Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anawataka Makardinali wawe ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili kwa kuonesha huruma kwa maskini pamoja na kusoma alama za nyakati. Baba Mtakatifu Francisko anawataka Makardinali wawe ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili kwa kuonesha huruma kwa maskini pamoja na kusoma alama za nyakati.  (Vatican Media)

Makardinali wawe ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili

Kuna jumla ya Makardinali 225, kati yao wenye uwezo wa kupiga na kupigiwa kura ni 128 na Makardinali 97 wamepoteza haki ya kupiga na kupigiwa kura. Baba Mtakatifu Francisko amekwisha wateuwa na kuwasimika Makardinali 88, kati yao ambao bado wako hai ni 84 na Makardinali 67 wana haki ya kupiga na kupigiwa kura wakati wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 5 Oktoba 2019 amewasimika Makardinali wapya 13 walioteuliwa hivi karibuni, ili kutangaza na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu kwa watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amewasihi Makardinali wapya kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini, ili kuondokana na utandawazi usioguswa na mahangaiko ya wengine, kiasi hata cha kunawa mikono kama ilivyokuwa kwa Pontio Pilato wakati akitoa hukumu dhidi ya Kristo Yesu. Amewataka Makardinali wapya kusoma alama za nyakati kwa kutambua hali halisi katika maisha na utume wa Kanisa, ili kuweza kuitangaza na kuitolea ushuhuda! Uongozi ni huduma kwa ajili ya watu wa Mungu na Kanisa katika ujumla wake. Hii ni changamoto kwa Mama Kanisa kutoka kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa XVI katika salam zake kwa Makardinali wapya amewataka kuwa waaminifu na watiifu kwa viapo vyao, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa Kanisa la Kristo.

Hadi tarehe 6 Oktoba 2019, takwimu zinaonesha kwamba kuna jumla ya Makardinali 225, kati yao wenye uwezo wa kupiga na kupigiwa kura ni 128 na Makardinali 97 wamepoteza kisheria haki ya kupiga na kupigiwa kura. Katika kipindi cha uongozi wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko amekwisha wateuwa na kuwasimika Makardinali 88, kati yao ambao bado wako hai ni 84 na Makardinali 67 wana haki ya kupiga na kupigiwa kura wakati wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Bara la Afrika lina Makardinali 29 kati yao kuna Makardinali 18 ambao wana haki ya kupiga na kupigiwa kura, akiwemo pia Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu Mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Baba Mtakatifu amekwisha kuitisha Baraza la Kawaida la Makardinali mara sita, kuanzia mwaka 2014. Takwimu zinaonesha kwamba, Kardinali Albert Vanhoye, aliyezaliwa tarehe 24 Julai 1923 ndiye Kardinali mwenye umri mkubwa zaidi kuliko Makardinali wote.

Kardinali Sigitas Tamkevičius SJ., Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu Kaunas nchini Lithuania. Kunako mwaka 1983 alikamatwa na kufungwa gerezani kwa muda wa miaka 10. Huko akatumikia kifungo na adhabu ya kazi ngumu, kama “njia ya kulishikisha adabu Kanisa”. Mwaka 1988 akapelekwa uhamishoni huko Siberia kwenye baridi kali hadi alipoachiliwa huru. Kardinali Sigitas Tamkevičius anasema, katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, wametembea katika Njia ya Msalaba, kwa mateso makali, nyanyaso na dhuluma dhidi ya Wakristo huko Lithuania. Katika kipindi hiki, Kanisa limeshuhudia karama ya wafiadini na waungama imani, ambao kweli wamekuwa mbegu ya Ukristo na chachu ya utakatifu wa maisha kwa watu wa Mungu katika shida na mahangaiko. Hii ni changamoto kwa waamini kuwa tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutetea, kuungama na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kwa mwamini ambaye hayuko tayari kushuhudia imani yake kiasi hata cha kuyamimina maisha yake, huyo ni dhaifu sana!

