Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 19-26 Novemba 2019 anafanya hija ya 32 ya Kitume Barani Asia ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo! Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 19-26 Novemba 2019 anafanya hija ya 32 ya Kitume Barani Asia ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo!  (AFP or licensors)

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Asia! Kumekucha!

Takwimu zinaonesha kwamba, Bara la Asia ni kati ya Mabara yenye idadi kubwa ya watu duniani. Vipaumbele vya jumla: kuwaimarisha waamini wa Kanisa Katoliki katika misingi ya imani, matumaini na mapendo; kukuza na kudumisha utamaduni wa majadiliano ya kidini na kiekumene; kuunga mkono jitihada za Jumuiya ya Kimataifa za kupiga rufuku matumizi ya silaha za nyuklia duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 19-26 Novemba 2019 Barani Asia kwa kutembelea: Thailand na Japan ni sehemu ya mchakato wa Kanisa wa kutaka kudumisha majadiliano ya kidini na kitamaduni ili kulinda: utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo, mafao ya wengi, haki na amani duniani na kwa namna ya pekee Barani Asia. Katika kipindi cha miaka mitano ya utume wake, Baba Mtakatifu Francisko amekwisha kutembelea nchi 51 duniani. Dr. Matteo Bruni Msemaji mkuu wa Vatican katika taarifa yake kwa vyombo vya habari amebainisha kwamba, hija hii ya kitume ni kati ya safari ndefu kuwahi kufanywa na Baba Mtakatifu, ukiachilia mbali ile hija yake ya kitume nchini Chile na Perù. Baba Mtakatifu anatarajiwa kutoa hotuba na mahubiri yatakayotafsiriwa kwa lugha za watu mahalia na Sr. Ana Rosa Sivori, Mmisionari wa Shirika la Wamisionari wa Bikira Maria Msaada wa Wakristo anayetekeleza utume wake nchini Thailand.

Wa pili kattika orodha hii ni Padre Renzo de Luca, Mkuu wa Shirika la Wayesuit, Kanda ya Japan, aliyetumwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati huo akiwa nchini Argentina. Baba Mtakatifu anarejea tena Barani Asia baada ya hija yake ya kitume nchini Korea mwaka 2014, Sri Lanka na Ufilippini mwaka 2015; Myanmar na Bangaladesh mwaka 2017. Takwimu zinaonesha kwamba, Bara la Asia ni kati ya Mabara yenye idadi kubwa ya watu duniani. Vipaumbele vya jumla: kuwaimarisha waamini wa Kanisa Katoliki katika misingi ya imani, matumaini na mapendo; kukuza na kudumisha utamaduni wa majadiliano ya kidini na kiekumene; kuunga mkono jitihada za Jumuiya ya Kimataifa za kupiga rufuku matumizi ya silaha za nyuklia duniani ili kudumisha amani na utulivu. Baba Mtakatifu Francisko anafuata nyayo za Mtakatifu Yohane Paulo II aliyetembelea nchi hizi kunako mwaka 1984 na Mwaka 1981. Licha ya Kanisa Katoliki kuwa na idadi ndogo sana ya waamini katika nchi hizi mbili, lakini, limekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu hususan katika huduma ya afya, elimu, ustawi na maendeleo ya wengi.

Baba Mtakatifu anaanza hija hii ya kitume, Jumanne jioni tarehe 19 Novemba 2019 na anatarajiwa kuwasili Bankok, Thailand, Jumatano, tarehe 20 Novemba 2019 majira ya asubuhi. Kwa ufupi, Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 19-23 Novemba 2019 anafanya hija ya 32 ya kitume nchini Thailand inayoongozwa na kauli mbiu: “Mitume wa Kristo, Wamisionari Mitume”. Hija hii ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 350 tangu kuanzishwa kwa utume wa Vikarieti ya Siam kunako mwaka 1669. Katika ulimwengu mamboleo ambamo watu wanaonja ukosefu wa amani, misigano, kinzani na utengano, mambo yanayo hatarisha umoja na mafungamano ya kijamii, utu na heshima ya mwanadamu, kuna haja kwa watu wote kushikamana ili kudumisha maendeleo ya kweli kwa ajili ya familia binadamu; kwa kukazia mshikamano katika haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Haya ni mambo ambayo Baba Mtakatifu Francisko anataka kuyapatia kipaumbele wakati wa hija yake ya kitume nchini Thailand.

Kuanzia tarehe 23 hadi 26 Novemba 2019,  Baba Mtakatifu atakuwa nchini Japan na hija hii inaongozwa na kauli mbiu “Linda Maisha Yote”. Pamoja na mambo mengine, Baba Mtakatifu anapania kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini, haki na amani. Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kutembelea Hiroshima na Nagasaki kama alivyofanya Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1981. Atakutana na kuzungumza na waathirika wa tetemeko la ardhi na Tsunami iliyoleta madhara makubwa katika mtambo wa Nyuklia wa Fukushima na vitongoji vyake kunako mwaka 2011. Ujumbe wa Baba Mtakatifu mjini Nagasaki ni wazi kabisa, matumizi ya nishati ya atomiki kwa ajili ya vita ni vitendo ambavyo vinakwenda kinyume kabisa cha kanuni maadili. Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linasema, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, yanayopaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa. Maandiko Matakatifu yanabainisha kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye aliyeumba dunia na kuifanya, ndiye aliyeifanya imara, hakuimba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu. Ili kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu kuna haja wanasema Maaskofu kusimama kidete kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote.

Papa: Barani Asia
18 November 2019, 15:32