Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI amesimulia historia, umuhimu na changamoto zilizoko wakati huu Tume ya Taalimungu Kimataifa inapoadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya uwep na utume wake. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI amesimulia historia, umuhimu na changamoto zilizoko wakati huu Tume ya Taalimungu Kimataifa inapoadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya uwep na utume wake. 

Papa Mstaafu Benedikto XVI: Historia na Umuhimu wa Tume ya Taalimungu Kimataifa.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika ujumbe wake kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Tume ya Taalimungu Kimataifa ianzishwe na Mtakatifu Paulo VI anasema, haya ni matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican sanjari na maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu. Amegusia historia, kinzani zilizojitokeza, changamoto na matumaini kwa siku za mbeleni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tume ya Taalimungu Kimataifa katika kipindi cha Mwaka 2019 inaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake kama sehemu ya matunda ya maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu, mchakato ulioanzishwa na Mtakatifu Paulo VI, ili kuwasaidia viongozi wa Kanisa kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao kama sehemu ya Mamlaka funzi ya Kanisa. Kanisa kwa busara kabisa lilianzisha pia Tume ya Biblia Kimataifa iliyokuwa inamsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kutoa ufafanuzi wa Maandiko Matakatifu na hiyo imekuwepo hata kabla ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Ni katika muktadha huu, Mtakatifu Paulo VI kwa hekima na busara ya kichungaji, akatamka kwamba, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa ndiye Rais wa Tume ya Taalimunhu Kimataifa na Tume ya Biblia Kimataifa na kwamba, tume hizi, zinawachagua Makatibu wake wakuu kutoka miongoni mwa wajumbe wa tume hizi mbili. Baadaye cheo cha katibu mwambata kiliongezwa, ili kuhakikisha kwamba, tume hizi zinapata msaada unaotakikana kwa wakati!

Huu ni ufafanuzi wa kihistoria uliotolewa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika ujumbe wake kwa Tume ya Taalimungu Kimataifa inapoadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Kazi mbali mbali zilizochapishwa na Tume ya Taalimungu Kimataifa kuanzia mwaka 1971 ziliwasaidia sana Maakofu katika maadhimisho ya Sinodi mbali mbali na baadaye, kuanzishwa utamaduni wa kuchapisha Wosia wa Kitume mara baada ya maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu. Tume hizi zilikuwa zinashiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi kwa kutoa wataalam waliobobea katika mada zilizokuwa zinajadiliwa, ili hatimaye, waweze kumshauri Khalifa wa Mtakatifu Petro anapochapisha Wosia wake wa Kitume. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anasema, ameshangazwa sana katika kipindi cha Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Tume hii ilijikuta inashindwa kutafsiri na kumwilisha mawazo makuu ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na matokeo yake, wanataalimungu mabingwa kama: Henri de Lubac, Yves Congar, Karl Rahner na wenzao hawakupata nafasi ya kuweza kushiriki katika maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Kuna wanataalimungu mashuhuri kama Hans Urs Von Balthasar Louis Bouyer, Padre Marie Joseph Le Guillou aliyeshughulikia nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kiasi hata cha kujikuta anapatwa na ugonjwa “Parkinson” na huo ukawa ni mwisho wa mchango wake katika taalimungu. Kuna baadhi ya wanataalimungu mashuhuri waliosukumiziwa kwenye “Kambi ya Upinzani” kiasi kwamba, hata mchango wao hakuthaminiwa tena kuwa ni sehemu ya amana na utajiri wa mafundisho ya Kanisa. Kuna mabingwa wa taalimungu waliokuwa wamebobea katika tasaufi ya maisha ya kiroho na majadiliano ya kiekumene ndani ya Kanisa, wakajikuta hawawezi “kufua tena dafu”, Karl Rahner na wenzake, wakaamua kujiweka pembeni. Katika kipindi cha Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Tume ya Kitaalimungu Kimataifa, baadaye waliibuka wanataalimungu mahiri kutoka katika lugha ya Kitalia. Hawa ni akina Padre Carlo Caffarra na Padre Raniero Cantalamessa.

