Tafuta

Vatican News
Papa Francisko amekazia umuhimu wa kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo kwa ufanisi zaidi! Papa Francisko amekazia umuhimu wa kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo kwa ufanisi zaidi!  (Vatican Media)

Hija ya Papa Francisko nchini Thailand: Majadiliano ya kidini

Papa katika hotuba yake kwa viongozi mbali mbali wa dini nchini Thailand amegusia kuhusu umuhimu wa dini duniani kushirikiana na kushikamana ili kukabiliana na changamoto mamboleo, kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Amesisitizia utume wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu katika ulimwengu mamboleo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chuo Kikuu cha Chulalongkorn, kilianzishwa kunako mwaka 1917 kwa heshima ya Mfalme Chulalongkorn aliyemtembelea Papa Leo XIII kunako mwaka 1897, mwanzo wa majadiliano ya kidini pamoja na mchakato wa kupambana na biashara ya utumwa duniani. Lengo la Chuo Kikuu hiki ni kutoa elimu bora kwa familia ya Mungu nchini Thailand bila ubaguzi na kilibahatika kutembelewa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1984. Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 22 Novemba 2019 wakati wa hija ya 32 ya kitume nchini Thailand amepata bahati ya kukitembelea na kuwashirikisha wanajumuiya wake vipaumbele katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro yaani: Upendeleo kwa maskini, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote sanjari na majadiliano ya kidini na kiekumene ili kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho kati ya watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa viongozi mbali mbali wa dini nchini Thailand amegusia kuhusu umuhimu wa dini mbali mbali duniani kushirikiana na kushikamana ili kukabiliana na changamoto mamboleo, kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Amesisitizia utume wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu katika ulimwengu mamboleo! Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza viongozi mbali mbali wa dini nchini Thailand kwa kuchagua tunu, amana na urithi wa maisha yao kiroho katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Thailand. Majadilaino ya kidini na kiekumene yanapania pamoja na mambo mengine kujenga na kuimarisha moyo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ili kusimama kidete kupambana na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Leo hii, Jumuiya ya Kimataifa inakabiliwa na athari za mtikisiko wa uchumi na masuala ya fedha; maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, vita, kinzani na mipasuko mbali mbali bila kusahau athari za mabadiliko ya tabianchi. Haya ni matukio yanayounda historia ya watu wa nyakati hizi wanaohitaji kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana; kujenga na kudumisha umoja na mshikamano sanjari na kufahamiana ili kwa pamoja, kuweza kusimama kidete kulinda na kutunza kazi ya uumbaji.

Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kushirikishwa kikamilifu ili kulinda na kutunza mazingira, kwa kusimamia misingi ya haki na amani, ili kujielekeza zaidi katika mtindo wa maisha ambao ni fungamani. Majadiliano ya kidini na kiekumene yasaidie kudumisha misingi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu; amana na utajiri wa maisha ya kiroho na kiutu; mambo ambayo yanaweza kutolewa ushuhuda ikiwa kama waamini wa dini mbali mbali wataweza kujenga utamaduni wa kukutana bila hofu. Waamini wa dini mbali mbali wanaitwa na kutumwa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wote waliovunjika na kupondeka moyo, kwa kushirikiana na kushikamana kwa pamoja kama ndugu wamoja. Wanapaswa kusimama kidete kulinda utu wa binadamu, haki msingi pamoja na uhuru wa kuabudu. Nchi ya Thailand imebarikiwa kuwa na utajiri na uzuri wa maliasili, wanaoweza kuwashirikisha watu wengine sehemu mbali mbali za dunia.

Heshima kwa wazee na watu wazima ni msingi unaoweza kuisaidia jamii kurithisha tunu msingi za maisha ya kiutu na kitamaduni kwa vijana wa kizazi kipya. Vijana wafundwe kuthamini amana na utajiri wa historia ya watu wao; waendeleze kumbu kumbu ili hatimaye, waweze kufanya maamuzi mazito katika maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, amekazia umuhimu wa vyuo vikuu pamoja na taasisi za elimu ya juu katika mchakato wa kupunguza matabaka ndani ya jamii; kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha haki jamii, utu, heshima na haki msingi za binadamu; suluhu ya amani katika migogoro mbali mbali inayojitokeza ndani ya jamii, daima mkazo ukiwa ni kulinda uhai wa binadamu. Vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu viwe ni mahali pa kuwarithisha vijana hekima na busara; ni mahali pa vijana kupewa stadi za maisha, ujuzi na maarifa. Kila mwamini anahamasishwa kuwa ni mjenzi wa utamaduni unaoimarisha umoja, heshima, amani na utulivu.

Papa: Majadiliano
22 November 2019, 17:04