Kardinali Eugenio Dal Corso, P.S.D.P., Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Benguela, nchini Angola. Alizaliwa huko “Lugo di Valpantena di Grezzana, nchini Italia kunako tarehe 16 Mei 1939. Ni kiongozi ambaye alisadaka maisha na ujana wake wote ili kushiriki katika utume wa kimisionari tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Amewahi kufanya utume wake nchini Argentina kwa muda wa miaka 11, lakini, kilele cha utume huu ni pale alipojisadaka na kutembea bega kwa bega na maskini na wale waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya watu wa Mungu nchini Angola. Amewatumikia watu wa Mungu nchini Angola kwa muda wa miaka 33. Kardinali Eugenio Dal Corso anasema, Bara la Afrika linaendelea kutoa matumaini makubwa kwa utume na maisha ya Kanisa. Anamshukuru Mwenyezi Mungu aliwemwezesha kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayomwilishwa katika huduma makini ya upendo unaokuza na kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari kwa watu wa Mungu.

Kardinali Eugenio Dal Corso anasema, Angola ni nchi ambayo imebahatika kuwa na utajiri na rasilimali nyingi ambazo kama zingeweza kutumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, leo hii, Angola ingekuwa imepiga hatua kubwa katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Kwa bahati mbaya, ubinafsi, rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma, ni kati ya mambo yanayoendelea kupekenya maisha ya watu wa Mungu nchini Angola. Anamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua na kuenzi karama ya umisionari na sasa yuko tayari kurejea nchini Angola kuendeleza wito na dhamana yake kama Kardinali mmisionari kwa kuwaendelea maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Lengo ni kutangaza, lakini zaidi kushuhudia imani na furaha ya Injili inayomwilishwa katika matendo.

Kanisa Katoliki nchini Angola linaendelea kujizatiti katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika hija yake ya kichungaji nchini Angola, aliwataka Maaskofu Katoliki Angola: Kuwapenda, kuwathamini na kuwahudumia maskini na wagonjwa, lakini huduma ya upendo wa kweli ni kuwatangaza Habari Njema ya Wokovu! Kardinali Eugenio Dal Corso anapenda kuungana na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwezi Oktoba 2019 kipindi maalum sana kwa maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Anasema, amesimikwa katika kipindi hiki maalum cha kusali na kutafakari utume na maisha ya Kanisa, kama msingi wa mchakato mzima wa uinjilishaji mpya unaotekelezwa na Mama Kanisa.

Kwa hakika hiki ni kipindi cha ushuhuda wa  huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Mwezi Oktoba 2019 Kanisa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume"Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari.” Ni muda wa: sala, katakesi, tafakari na matendo ya huruma! Kardinali Eugenio Dal Corso anasema kwake hiki ni kipindi cha kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hata baada ya zaidi ya miaka 2000 ya Ukristo, bado kuna asilimia 70 ya watu ambao bado hawajamfahamu Kristo Yesu. Huu ni wakati wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Kardinali Eugenio Dal Corso anasisitiza kwamba, licha ya matatizo na changamoto kubwa zinazoendelea kuwakabili watu wa Mungu Barani Afrika, lakini, Bara la Afrika kwa siku za usoni, litakuwa na mchango mkubwa katika medani mbali mbali za maisha ya: kiroho, kiuchumi na kitamaduni.

Kumbe, huu ni wakati wa kuwekeza katika rasilimali watu sanjari na ujenzi wa miundo mbinu itakayoliwezesha Bara la Afrika kuwa ni dira na mwongozo si tu katika masuala ya kiuchumi, lakini zaidi katika kuzingatia kanuni, maadili na utu wema. Utajiri wa madini na maliasili iliyoko Barani Afrika, idhibitiwe kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rushwa, wizi na ubadhirifu wa mali ya umma ni vikwazo vikuu vya maendeleo fungamani ya binadamu. Kardinali Eugenio Dal Corso anakaza kusema, Afrika kumenoga! Si bure Bara la Afrika kupigwa madongo!

Papa: Makardinali

 

07 October 2019, 08:40