Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amewataka Waagustino kuhakikisha kwamba, wanadumisha ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa na katika Ulimwenguni. Baba Mtakatifu Francisko amewataka Waagustino kuhakikisha kwamba, wanadumisha ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa na katika Ulimwenguni.  (Vatican Media)

Wosia wa Papa Francisko kwa Shirika la Waagustino: Ushuhuda!

Baba Mtakatifu Francisko amewaasa wanashirika la Mtakatifu Augustino kuendelea kuishi kadiri ya maongozi ya Mwenyezi Mungu, wadumishe maisha kijumuiya; tafakari zao za ndani wakiwa katika umoja wa kidugu. Amewaeleza kuwa umoja huo ndio unaweza kutoa ushuhuda wazi, imara na bila mabishano. Lakini watambue kuwa huo ni wajibu mkubwa unaopaswa kuutolea ushuhuda!

Na Padre Angelo Shikombe, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amewataka wanashirika la Mtakatifu Augustino wadumu katika umoja wa sala na maisha ya kidugu. Baba Mtakatifu ameyasema hayo, tarehe 13 Septemba 2019 katika hotuba yake kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirika ulijumuisha wanashirika 150 kutoka katika nchi mbali mbali wanakofanya utume wo. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amewaasa wanashirika la Mtakatifu Augustino kuendelea kuishi kadiri ya maongozi ya Mwenyezi Mungu kwa pamoja katika tafakari zao za ndani wakiwa katika umoja wa kidugu. Amewaeleza kuwa umoja huo ndio unaweza kutoa ushuhuda wazi, imara na bila malumbano. Lakini, watambue kuwa huo ni wajibu mkubwa unaopaswa kutekelezwa na kushuhudiwa katika uhalisia wa maisha. Aidha, Baba Mtakatifu amewaomba wasiizime karama ya mwanzilishi wao ya kudumu katika kumtafuta Mungu kwa moyo wa pekee usiogawanyika katika Kristo katika majitoleo pekee ya kustawisha ufalme wa Mungu.

Ikumbukwe kuwa Shirika la Mtakatifu Augustino lilianzishwa mnamo mwaka 1244 katika misingi ya kuishi na na kukuza roho ya maisha ya kijumuiya kama walivyokuwa wakiishi Jumuiya za wakristo wa kwanza. Jumuiya hii imeundwa na watu, wanaume na wanawake, ambao, wanafuata mafundisho ya sheria inayodai, waishi pamoja kwa amani, kwa roho moja na moyo mmoja wakiwa katika mahusiano ya karibu na Mwenyezi Mungu kwa sala na sadaka zao. Upendo huo ndiyo moyo wa Kanisa ambao uko hatarini kuzimwa kutokana na changamoto mamboleo. Wakati wa kipindi cha uongozi wa Mtakatifu Paulo VI mfumo mamboleo ndiyo ulianza kuingia na leo ndiyo maisha ya ulimwengu mamboleo. Hivyo Injili ya ukombozi inayofafanuliwa katika Shirika la Mtakatifu Augustino iendelee kukoleza katika ulimwengu mamboleo. Wanashirika la Mtakatifu Augustino wameitwa kushuhudia na kuupasha moto, kuuhuisha na kuufanya huo upendo uonekane wazi katika maisha ya watu.

Ushuhuda huo unaanza katika maisha ya Jumuiya zao, wakishirikishana kwa upendo vitu vilivyo vidogo na kupeana fursa za uinjilishaji na kumpatia Kristo mfufuka nafasi yake ya kuzitakasa roho zao. Upendo huo unapaswa kuwa wa unyenyekevu na kweli, na siyo upendo wa kuigiza. Jitihada za kumtafuta Mwenyezi Mungu zisije zikaghubikwa na matarajio mengine kwani huo ndio utume wao. Kama alivyoandika Mtakatifu Augustino “Upendo si mwisho na nyezo ya maisha ya kitawa, bali ni kiini cha maisha ya kitawa. tunaanza kwa upendo, tunadumu katika upendo na kuhitimisha utume wetu katika upendo. Mtakatifu Monica mama wa Mtakatifu Augustino alisali kwa bidii na kupewa na Mwenyezi Mungu zaidi ya kile alichotafuta, hivyo hii ni hamasa kwao ya kuendelea na utume wa Kanisa. Akitafsiri barua ya kwanza ya Mtakatifu Yohane Mtume, Baba Mtakaifu amesema, Kanisa linaitwa kama Mama wa upendo (Materi charitas) na kama mtu angependa kujua kama ana roho wa Bwana angejiuliza moyoni mwake kama hakimbilii Sakramenti bali ana uthubutu wa kuziishi.

Ni kuendelea kujiuliza kama upendo dhidi ya jirani yako umepoa, basi ni wakati wa kuupasha moto tena, lakini watu hawawezi kuwa na upendo pasipokuwa na Roho wa Mungu, maana Mungu Mwenyewe ni upendo. Upendo wa Mungu umemiminwa mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Hivyo Katiba yao inawadai kuwa na upendo huo na kuuishi kwa upole. Wanaopendana hufanyika kuwa ndugu. Upendo huo pia hufungamana na msamaha kama Kristo anavyotuita sisi sote kuwasameha hata wale wasioomabmsamaha (Lk 23 .34) hii ndiyo njia ya upendo. Baada ya kuwaasa yote hayp,  Baba Mtakatifu amewakumbusha tena kuwa changamoto yao kubwa wanayopaswa kukabiliana nayo ni uwajibikaji, kuishi maisha ya jumuiya wakishirikishana pamoja mang’amuzi ya kimungu  na kuyashuhudia kwa ulimwengu. Katika kashfa za Kanisa au pia za kifamilia, amani itawale katika njia za mapito yao kwa sababu kashfa zinakuja zenyewe na wengine hufikiri kuwa hakuna njia ya kupitia, lakini Kristo ndiye njia yenyewe.

Mwishoni kabisa Baba Mtakatifu amesema, Msalaba ndicho kipimo cha upendo, na ni dhahiri kuwa kunaweza kuwa na upendo pasipo msalaba kama hakuna msalaba, lakini penye msalaba nmna mtu anavyoupokea msalaba huo ndiyo upendo. Hayo ndiuyo maisha ya Bwana wetu kama alivyo na kama anavyotutafuat kila siku.  Na mwishoni Baba Mtakatifu aliwatakia baraka na maombezi ya Bikira Maria Mama wa Yesu na mwanga wa Kanisa,  awalinde na kuwasindikiza katika utume na maisha yao.

Papa: Augustino
15 September 2019, 10:22