Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaojisadaka kwa ajili ya Injili ya upendo kwa maskini sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaojisadaka kwa ajili ya Injili ya upendo kwa maskini sehemu mbali mbali za dunia. 

Papa Francisko: Injili ya huruma inamwilishwa kati ya maskini!

Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru wote hawa kwa ukarimu pamoja na kutumiza vyema karama na talanta walizokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha imani tendaji. Huu ni ukarimu wa Kiinjili unaowafikia moja kwa moja maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hii ni Injili ya upendo katika matendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dr. Matteo Bruni Msemaji mkuu wa Vatican katika taarifa yake kwa vyombo vya habari amebainisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa jioni tarehe 13 Septemba 2019 amekutana na kuzungumza na viongozi wa Kampuni ya Lamborghini kutoka Italia inayojihusisha na utengenezaji wa magari ya kifahari kwa ajili ya michezo. Kampuni hii ilianzishwa kunako mwaka 1963 na mfanya biashara maarufu Ferruccio Lamborghini. Mkutano huu, umewahusisha hata viongozi wa Mfuko wa OMAZE waliohusika na kupiga mnada gari iliyotolewa na Kampuni ya Lamborghini kama zawadi kwa Baba Mtakatifu kunako tarehe 15 Novemba 2017. Mnunuzi wa gari hii kutoka Jamhuri ya watu wa Czech alikuwepo pia kushuhudia fedha iliyopatikana inawasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Katika mkutano huu, Baba Mtakatifu amekabidhiwa hundi ya Euro 900, 000, Kiasi cha Euro 200, 000 kimetolewa kama mchango kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa Seminari na Kituo cha Chekechea nchini Haiti; ambayo bado inahitaji msaada mkubwa ili kuweza kuanza upya baada ya kuathirika vibaya na tetemeko la ardhi lililojitokeza kunako mwaka 2010. Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru wote hawa kwa ukarimu pamoja na kutimiza vyema karama na talanta walizokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha imani tendaji. Huu ni ukarimu wa Kiinjili unaowafikia moja kwa moja maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Itakumbukwa kwamba, jumla ya Euro 300, 000, zilitolewa kwa Jumuiya ya Papa Yohane XXIII wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu ilipoanzishwa na Don Oreste Benzi kunako mwaka 1968. Taarifa inaendelea kudadavua kwamba, kiasi Euro 200, 000, kilitolewa kwa ajili ya kuchangia Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji, kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa Uwanda wa Ninawi ambao una historia ndefu katika maisha ya Wakristo, kielelezo cha imani na mateso mbali mbali. Hata leo hii watu wanaoishi katika eneo hili wamejaribiwa; wakasalitiwa; nyumba zao za ibada zikaharibiwa na kunajisiwa! Yote haya yalijitokeza kunako mwaka 2014. Huo ukawa ni mwanzo wa kuibuka kwa wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Kiasi kingine cha fedha kimepelekwa kwenye Asasi ya “Amici Central Africa Onlus” pamoja na GICAM ambao wamepata Euro 160, 000.

Papa: Msaada
17 September 2019, 10:22