Tafuta

Vatican News
Padre Michael Czerny ni kati ya Makardinali wateule ambaye, tarehe 4 Oktoba 2019 anawekwa wakfu kuwa Askofu mkuu na tarehe 5 Oktoba 2019 anasimikwa kuwa Kardinali. Padre Michael Czerny ni kati ya Makardinali wateule ambaye, tarehe 4 Oktoba 2019 anawekwa wakfu kuwa Askofu mkuu na tarehe 5 Oktoba 2019 anasimikwa kuwa Kardinali.  (Vatican Media)

Padre Michael Czerny: Askofu mkuu na Kardinali kwa mpigo!

Kardinali mteule Michael Czerny, S.J., alizaliwa tarehe 18 Julai 1946 huko Brno, nchini Czechoslovakia ya zamani. Mwaka 1963 akajiunga na Wayesuit na kupewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 9 Juni 1973. Baada ya kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwatetea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, tarehe 4 Oktoba anawekwa wakfu kuwa Askofu mkuu na Kardinali, 5 Oktoba 2019.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 4 Oktoba 2019, katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican anatarajiwa kuwaweka wakfu Maaskofu wakuu wateule 4 ambao ni: Monsinyo Antoine Camilleri, Mosinyo Paolo Rudelli, Monsinyo Paolo Borgia, pamoja na Kardinali mteule Michael Czerny, S.J., Katibu mkuu msaidizi, Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza ya Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu. Kardinali mteule Michael Czerny, S.J., alizaliwa tarehe 18 Julai 1946 huko Brno, nchini Czechoslovakia ya zamani. Mwaka 1963 akajiunga na Shirika la Wayesuit na kupewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe 9 Juni 1973. Kwa miaka mingi katika maisha na utume wake, amekuwa mstari wa mbele katika masuala ya haki jamii. Amewahi kuwa pia Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha “Central America University, UCA”.

Kati ya mwaka 1992 hadi mwaka 2002 aliteuliwa kuwa Katibu wa masuala ya haki jamii kwenye Makao makuu ya Shirika la Wayesuit. Ni muasisi wa mtandao wa Wayesuit dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi Barani Afrika, “Jesuit AIDS Network”. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akatambua mchango wake katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika na kunako mwaka 2009 akamteuwa kuwa Mtaalam msikilizaji wakati wa Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Bara la Afrika. Kuanzia mwaka 2010 akateuliwa kuwa ni mshauri wa Baraza la Kipapa la Haki na Amani. Tarehe 14 Desemba 2016 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Katibu mkuu msaidizi, Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza ya Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu na kunako mwaka 2018 akateuliwa kuwa ni mjumbe wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana iliyoadhimishwa mwezi Oktoba hapa mjini Vatican.

Padre Michael Czerny, kama anavyofahamika na wengi hivi karibuni, aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa mmoja wa Makatibu Maalum wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Anasema, Kanisa kama mfano wa Msamaria mwema, linataka kujikita zaidi katika mchakato wa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; Ukanda wa Amazonia, kwa kuanzisha majadiliano katika ukweli na uwazi na hatimaye, kufanya maamuzi magumu katika maisha na utume wa Kanisa.

Padre Czerny
04 October 2019, 14:25