Kwa lugha ya Kijerumani Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, anamkumbuka Karl Lehmann alichakarika usiku na mchana na matunda ya kazi zake yanaanza kuonekana wakati huu. Lengo la mchango huu wa kihistoria ni kuonesha uhusiano wa karibu uliokuwepo kati ya Tume ya Taalimungu Kimataifa na Mamlaka Funzi ya Kanisa, yanayopaswa kufanyiwa upembuzi yakinifu kwa ajili ya mafao ya Kanisa. Chanzo na mchango wa Tume hii katika kipindi cha Miaka 50 ya maisha na utume wake, ni mambo yanayopaswa kusikilizwa tena na kufanyiwa tafakari ya kina. Karl Lehmann alichangia sana katika nyaraka za “Gaudium et spes” yaani “Kanisa katika Ulimwengu mamboleo kama chombo cha furaha na matumaini ili kushughulikia kwa kina na mapana maendeleo fungamani ya binadamu na wokovu wa Kikristo. Taalimungu ya ukombozi, ikaingizwa hapa ili kuokoa maisha na utume wa Kanisa huko Amerika ya Kusini, kwa kulitaka Kanisa kuwekeza katika uhalisia wa maisha ya watu: kisiasa na kiuchumi.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anaendelea kudadavua kwamba, uhusiano kati ya Mamlaka Funzi ya Kanisa na mafundisho ya Kitaalimungu ni kati ya majukumu mazito ambayo yamekuwa yakifanyiwa kazi na Tume ya Taalimungu Kimataifa na kwamba, hili limekuwa ni tatizo kubwa kwa taalimungu maadili. Matokeo yake ni wanataalimungu kama Heinz Schurman na Hans Urs Von Barthasar wakajikuta wanapoteza mwelekeo kuhusu Sakramenti ya Ndoa na Kanisa kufuata mwelekeo wa William May, mwamini mlei aliyekuwa ameoa na kubahatika kupata watoto wengi hawakuweza kufikia malengo yao kama ilivyokuwa pia kwa  wanataalimgu kutoka nchini Poland kama vile Prof. Andrzej Szoztek na Padre Servais Pinckaers akia amekita mawazo yake kwenye mafundisho ya Mtakatifu Thoma wa Akwino kuhusu maadili na fadhila za Kikristo naye hakupata ushirikiano wa kutosha! Mtakatifu Yohane Paulo II ajikita sana mafundisho yake katika taalimungu maadili na matokeo yake ni Wosia wa Kitume wa Veritatis splendor, uliochapishwa tarehe 6 Agosti 1993 baada ya kuchapishwa kwa Katekisim ya Kanisa Katoliki.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anakaza kusema, bado kuna tatizo na changamoto kati uhusiano kati ya Mamlaka Funzi ya Kanisa, mafundisho ya Kitaalimungu na taalimungu maadili. Tume ya Taalimungu Kimataifa inapaswa kuendelea kulishughulia tatizo hili na hatimaye kupata muafaka wa kudumu. Tume hii inapaswa pia kuwa ni jukwaa la kuliwezesha Kanisa kusikiliza sauti na kilio cha Makanisa machanga duniani yaani sauti kutoka Barani Afrika na Asia katika ujumla wake ili kuunda utamaduni mpya wa kitaalimungu sanjari na mchakato wa majadiliano ya kidini. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI baada ya kudadavua historia, dhamana, utume na kinzani zilizojitokeza katika Tume ya Taalimungu Kimataifa anapenda kuipongeza Tume hii katika jitihada zake za kuunganisha ili hatimaye, Kanisa liweze kuwa na taalimungu maadili moja pamoja na kudumisha mshikamano wa wanataalimungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Tume hii ni sauti makini inayopaswa kusikilizwa, kama chemchemi ya historia na amana ya Kanisa; dira, mwelekeo na matumaini kwa siku za mbeleni kama njia ya kushuhudia ufunuo wa Mungu. Tume hii imekuwa ni msada mkubwa kwake binafsi ili kuweza kukutana na lugha pamoja na mawazo kutoka katika tamaduni mbali mbali katika mchakato wa kutafuta Ukweli mpana zaidi katika hali ya unyenyekevu.

Benedikto XVI: Ujumbe
29 November 2019, 18:05