Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko asema, upendo, huruma na msamaha ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu. Baba Mtakatifu Francisko asema, upendo, huruma na msamaha ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu. 

Papa Francisko asema: Huruma & upendo ni kiini cha Habari Njema!

Hakuna sababu ya kuchelewa kumwamini Mwenyezi Mungu hata katika changamoto ngumu za maisha kwani Mwenyezi Mungu ana uwezo wa kuyabadili maisha ya kila mtu. Upendo na msamaha wa kweli ndicho kiini cha Habari Njema ya Wokovu, lakini pia inaweza kukataliwa kama alivyofanya yule kijana mkubwa, aliyejidhania kuwa ana haki zaidi kuliko hata ya yule Baba mwenye huruma.

Na Padre Angelo Shikombe, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili15 Septemba 2019, amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusameheana na kusahau makosa ya wengine. Akichukua mfano wa Yesu Kristo aliyejifungamanisha na wadhambi na hatimaye kufikiriwa vibaya na makundi ya Mafarisayo, Baba Mtakatifu amesema, watu wanapaswa kuipokea Injili na kumuiga Kristo anayewapokea wadhambi na kula nao. Hilo ndilo liko mbele ya kila mtu kumpokea mwenzake kama Kristo naye anavyowapokea wanaomtafuta katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Akiwahamasisha kusoma Injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Luka sura 15, yenye mifano mitatu ya kushangaza, katika mfano wa kwanza  wa mchungaji kupotelewa na kondoo wake na kuwaacha tisini na kenda akaenda kumtafuta yule aliyepotea, Baba Mtakatifu anasistiza juu ya upendo wa Mungu hasa kwa wale ambao bado hawajampoea Yesu katika maisha yao. Hawa ni wale ambao hawajaweza kuishinda dhambi ambao kutokana na ugumu wa maisha hawaamini katika upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Katika mfano wa pili wa mwanamke kupotelewa na shilingi na kuitafuta mpaka aipate, Baba Mtakatifu amesema, hakuna anayeweza kuwa mbadala wa mwingine katika upendo wa Mungu.

Na katika mfano wa tatu wa Baba mwenye huruma anayemsubiri mwanaye arudi, Baba Mtakatifu amesema, Mungu huwasubiri watu wote bila kuchoka. Ni binadamu wenyewe wanaokumbatiwa kwani wao ndio shilingi iliyopotea na kondoo aliyepatikana na kuwekwa mabegani mwa Mchungaji mwema. Hakuna sababu ya kuchelewa kumwamini Mwenyezi Mungu hata katika changamoto ngumu za maisha kwani Mwenyezi Mungu ana uwezo wa kuyabadili maisha ya kila mtu. Upendo na msamaha wa kweli ndicho kiini cha Habari Njema ya Wokovu, lakini pia inaweza kukataliwa kama alivyofanya yule kijana mkubwa, aliyejidhania kuwa ana haki zaidi kuliko hata ya yule Baba mwenye huruma.

Kijana mkubwa alikuwa na shingo ngumu kiasi cha kushindwa kuonja huruma ya Baba yake. Akajifungia katika ubinafsi wake kwa kujidai kuwa ni mwenye haki na hata kuthubutu kumnyooshea kidole mdogo  wake. Anasahau kwamba wako pamoja na mmdogo wake, na kudhani kwamba yeye ndiye mwana pekee kwa Baba yake. Hata waamini wanaweza kutumbukia katika kishawishi cha kujihesabia haki na kusahau kwamba, hata wao ni wadhambi na wanahitaji huruma na upendo wa Mungu. Bila msaada wa neema ya Mungu si rahisi sana kwa mwamini kushinda dhambi na ubaya wa moyo! Waamini na watu wenye mapenzi mema wanaweza kuishinda dhambi kwa kukubali kupokea msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kuwa tayari kuwasamehe wale wanaowakosea.

Kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, waamini wanapokea huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kwani ni Mungu anayeshinda dhambi. Mungu akisamehe hakumbuki tena dhambi walizo mtendea. Hivyo Mungu ni mwema sana kwa watu wake, anafuta ubaya, anawaunda upya tena pamoja na kuwakirimia amani na utulivu wa ndani. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, dhambi haina neno la mwisho katika maisha ya mwamini. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko aliwaweka waamini na watu wote wenye mapenzi mema chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, anayefungua vifungo vya maisha; anayewasaidia kuondokana na kiburi cha kudhani kwamba, wao ni wenye haki zaidi na kuwasaidia kuwa na hamu ya kukimbilia huruma na upendo wa Mungu, ili uweze kuwakumbatia na kuwaambata katika maisha na kuwasamehe dhambi zao.

Papa: Angelus

 

 

15 September 2019, 13:09