Tafuta

Watakatifu wapya ni mahujaji wa imani iliyomwilishwa katika upendo, kielelezo cha shukrani kwa Mwenyezi Mungu! Watakatifu wapya ni mahujaji wa imani iliyomwilishwa katika upendo, kielelezo cha shukrani kwa Mwenyezi Mungu! 

Watakatifu Wapya 2019: Mahujaji wa imani mapendo kwa maskini!

Watakatifu wapya ni mahujaji wa imani na waombezi wa watu wa Mungu. Kati yao kuna watawa watatu wanaoonesha kwamba, maisha ya kitawa ni hija ya upendo kuekelea katika vipaumbele vya maisha ya maskini.. Mt. Margarita ni shuhuda wa sala inayomwilishwa katika maisha ya kila siku. Kardinali Newman ni shuhuda wa utakatifu unaojikita kujikita katika amani na utulivu wa ndani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ushuhuda wa furaha ya maisha ya Kikristo  ni chemchemi ya wito wa utakatifu wa maisha unaoweza kumwilishwa sehemu na mahali popote pale; kwa watu wa rika na hali tofauti za kijamii. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 13 Oktoba 2019, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amewatangaza watakatifu wapya watano. Hawa ni: Kardinali John Newman, muasisi wa Kituo cha Michezo cha Mtakatifu Filippo Neri kilichoko nchini Uingereza. Sr. Giuseppina Vannini, Muasisi wa Shirika la Mabinti wa Mtakatifu Camillus; Maria Theresa Chiramel Mankidiyan, Muasisi wa Shirika la Watawa wa Familia Takatifu; Sr. Dulce Lopes Pontes wa Shirika la Watawa Wamisionari wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili na Mama wa Mungu pamoja na Margarita Bays, Bikira na mtawa wa Utawa wa tatu wa Mtakatifu Francisko wa Assisi.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amewataka waamini kujizatiti katika safari ya imani inayo okoa, kwa kufuata mfano wa wale wakoma kumi walioponywa na Kristo Yesu; kwanza kabisa, walimwomba ili awaponye, akawaambia kutembea kwenda kujionesha kwa Makuhani na hatimaye, Msamaria, akarejea kumpa Mungu utukufu. Ikumbukwe kwamba, wagonjwa wa Ukoma walitengwa na jamii na ndiyo maana hata walipomwendea Kristo Yesu, walisimama mbali, lakini wakapaaza sauti, kulilia huruma na upendo wa Mungu unaoponya na kuokoa; huruma inayowawezesha wale waliosetwa na kunyong’onyezwa na udhaifu wao wa kibinadamu kuweza kusimama tena, kwa sababu Mwenyezi Mungu anasikiliza na kujibu kilio cha waja wake, waliopweke na wanaoteseka.

Kama ilivyokuwa kwa wale wakoma, waamini nao wanahitaji kugangwa na kuponywa udhaifu unaowafanya kushindwa kujiamini wao wenyewe, katika maisha na matokeo yake, wanakuwa ni watumwa na hatimaye kuganda kwenye: Luninga, matumizi haramu ya dawa za kulevya, michezo ya kamari na upatu; fedha na mali, matumizi mabaya ya simu za viganjani pamoja na tabia ya kuwahukumu wengine vibaya. Mwenyezi Mungu anaganga, anaponya na kuwaweka huru waja wake, ikiwa kama watathubu kumwomba kwa imani, ili kuwaponya na ubinafsi unaowafunga katika undani wao; dhambi na ubaya wa moyo pamoja na woga usiokuwa na mashiko. Wagonjwa wa Ukoma ni watu wa kwanza kabisa kuomba huruma ya uponyaji kutoka kwa Kristo Yesu, baadaye akafuatia kipofu na hatimaye, yule mhalifu aliyesulubiwa pamoja na Yesu pale Mlimani Kalvari. Jina la Yesu maana yake, Mungu anaokoa!

