Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Vipaumbele vya Mababa wa Sinodi: Wongofu: Kieokolojia, Kimisionari, Kitamaduni, na katika shughuli za Kichungaji Ukanda wa Amazonia Papa Francisko: Vipaumbele vya Mababa wa Sinodi: Wongofu: Kieokolojia, Kimisionari, Kitamaduni, na katika shughuli za Kichungaji Ukanda wa Amazonia  (@Cimi)

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Vipaumbele vya Sinodi

Mambo msingi ni : Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, wongofu wa kitamaduni unaojikita katika mchakato wa utamadunisho; wongofu wa kiekolojia; wongofu wa kijamii kwa kuheshimu utu na utambulisho wa watu mahalia. Wongofu wa kichungaji, uwawezeshe wananchi wa Ukanda wa Amazonia kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa kama wakleri na watawa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Utamaduni wa kukutana, kujadiliana, kusikilizana na hatimaye kutoa mang’amuzi ya pamoja ni kati ya vipaumbe vya kwanza wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia mintarafu mwanga wa Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” na Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote”. Mambo makuu yaliyochambuliwa ni: ekolojia ya mazingira na utamaduni; ekolojia ya kisiasa na kiuchumi; elimu makini pamoja na tasaufi ya kiekolojia. Tema zote hizi zimesaidia kutengeneza “Instrumentum Laboris” yaani “Hati ya Kutendea Kazi” wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia iliyofunguliwa na Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 6 Oktoba 2019 kwa Ibada ya Misa Takatifu yamefungwa rasmi tarehe 27 Oktoba 2019. Maadhimisho yote haya yamewawezesha Mababa wa Sinodi kutoa Hati ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kwa Mwaka 2019.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, Jioni tarehe 26 Oktoba 2019 alitoa hotuba ya kufunga maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Katika hotuba hiyo, amekazia dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, wongofu wa kitamaduni unaojikita katika mchakato wa utamadunisho; wongofu wa kiekolojia unaofumbatwa katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; wongofu wa kijamii kwa kuheshimu utu na utambulisho wa watu mahalia. Wongofu wa kichungaji, uwawezeshe wananchi wa Ukanda wa Amazonia kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kama wakleri na watawa! Kanisa linapaswa kuendeleza utume wake miongoni mwa vijana wa kizazi kipya pamoja na kuendelea kuwahamasisha mapadre na wamisionari kujisadaka kama zawadi ya Roho imani kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu Ukanda wa Amazonia. Baba Mtakatifu amekazia pia dhamana na utume wa wanawake katika Kanisa Ukanda wa Amazonia.

Tema nyingine ni Madhehebu ya Watu wa Amazonia, mchango wa vyombo vya mawasiliano ya jamii pamoja na umuhimu wa kuzingatia mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa! Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa pengine ndiyo tema ambayo Baba Mtakatifu Francisko angependa Kanisa liweze kuitafakari kwa kina kwa siku za usoni. Tangu wakati huu, Baba Mtakatifu anasema, anaanza kuchakarika ili kuhakikisha kwamba, “Waraka wa Kitume Baada ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia” unachapishwa katika kipindi cha mwaka ujao, yaani 2020. Kanisa litaendelea kutafakari kuhusu Ushemasi wa Wanawake kama ulivyokuwa kwenye Kanisa la Mwanzo. Maadhimisho ya Sinodi ni mchakato unaofumbatwa katika utamaduni wa kutembea bega kwa bega kama Kanisa; kwa kusikilizana, kujadiliana na hatimaye, kuamua na kutenda katika umoja na mshikamano; kwa kuzingatia Mapokeo ya Kanisa sanjari na kuendelea kusoma alama za nyakati.

Baba Mtakatifu anasema, Kanisa Ukanda wa Amazonia linawajibika kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili; kwa kusimama kidete katika wongofu wa kitamaduni unaothamini tamaduni, mila na desturi njema za watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia. Mama Kanisa hana budi kushikamana na kuungana na watu wa Ukanda wa Amazonia, kwa kulinda: utu, heshima na haki zao msingi. Utamadunisho ni sehemu ya mchakato wa umwilisho wa tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha ya watu. Baba Mtakatifu ameridhishwa na tafakari kutoka kwa Mababa wa Sinodi kwamba, Mapokeo ya Kanisa yanafumbatwa katika utamadunisho! Wongofu wa Kiekolojia: Baba Mtakatifu anasema, umefika wakati wa kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha maskini wanaotishiwa na uchafuzi na uharibifu wa mazingira. Matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum.

