Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Barua Binafsi: Aperuit Illis: Domenika ya Neno la Mungu" Kuadhimishwa kila mwaka, Jumapili III ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa. Papa Francisko: Barua Binafsi: Aperuit Illis: Domenika ya Neno la Mungu" Kuadhimishwa kila mwaka, Jumapili III ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa.  (AFP or licensors)

Papa: Domenika ya Neno la Mungu: Jumapili III ya Mwaka

Papa kwa njia ya barua binafsi “Motu Proprio” “Aperuit Illis” ameanzisha “Domenika ya Neno la Mungu” itakayokuwa inaadhimishwa kila mwaka, Jumapili ya III ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jumapili hiyo itakuwa ni fursa kwa watu wa Mungu kujenga utamaduni wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Jerome kwa agizo la Papa Damasi wa kwanza, kwa muda wa miaka 23 alifanya kazi ya kutafsiri na kupanga vitabu vya Biblia kwa lugha ya Kilatini, maarufu kama “Vulgata” iliyopitishwa na Mababa wa Mtaguso wa Trento (1545-1563) kwamba inafaa kufundishia imani. Alifariki dunia tarehe 30 Septemba 420 akiwa ameliachia Kanisa utajiri mkubwa wa Maandiko Matakatifu. Mama Kanisa ameanza kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 1600 tangu Mtakatifu Jerome alipofariki dunia. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya barua binafsi “Motu Proprio” “Aperuit Illis” ameanzisha “Domenika ya Neno la Mungu” itakayokuwa inaadhimishwa kuanzia sasa kila mwaka, Jumapili ya III ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Jumapili hiyo itakuwa ni fursa kwa watu wa Mungu kujenga utamaduni wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao.

Ni nafasi adhimu kwa Kanisa kutangaza, kushuhudia na kusambaza Neno la Mungu. Huu ni muda muafaka wa kuombea umoja wa Wakristo pamoja na kudumisha majadiliano ya kiekumene na kidini pamoja na Wayahudi. Waamini wanashauriwa kulisoma Neno la Mungu, Kulisikiliza na hatimaye, kujitahidi kulimwilisha katika uhalisia wa maisha yao. Katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Neno la Mungu lipewe kipaumbele cha kwanza, kwa kuandaa mahubiri kuhusiana na Maandiko Matakatifu pamoja na kutoa huduma kwa Wasomaji wa Neno la Mungu. Hapa, Wasomaji wa Neno la Mungu wanapaswa kuandaliwa vyema, ili waweze kulitangaza kwa ukamilifu, kama ilivyo kwa wahudumu wa Ekaristi Takatifu kwa wagonjwa na wazee parokiani. Hii ni siku ambayo wasomaji watakabidhiwa Biblia Takatifu, ili waendeleze tafakari hii katika uhalisia wa maisha yao, daima wakijitahidi kusali na kulitafakari Neno la Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, “Domenika ya Neno la Mungu” inapata chimbuko lake kutoka katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, chimbuko la toba na wongofu wa ndani unaowakirimia waamini upendo, huruma na msamaha wa dhambi zao. Kwa njia ya Roho Mtakatifu, Mitume walipewa uwezo wa kutangaza na kushuhudia Fumbo la Wokovu. Utambulisho wa Wakristo unafumbatwa kwa namna ya pekee, katika mahusiano ya dhati kati ya: Kristo Mfufuka, Maandiko Matakatifu na Jumuiya ya waamini. Ndiyo maana Mtakatifu Jerome anasema “Kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomfahamu Kristo”. Baba Mtakatifu anasema, wazo la kuanzisha “Domenika ya Neno la Mungu” lilimwijia mara baada ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, ili kuendeleza majadiliano kati ya Mwenyezi Mungu na waja wake; mwaliko wa kuendelea kulipyaisha Kanisa kwa amana na utajiri unaobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu.

