Tafuta

Papa Francisko akiwa mjini Hiroshima, Japan amesema amani ya kweli inasimikwa katika msingi wa: Ukweli, haki, upendo na uhuru kama ulivyofafanuliwa na "Pacem in Terris" Papa Francisko akiwa mjini Hiroshima, Japan amesema amani ya kweli inasimikwa katika msingi wa: Ukweli, haki, upendo na uhuru kama ulivyofafanuliwa na "Pacem in Terris" 

Hija ya Papa Francisko nchini Japan: Hiroshima: Amani Duniani!

Papa Francisko amezungumzia: Madhara ya vita; misingi ya amani duniani kama inavyofafanuliwa na Mtakatifu Yohane XXIII. Amekazia umuhimu wa kukumbuka, kutembea na kulinda kwa pamoja kama njia ya kudumisha amani duniani. Hiroshima ni mji ambao ndoto na matumaini ya watu yalitoweka na kuwaachia watu maafa makubwa ambayo kamwe hayataweza kusahaulika kwa urahisi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Michezo wa “Baseball”, Nagasaki, aliondoka na kuelekea mjini Hiroshima umbali wa Km 461 kutoka Nagasaki. Hiroshima maana yake ni “Kisiwa Kikubwa”. Baba Mtakatifu amekwenda moja kwa moja hadi kwenye Uwanja wa Kumbu kumbu ya Amani Hiroshima na huko amelakiwa na viongozi wa Serikali na Kanisa pamoja na kuweka sahihi kwenye Kitabu cha wageni mashuhuri mjini hapo. Amesikiliza shuhuda za wahanga wawili: Yoshiko Kajimoto pamoja na Koji Hosokawa. Wameelezea jinsi walivyoshuhudia marafiki zao wakizikwa wangali hai baada ya kufunikwa na kifusi cha udongo, kufumba na kufumbua wakaona mji wote umeteketea na kutoweka kabisa, giza nene likaufunika mji wa Hiroshima na harufu mbaya ikaanza kusikika na hapo kukawa na milipuko mbali mbali. Zaidi ya watu 140, 000 kati ya watu 350, 000 waliokuwa wanaishi hapo wakapoteza maisha.

Hiroshima ukageuka kuwa ni makaburi ya watu wake; wengi waliathirika na hatimaye kufariki dunia kutokana na mionzi ya nyuklia. Hata leo hii kuna maelfu ya watu ambao wameathirika kutokana na mashambulizi ya mabomu ya nyuklia. Shuhuda za waathirika wa mashambulizi ya nyuklia mjini Hiroshima ziwe ni fundisho kuhusu madhara makubwa yanayoweza kusababishwa na matumizi ya silaha za maangamizi kama ilivyokuwa mjini Nagasaki na Hiroshima. Ni wajibu na dhamana kwa vijana wa kizazi kipya kuwa kweli ni vyombo na wajenzi wa amani duniani. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, amezungumzia kuhusu: madhara ya vita; misingi ya amani duniani kama inavyofafanuliwa na Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa Kitume, “Pacem in terris” yaani: “Amani Duniani”. Amekazia umuhimu wa kukumbuka, kutembea na kulinda kwa pamoja kama njia ya kudumisha amani duniani. Baba Mtakatifu anasema, Hiroshima ni mji ambao ndoto na matumaini ya watu yalitoweka na kuwaachia watu maafa makubwa ambayo kamwe hayataweza kusahaulika kwa urahisi.

Baba Mtakatifu anasema amekuja Hiroshima ili kutoa heshima yake kwa waathirika wa mashambulizi ya mabomu ya atomiki na kwamba, yuko kati yao kama hujaji wa amani katika ukimya na sala, ili kuwakumbuka na kuwaombea wale wote wanaotaka kujizatiti katika mchakato wa kutafuta amani. Moyoni wake amebeba machozi na masikitiko ya maskini ambao ndio waathirika wakubwa wa vita, chuki na kinzani mbali mbali. Baba Mtakatifu anasema, yuko kati kati yao kama sauti ya watu wasiokuwa na sauti; shuhuda wa ukosefu wa haki; mambo yanayotishia: amani na mafungamano ya kijamii; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na vita inayohatarisha mustakabali wa amani duniani. Matumizi ya silaha za nyuklia ni uhalifu dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja mazingira nyumba ya wote. Hakuna amani ya kweli wakati bado kuna mashindano ya utengenezaji wa silaha duniani; kuna sera za kibaguzi, chuki na uhasama.

Ikumbukwe kwamba, amani ya kweli inasimikwa katika misingi ya: Ukweli, haki, upendo na uhuru wa kweli kama anavyofafanua Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa Kitume “Pacem in terris” yaani: “Amani Duniani”. Kimsingi, watu wanatofautiana kwa mambo mengi sana, lakini kanuni hizi zinaweza kutumika ili kuheshimu na kuwawajibisha wanasiasa, ili kujizatiti katika kudumisha mafao ya wengi. Hii ni changamoto kwa watu wa Mungu kudumisha upendo, kwa kukuza majadiliano, mshikamano na matumizi bora zaidi ya nguvu kazi. Amani duniani inahatarishwa sana kutokana na vitisho vya silaha za nyuklia. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, amani siyo tu kutokuwepo kwa vita, bali ni matunda ya haki, maendeleo, mshikamano, utunzaji bora wa mazingira pamoja na kusimamia mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anasema, Hiroshima iwe ni kumbu kumbu, ili watu wajitahidi kutembea kwa pamoja, kulinda na kudumisha misingi ya amani duniani.

Watu wasimame na kuthubu kusema, hatutaki tena vita! Watu wa Mungu wathubutu kujenga matumaini kwa kuwa ni vyombo vya upatanisho na haki na kwamba, wote wanayo hatima moja katika maisha. Kumbe, watu wote wanapaswa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya mustakabali wa maisha yao kwa siku za usoni. Huu ni wakati wa kukataa katu katu utengenezaji na majaribio ya silaha za nyuklia. Watu wana kiu ya haki na amani ya kudumu.

Papa: Amani Duniani
24 November 2019, 15:05