukrani kwa wamisionari wa kwanza na Mashuhuda wa imani kutoka Japan ambao aliwahi kusikia umaarufu wao, uliomtia shime katika maisha yake kama Myesuit.

Sadaka yao kamwe haitaweza kusahaulika, kwani ni wao sasa wamekuwa ni chachu ya uinjilishaji mpya nchini Japan. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Kanisa nchini Japan licha ya matatizo na changamoto mbali mbali litaendelea kuwa ni alama ya matumaini yanayobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba, mwaliko kwa waamini kushirikishana ule uzuri wa Injili ambayo ni ukweli na uzima. Waamini wawe na ujasiri wa kutua “mizigo” inayowakwamisha kutembea katika njia ya unyenyekevu, uhuru, “parrhesia” yaani “kile kilicho chema na kizuri” pamoja na upendo. Hawa ni mashuhuda wa imani katika Karne ya Ishirini na Moja, changamoto na mwaliko wa kuchuchumilia na kuambata Heri za Mlimani; Uhuru wa Kuabudu na Kidini; Kwa kutokubali sera zinazoweza kuwatumbukiza watu katika misimamo mikali ya kidini na kiimani; utengano na ubaguzi, siasa kali na mambo yote yanayotaka kuvuruga matumaini ya watu wa Mungu kwa siku za mbeleni. Baada ya hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amewaongoza waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema waliohudhuria kusali Sala ya Malaika wa Bwana!

Papa: Mashuhuda wa Imani
24 November 2019, 15:28