Barua hii ni jibu ya kilio cha watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waliotaka kujenga na kudumisha umoja unaobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu. Ni mwaliko wa kulisoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha na kulishuhudia katika uhalisia wa maisha yao. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika hati yao “Dei Verbum” yaani “Neno la Mungu wanagusia kuhusu “Ufunuo; Urithishaji wa ufunuo wa Kimungu; Uvuvio wa Kimungu na ufafanuzi wa Maandiko Matakatifu; Agano la Kale pamoja na Agano Jipya wanatilia mkazo umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa. Umoja wa Wakristo upate chimbuko lake kwa kusikiliza Neno la Mungu, linalofafanuliwa na wachungaji, kiasi kwamba, hata Mahubiri yanachukuliwa kuwa kama “Kisakramenti” muda muafaka wa kufafanua uzuri wa Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya waamini. Makatekisita, wafundwe kikamilifu, ili wawasaidie waamini kukua katika imani kama ilivyokuwa kwa wale wafuasi wa Emmau, waliobahatika kufafanuliwa Maandiko Mtakatifu na Kristo Yesu alipokuwa anatembea pamoja nao njiani.

Maandiko Mtakatifu yanazungumzia kuhusu Fumbo la Pasaka, Imani ya Wakristo inayopata chimbuko lake kwa kusikiliza Neno la Mungu katika maadhimisho ya Liturujia, Sala na Tafakari binafsi. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema: “Kanisa limeheshimu daima Maandiko Matakatifu kama lilivyoheshimu Mwili wa Bwana, wala halikukosa kamwe, hasa katika Liturujia takatifu, kujilisha mkate wa uzima na kuwapa waamini kutoka katika meza moja ya Neno la Mungu na pia ya Mwili wa Kristo. Kanisa limeyaamini daima na linaendelea kuyaamini Maandiko Matakatifu, pamoja na Mapokeo Matakatifu, kuwa ndiyo kanuni kuu kuliko zote ya maisha yake ya imani”. Kuna uhusiano wa pekee kati ya Neno la Mungu na Maadhimisho ya Ekaristi Takatifu; Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa; Neno la Mungu linafaa kwa ajili ya malezi na makuzi ya maisha ya waamini: kiroho na kimwili kwa sababu mhusika mkuu ni Roho Mtakatifu.

Neno la Mungu linatenda kazi ndani ya yule anayelisikiliza kwa makini, kiasi cha kumwajibisha kuwashirikisha wale wote anaokutana nao, ili kujenga na kudumisha umoja na mafungamano ya watoto wa Mungu. Neno la Mungu ni chemchemi ya upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma kwa akina Lazaro wanaoendelea kuteseka sehemu mbali mbali za dunia hata katika ulimwengu mamboleo, changamoto na mwaliko wa “kufyekelea mbali ubinafsi na uchoyo”, ili kujenga na kudumisha umoja, ushirikiano na mshikamano. Baba Mtakatifu Francisko anasema, tukio la Yesu kugeuka sura mbele ya wafuasi wake, akaonekana akizungumza na Musa na Elia, ni ushuhuda wa utimilifu wa Sheria na Unabii. Maandalizi makini ya kupambana uso kwa uso na Kashfa ya Msalaba yaani: Mateso, Kifo na hatimaye, Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Katika mchakato mzima wa kusoma, kusikiliza, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya waamini, Bikira Maria anabaki kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika kumwilisha Heri za Mlimani; muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu katika maisha yake.

Huu ni mwaliko wa kusikiliza Neno la Mungu na kulihifadhi katika sakafu ya nyoyo za waamini. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha Barua hii binafsi“Motu Proprio” “Aperuit Illis” inayoanzisha “Domenika ya Neno la Mungu” itakayokuwa inaadhimishwa kuanzia sasa kila mwaka, Jumapili ya III ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa kwa kusema kwamba, Neno la Mungu li karibu sana “Lakini neno li karibu nawe sana, li katika kinywa chako na moyo wako, upate kulifanya.” (Kumb. 30:14).

Papa Domenika Neno la Mungu
02 October 2019, 14:24