Tafuta

Vatican News
Kardinali  José de Jesús Pimiento Rodríguez, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la  Manizales (Colombia) amefariki dunia tarehe 3 Septemba 2019 akiwa na umri wa miaka 100. Kardinali José de Jesús Pimiento Rodríguez, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Manizales (Colombia) amefariki dunia tarehe 3 Septemba 2019 akiwa na umri wa miaka 100. 

Papa Francisko asikitishwa na kifo cha Kardinali Josè Pimiento

Kardinali José de Jesús Pimiento Rodríguez alizaliwa mwaka 1919, akapewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe 28 Agosti 1955. Mwakai 1955 akawekwa wakfu kuwa Askofu. Mwaka 1975 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manizales. Kunako mwaka 1996, Mtakatifu Yohane Paulo II akaridhia kung’atuka kwake kutoka madarakani. Tarehe 14 Februari 2015 akateuliwa kuwa Kardinali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa kwa taarifa za kifo cha Kardinali José de Jesús Pimiento Rodríguez, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Manizales, nchini Colombia, kilichotokea tarehe 3 Septemba 2019. Katika maisha na utume wake, anasema Baba Mtakatifu Kardinali José de Jesús Pimiento Rodríguez alisimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Alitetea sana umuhimu wa jamii kupata elimu makini kama silaha ya ukombozi na ufunguo kwa maisha bora zaidi. Baada ya safari yake hapa duniani, Baba Mtakatifu anamwombea ili aweze kupata maisha na uzima wa milele. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kutuma salam zake za rambi rambi kwa ndugu, jamaa, marafiki pamoja na watu wote wa Mungu walioguswa na kutikiswa na msiba huu mzito wa Kardinali José de Jesús Pimiento Rodríguez ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 100 tangu alipozaliwa.

Kimsingi Kardinali José de Jesús Pimiento Rodríguez alizaliwa tarehe 18 Februari 1919, akapewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe 28 Agosti 1955 akiwa na umri wa miaka 22 tu ya ujana wake. Tarehe 28 Agosti 1955 akawekwa wakfu kuwa Askofu akiwa na umri wa miaka 36. Tarehe 22 Mei 1975 akateuliwa na Mtakatifu Paulo VI kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manizales. Kunako mwaka 1996, Mtakatifu Yohane Paulo II akaridhia kung’atuka kwake kutoka madarakani. Akateuliwa kuwa Kardinali na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 14 Februari 2015. Katika umri wake, amevunja rekodi ya kuwa ni Kardinali mzee kuliko wote duniani. Ni kiongozi aliyejitahidi kuhakikisha kwamba, anamwilisha Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa. Amewashiriki mara nyingi katika maadhimisho ya Sinodi mbali mbali ndani ya Kanisa. Hawa ndio vigogo wa Kanisa wanaoendelea kupukutika na hatimaye, kulala katika usingizi wa amani, wakiwa na tumaini la ufufuko katika wafu!

05 September 2019, 18:54