Kumwita Mwenyezi Mungu kwa jina lake halisi ni kielelezo makini cha mwamini anayejiaminisha mbele ya Mungu, na ni chachu ya kukua na kukomaa kwa imani, kwa kumwekea wazi Kristo Yesu, udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Yesu kwa sababu Mungu anaokoa. Anawataka kusali kwa sababu sala ni mlango wa imani na dawa ya maisha ya kiroho! Hatua ya pili katika safari ya imani ni kutembea kama ilivyokuwa kwa wale wakoma kumi, ikawa walipokuwa wakienda wakatakasika. Mwenyezi Mungu anawaganga na kuwaponya waja wake katika safari ya maisha ya kila siku. Imani inawataka watu wa Mungu kutoka katika “bandari salama” na “viota vya maisha yao”, kwa sababu imani inaongezeka kwa njia ya sadaka na inakomaa katika majaribu na inadumu kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu katika unyenyekevu kama ilivyokuwa kwa wale wakoma na Naamani, Jemedari mpagani.

Huu ni mwaliko kwa waamini kukuza imani kwa njia upendo mnyenyekevu unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha, katika uvumilivu wa kila siku, kwa kumwita Kristo Yesu na kusonga mbele kwa imani na matumaini thabiti! Hatua nyingine muhimu katika kukuza na kudumisha imani inayooneshwa na wale wakoma kumi, waliokuwa wakienda na kutakaswa kwa pamoja, lakini kwa bahati mbaya, ni Msamaria tu, ndiye aliyethubutu kurejea tena kumpa Mungu utukufu. Jambo hili lilimhuzunisha sana Yesu, kiasi cha kuuliza wale kenda wa wepi? Ni wajibu wa waamini wanapoadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, yaani “Shukrani” kujizatiti kuwasaidia wengine walioelemewa na uzito wa safari, kiasi hata cha kushindwa kusonga tena mbele kwa ari na moyo mkuu; wawe ni walinzi wa ndugu na jamaa zao; kwa kuwaombea; kwa kuwasikiliza na kujibu kilio chao cha ndani kwa imani na upendo thabiti na kwa njia hii, imani itakuwa na kuchanua kama maua ya kondeni.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ni wale tu wenye imani thabiti, wanaofahamu umuhimu wa kushukuru hao ndio wanao okolewa kwa imani na hatimaye, kupata uzima wa milele kwa kukutana na Kristo Yesu, chemchemi na utimilifu wa maisha. Kwa mwamini anayekutana na Kristo Yesu anakuwa ni kielelezo makini cha moyo wa shukrani, kama njia ya kumkumbatia na kumwambata Kristo Yesu katika maisha, si tu kwa sababu amemwokoa mja wake kutoka katika “kasheshe za maisha”. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa na moyo wa shukrani kama yule Msamaria mwema, aliyemtukuza Mungu kwa sauti kuu na kumwangukia Yesu miguuni pake. Waamini wawe na ujasiri wa kudumu katika imani kwa kukuza moyo wa shukrani kwani hili ni tendo la imani linaloendelea kupyaisha maisha ya mwamini.

Baba Mtakatifu anawataka wanandoa na familia zao kuwa ni mashuhuda wa shukrani. Baada ya kumwomba Mwenyezi Mungu, kutembea katika umoja na mshikamano, familia ya Mungu, Jumapili ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa limekutanika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ili kumshukuru Mungu kwa Wenyeheri watano kuandikwa rasmi kwenye Kitabu cha Watakatifu wa Kanisa. Hawa ni wale ambao wametembea katika imani na kwa sasa wanakuwa waombezi wa watu wa Mungu. Kati yao kuna watawa watatu wanaoonesha kwamba, maisha ya kitawa ni hija ya upendo kuekelea katika vipaumbele vya maisha ya watu, vinavyosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mtakatifu Margarita Bays anaonesha umuhimu wa sala inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku; uvumilivu na sadaka ambayo imemwezesha Mwenyezi Mungu kumkirimia kuweza kuishi mng’ao wa Fumbo la Pasaka.

Kardinali John Henry Newman ni shuhuda wa utakatifu unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku, kwa kujikita katika amani na utulivu wa ndani; kwa kuwashirikisha wengine ile furaha inayofumbatwa katika utu wema, upendo, kiasi na fadhila pasi na kujitafutia makuu. Baba Mtakatifu amehitimisha mahubiri yake, kwa kuwataka waamini wawe ni mwanga wa uungwana katika giza la maisha ya walimwengu. Wamwombe Kristo Yesu aendelee kukaa pamoja nao, ili waweze kung’aa kama Yesu mwenyewe na kuwa mwanga kwa wengine!

Papa: Watakatifu
13 October 2019, 15:53