Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema, Mwezi Oktoba ni Mwezi wa Rozari Takatifu: Waamini wajibidiishe kusali Rozari ili kupata neema, baraka; wawaombee viongozi wa serikali, amani, amani na upendo. Papa Francisko asema, Mwezi Oktoba ni Mwezi wa Rozari Takatifu: Waamini wajibidiishe kusali Rozari ili kupata neema, baraka; wawaombee viongozi wa serikali, amani, amani na upendo. 

Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019: Mwezi wa Rozari Takatifu

Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya kuombea amani ulimwenguni, busara na hekima kwa viongozi wa serikali; imani na mafungamano ya kifamilia kwa waamini wote. Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa iwawezeshe waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Rozari, Utume & Umisionari.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 yalifunguliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya Masifu ya Jioni, tarehe 1 Oktoba 2019 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Tarehe 7 Oktoba 2019 waamini wakasali na Rozari ya Kimisionari Kimataifa na kwamba kilele cha maadhimisho haya ni tarehe 20 Oktoba 2019, kwa Ibada ya Misa Takatifu inayotarajiwa kuongozwa na Baba Mtakatifu Francisko. Wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 9 Oktoba, amewakumbusha waamini kwamba, Jumatatu, tarehe 7 Oktoba 2019, Kanisa limeadhimisha Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu. Ni matamanio ya Bikira Maria kuona waamini wakijibidiisha kusali Rozari Takatifu kila siku, ili waweze kujichotea neema na baraka zinazobubujika kutoka katika Sala hii, ambayo kimsingi ni muhtasari wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Ni sala inayowaongoza waamini kwenye furaha na maisha ya uzima wa milele.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya kuombea amani ulimwenguni, busara na hekima kwa viongozi wa serikali; imani na mafungamano ya kifamilia kwa waamini wote. Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa iwawezeshe waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini kwamba, Mwezi Oktoba 2019, umetengwa maalum na Mama Kanisa kwa ajili ya kuhamasisha ari na mwamko wa kimisionari duniani, kwa mwaka huu 2019, Kanisa linapoadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume "Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari. Baba Mtakatifu anawaalika majandokasisi, kujibu na kuitikia wito wa Mungu katika maisha yao, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Ili kuweza kufikia lengo hili, wanapaswa kujizatiti katika masomo, sala sanjari na kukuza fadhila za Kimungu ndani mwao yaani; imani, matumaini na mapendo, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu

Papa Benedikto XV katika Waraka wake wa Kitume"Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari” alifungua rasmi ukurasa mpya wa maisha na utume wa Kanisa mintarafu shughuli za kimisionari, kwa kulitaka Kanisa kuanzisha mchakato wa majiundo na malezi kwa ajili ya kuyategemeza Makanisa mahalia kwa rasilimali watu, yaani mihimili ya uinjilishaji! Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa. Kanisa la Kristo katika utume”. Kanisa linaendeleza wito na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, agizo kutoka kwa Kristo mwenyewe kwa wafuasi wake. Hiki ni kipindi maalum sana kwa maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni muda wa kutangaza furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa; Kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa ari na ushiriki mkamilifu na hatimaye, Kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Papa: Mwezi Oktoba
09 October 2019, 14:09