Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu amesikitishwa sana na kifo cha Kardinali Serafim Fernandes de Araujo, kilichotokea tarehe 8 Oktoba 2019, huko Brazil, akiwa na umri wa miaka 95! Baba wa maskini na yatima! Baba Mtakatifu amesikitishwa sana na kifo cha Kardinali Serafim Fernandes de Araujo, kilichotokea tarehe 8 Oktoba 2019, huko Brazil, akiwa na umri wa miaka 95! Baba wa maskini na yatima!  (AFP or licensors)

Kardinali Serafim F. Araujo, Baba wa maskini amefariki dunia!

Marehemu Kardinali Serafim F. Araujo alizaliwa mwaka 1924 huko Jimboni Aracuas. Akapewa Daraja Takatifu mwaka 1949. Akateuliwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo Kuu la Belo Horizonte na kuwekwa wakfu mwaka 1959. Kunako mwaka 1982 akateuliwa kuwa Askofu mkuu mwandamizi Jimbo kuu la Belo Horizonte na kusimikwa rasmi mwaka1986. Akateuliwa kuwa Kardinali mwaka 1998

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikito makubwa taarifa ya kifo cha Kardinali Serafim Fernandes de Araujo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu la Belo Horizonte nchini Brazil, aliyefariki dunia Jumanne, tarehe 8 Oktoba 2019 akiwa na umri wa miaka 95. Baba Mtakatifu katika salam zake za rambi rambi alizomtumia Askofu mkuu Walmor Oliviera Azevedo wa Jimbo Kuu la Belo Horizonte ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil anasema anapenda kuungana na familia ya Mungu Jimbo kuu la Belo Horizonte kwa ajili ya kusali na kumwombea Marehemu Kardinali Serafim Fernandes de Araujo kwa kumwaminisha chini ya huruma ya Mungu. Katika maisha na utume wake, Marehemu Kardinali Serafim Fernandes de Araujo alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Kanisa la Mungu. Yeye alikuwa ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na kwa muda wa miaka zaidi ya 50 akawaongoza, akawatakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu Jimbo kuu la Benezes.

Ni kiongozi aliyeonesha moyo wa upendo kwa Kristo na Kanisa lake; akajenga na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa wasafiri. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, sasa ataweza kumpokea na kumkaribisha mtumishi wake Kardinali Serafim Fernandes de Araujo kwenye makao na maisha ya uzima wa milele. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoa baraka zake za kitume kwa wale wote walioguswa na kutikiswa na msiba huu mzito, ili waweze kufarijika kwa sala na sadaka yake. Itakumbukwa kwamba, Marehemu Kardinali Serafim Fernandes de Araujo alizaliwa tarehe 13 Agosti 1924 huko Jimboni Aracuas. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 12 Machi 1949, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 19 Januari 1959 akateuliwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo Kuu la Belo Horizonte na kuwekwa wakfu kama Askofu tarehe 7 Mei 1959.

Tarehe 22 Novemba 1982 akateuliwa kuwa Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Belo Horizonte na hivyo kusimikwa rasmi tarehe 5 Februari 1986. Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 21 Februari 1998 akamteuwa kuwa Kardinali. Na hatimaye, tarehe 28 Januari 2004 akang’atuka kutoka madarakani. Hayati Kardinali Serafim Fernandes de Araujo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu la Belo Horizonte nchini Brazil katika maisha na utume wake, alijipambanua kwa kuwa mdau wa elimu na tasnia ya mawasiliano ya jamii, kwa kujisadaka kufanya maboresho makubwa ya kiteknolojia katika Radio na Gazeti la Jimbo. Alikuwa ni Jaalimu “wa kutupwa” alipokuwa akisimama darasani, wanafunzi wengi walifurahia jinsi ambavyo alibarikiwa na Mwenyezi Mungu katika mchakato wa kurithisha ujuzi na maarifa kwa vijana wa kizazi kipya. Umaarufu wake ulivuma ndani na nje ya Brazil, kiasi cha kualikwa sehemu mbali mbali za dunia, ili kushirikisha ujuzi na weledi wake katika kufundisha.

Kardinali Serafim Araujo aliguswa sana na mahangaiko ya wanafunzi waliokuwa wanatoka kwenye familia maskini, kiasi cha kuanzisha Mfuko wa Masomo kwa ajili ya maskini kwani alitambua kwamba, elimu ndio ufunguo wa maisha bora kwa kila mtu. Alitumia ujuzi wake katika kupanga na kutekeleza sera za uinjilishaji makini Jimboni mwake. Akapewa pia dhamana ya kuandaa maadhimisho ya Kongamano la V la Amerika ya Kusini lililoadhimishwa kunako mwaka 1995. Hayati Kardinali Serafim Fernandes de Araujo anakumbukwa sana kwa kuhamasisha ari na mwamko wa kimisionari Jimboni mwake, kwa kuwataka watu wa Mungu kushiriki kikamilifu katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa njia ya ushiriki mkamilifu. Mkakati huu ukawa ni mfano bora wa kuigwa hata kwa Majimbo mengine nchini Brazil. Aliwataka waamini walei kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutambua kwamba, wao kimsingi walikuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa Mataifa na hivyo walipaswa kutumia karama na mapaji yao kwa ajili ya kuyatakatifuza malimwengu.

Alikazia umuhimu wa ushirikiano kati ya Wakleri na waamini walei; malezi, makuzi na majiundo makini ya wakleri na walei; akawahimiza watu wa Mungu kujenga na kuendeleza Ibada mbali mbali za Kanisa ili kujichotea neema, rehema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Aliwataka waamini walei kuhakikisha kwamba, wanatumia kikamilifu vyombo vya mawasiliano ya jamii kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu, msingi madhubuti wa Mafundisho Jamii ya Kanisa. Hayati Kardinali Serafim Fernandes de Araujo alikuwa ni mtoto wa kwanza kati ya watoto 16 kutoka katika familia yake. Kumbe, ni mtu aliyeguswa kwa karibu sana na umaskini wa jirani zake, kiasi cha kuanzisha Kituo cha Watoto waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi Jimboni mwake, ili kulinda utu, heshima na haki zao msingi pamoja na kuwapatia fursa ya masomo. Alikazia utume wa Kanisa miongoni mwa watoto wadogo, ili kuwarithisha amana na utajiri wa Kanisa hatua kwa hatua katika maisha yao.

Ni kiongozi aliyejisadaka kwa ajili ya Injili ya uhai na akawa chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu kwa wagonjwa waliokuwa kufani! Aliwataka watu wa Mungu Jimboni mwake, kuhakikisha kwamba, wanawaonesha huruma na upendo, wagonjwa wote waliokuwa wanakutana nao katika maisha, lakini zaidi, huruma na upendo huo wapewe wale waliokuwa kufani! Hayati Kardinali Serafim Fernandes de Araujo sasa anapumzika kwa amani. Ni matumaini ya Kanisa kwamba, wale wote walionja huruma na upendo wake wa kibaba sasa wamempokea, ili aweze naye kushiriki ile furaha na maisha ya uzima wa milele! Baba wa maskini na wanyonge, sasa apumzike kwa amani! Amina!

Papa: Rambi rambi
10 October 2019, 15:21