Ukanda wa Amazonia ni ufunuo wa Uso wa Kristo ambaye ni maskini, mwenye njaa na mgeni asiyekuwa na makazi maalum. Baba Mtakatifu amemsifu Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol kwa mchango wake katika kuibua dhima ya Kikristo katika ekolojia fungamani. Utunzaji bora wa mazingira hauna budi kwenda sanjari na Injili ya uhai kama njia muafaka ya kulinda, kudumisha na kuendeleza haki ya mtu kuishi dhidi ya utamaduni wa kifo. Utunzaji bora wa mazingira ni chanda na pete na ulinzi wa uhai wa binadamu kwani haya ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana. Matumizi mabaya ya utajiri na mali asili ni hatari sana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vijana wa kizazi kipya wanayo haki ya kudai mchakato wa utunzaji bora wa mazingira kwa ajili ya kizazi kijacho! Uchafuzi na uharibifu wa mazingira ni changamoto kubwa si tu Ukanda wa Amazonia, bali hata sehemu mbali mbali za dunia kama ilivyo kwenye Bonde la Mto Congo, Argentina nk,.

Katika muktadha wa wongofu wa kitamaduni na kijamii, Baba Mtakatifu anasema,  Kanisa Ukanda wa Amazonia linawajibika kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili; kwa kusimama kidete katika wongofu wa kitamaduni na kijamii. Mama Kanisa anatambua kwamba, utamadunisho ni sehemu ya mchakato wa umwilisho wa tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha ya watu. Utumwa mamboleo, rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma; biashara ya binadamu na viungo vyake ni mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya watu, kiasi hata cha kubomolea mbali: tamaduni, mila na desturi njema za watu! Baba Mtakatifu anasema, wongofu wa shughuli za Kichungaji ni muhimu sana Ukanda wa Amazonia kwa kujikita katika njia ya umisionari ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Ni mchakato unaopania kuimarisha utume wa wakleri, watawa na waamini walei kama njia ya kuadhimisha mafumbo ya Kanisa na kuyatakatifuza malimwengu.

Njia mpya za utume wa Kanisa zinahitaji kipaji cha ubunifu na kuendelea kusoma alama za nyakati. Wazawa wapewe nafasi ya kupata malezi na majiundo ya Kikasisi, kwani kwa kushindwa kufanya hivyo ni kuwakosea haki wazalendo. Baba Mtakatifu anasema, Kanisa litaendelea kufanya tafakari ya kina kuhusu Ushemasi wa wanawake, kwa kuwachagua wajumbe wapya. Wanawake wanao mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Wanapaswa kuwezeshwa ili watekeleze vyema utume wao. Kanisa linapaswa kuendelea kujipyaisha kwa kukazia malezi na majiundo ya awali na endelevu kwa ajili ya wakleri, watawa na waamini walei. Kuna haja ya kuwafunda vijana watakaoweza kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili hata katika maeneo magumu na tete. Changamoto hii pia inapaswa kufanywa na wale wanadiplomasia wa Kanisa, ili kuweza kujifunza mahangaiko ya watu kwenye nchi za kimisionari. Mapadre wa “Fidei Donum” “Zawadi ya imani” wanapaswa kukuza na kudumisha ari na moyo wa kimisionari.

Papa Francisko anawapongeza Mapadre wa “Fidei Donum” kutoka Afrika, Asia na Amerika ya Kusini wanaojisadaka kwa ajili ya huduma Barani Ulaya na Amerika na wanapohitimisha mikataba yao wanarejea tena majimboni mwao kuendeleza huduma. Mababa wa Sinodi wanashauri iwepo Ibada kwa ajili ya watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kamba, takwimu zinaonesha kwamba, kuna Makanisa 23 yenye Ibada zao maalum, kumbe hakuna sababu ya kuwa na wasi wasi wa Kanisa kuratibu Ibada hizi zitakazosaidia kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Mama na Mwalimu wa wote. Kuna uwezekano wa kuanzisha kitengo cha Ukanda wa Amazonia kwenye Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu. Baba Mtakatifu amewashukuru Mababa wa Sinodi na wajumbe wote walioshiriki katika kufanikisha maadhimisho haya ambayo yamejikita katika wongofu wa: kiekolojia, kitamaduni, kijamii na kichungaji.

Huu ni mwaliko kwa waamini kuangalia mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kukazia umoja na mshikamano wa dhati, ili kutoa majibu muafaka ya changamoto, matatizo na fursa zilizopo kati ya watu. Upendo kwa Mungu na jirani ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa.

Papa: Sinodi Amazonia

 

28 October 2019, 12:37