Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amehimiza ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana ili kujenga dunia inayosimikwa katika haki na udugu. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amehimiza ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana ili kujenga dunia inayosimikwa katika haki na udugu.  (AFP or licensors)

Hija ya Papa Francisko nchini Japan: Hotuba kwa viongozi wa kisiasa na wanadiplomasia

Papa Francisko amegusia: Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Japan; amehimiza mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana ili kuwa na mwono mpana wa ujenzi wa dunia inayosimikwa katika haki na udugu na kwamba, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni sehemu ya mchakato wa kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kauli mbiu iliyochaguliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Japan kwa ajili ya hija ya 32 ya Baba Mtakatifu nchini Japan kuanzia tarehe 23-26 Novemba 2019 ni: “Linda Maisha Yote”. Huu ni ujumbe mzito unaotikisa “sakafu ya nyoyo za watu” ili kusimama kidete kulinda: haki, tunu msingi, utu na heshima ya binadamu dhidi ya vitisho vinavyohatarisha misingi ya amani na utulivu na hasa zaidi mashindano na umiliki wa silaha za kinyuklia. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 25 Novemba 2019 amemtembelea Mfalme Naruhito wa Japan na kufanya naye mazungumzo ya faragha pamoja na kumtakia heri na fanaka kwa kuanza awamu mpya ya uongozi wake. Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na Bwana Shinzo Abe, Waziri mkuu wa Japan na baadaye akatoa hotuba kwa viongozi wa serikali na wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi zao huko Japan. Baba Mtakatifu katika hotuba yake akazia uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Japan; amehimiza mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana ili kuwa na mwono mpana zaidi wa ujenzi wa dunia inayosimikwa katika haki na udugu wa kibinadamu.

Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni sehemu ya mchakato wa kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu! Tangu mwanzo, wamisionari wa kwanza walipowasili nchini Japan kumekuwepo na uhudiano mzuri wa kidiplomasia kati ya Vatican na Japan; uhusiano ambao umeendelea kuimarishwa kwa njia ya tamaduni pamoja na ziara za kidiplomasia ambazo zimesaidia sana kudhibiti kinzani na matatizo baina ya nchi hizi mbili, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anasema, hija yake ya kitume nchini Japan inapania kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo, ili waendelee kujisadaka bila ya kujibakiza katika huduma kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kauli mbiu inaoongoza hija hii ni “Linda Maisha Yote” , kwa kutambua na kuthamini utu wa mwanadamu; kwa kuendelea kujenga na kuimarisha mshikamano wa upendo kwa ajili ya watu wenye shida mbali mbali.

Katika hija yake nchini Japan, amepata nafasi ya kusikiliza kwa makini shuhuda zilizotolewa na waathirika wa tetemeko la ardhi, tsunami pamoja na madhara yaliyosababishwa na mtambo wa nyuklia wa Fukushima Daiichi na kwamba, ameguswa kwa namna ya pekee na mahangaiko pamoja na mateso ya wananchi hawa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, anaendelea kufuata nyayo za watanguliz wake katika mjadala unaopania kudumisha amani inayotishwa sana na mashindano ya silaha: Utengenezaji pamoja na mchakato wa ulimbikizaji wa silaha duniani! Utumiaji wa silaha za atomiki ulisababisha maangamizi makubwa kwa miji ya Hiroshima na Nagasaki, tukio hili ambali lilitikisa historia ya binadamu, lisijirudie tena na kwamba, kinzani zinazojitokeza kati ya mataifa zipatiwe ufumbuzi kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kupata amani ya kudumu. Suala la nguvu za kinyuklia linapaswa kushughulikiwa kikamilifu kwa kuwa na taasisi ambayo itakuwa na uwezo wa kuchakata masuala mbali mbali ili kuapata muafaka wa kimataifa.

Kumbe, ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana, ukiwa umejikita katika hekima na busara na mwono mpana wa mambo ni muhimu sana katika ujenzi wa dunia inayosimikwa katika haki na udugu wa kibinadamu. Japan iko mstari wa mbele katika falsafa ya utamaduni wa watu kukutana kwa njia ya elimu, tamaduni, michezo, utalii mambo yanayojenga na kudumisha utulivu, haki, mshikamano na upataniso, kiungo muhimu sana katika kukuza amani duniani. Michezo imekuwa ikiwaunganisha hata wale wanaodhaniana kuwa ni maadui. Michezo ya Olympic itakayoadhimishwa nchini Japan, 2020 itasaidia kujenga moyo wa mshikamano unaovuka mipaka ya kikanda na kimataifa kwa ajili ya mafao ya binadamu wote. Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu ilitiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.

Huu ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Japan katika historia ya maisha yake, imejitahidi sana kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho; kwa kukuza mahusiano ya dini mbali mbali ambayo yamesaidia mchakato wa ujenzi wa amani sanjari na kuwasaidia vijana wa kizazi kipya kuzama zaidi katika kanuni maadili na utu wema kama msingi wa ujenzi wa jamii yenye utu na inayosimikwa katika haki.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu ni kwa ajili ya mustakabali wa familia ya binadamu kwa siku za mbeleni kwa kuhimiza majadiliano kama njia muafaka ya ushirikiano na kanuni katika mchakato wa kufahamiana. Baba Mtakatifu amefurahishwa na mazingira mazuri yaliyoko nchini Japan, changamoto na mwaliko wa kuyalinda na kuyaendeleza ili yasikumbwe tena na majanga asilia bali hata na uchoyo na unyonyaji unaofanywa kwa mikono ya binadamu. Changamoto ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni kilio cha vijana wengi duniani, wanaohitaji kupata majibu ya uhakika yanayotekelezwa kwa vitendo. Utunzaji bora wa mazingira ni sehemu ya ekolojia ya binadamu inayopania kupunguza pengo kubwa kati ya maskini na matajiri katika mfumo wa uchumi kimataifa; “kwa matajiri kuendelea kuneemeka na maskini kupukutika kama nzige”.

Baba Mtakatifu anaipongeza Japan kwa kuweka sera na mikakati madhubuti katika kupambana na umaskini nchini humo na kwamba, juhudi hizi zinapaswa kuendelezwa hata katika uwanja wa Jumuiya ya Kimataifa, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili kukuza uchumi shirikishi na hivyo kuondokana na baadhi ya watu kutumbukia katika upweke hasi na hali ya kujikatia tamaa ya maisha. Ubora wa sera za uchumi unapimwa kwa juhudi za kulinda na kudumisha uhai wa binadamu. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru viongozi wa Japan kwa mwaliko wa kutembelea nchi yao. Anawashukuru kwa ukarimu na kuwataka kuendelea kujizatiti katika kulinda na kudumisha maisha, utu na haki msingi za binadamu.

hotuba Viongozi
25 November 2019, 16:25