Tafuta

Vatican News
Papa: visita a sorpresa 'Cittadella Cielo' a Frosinone Papa: visita a sorpresa 'Cittadella Cielo' a Frosinone   (ANSA)

Papa Francisko: Miaka 25 ya Nuovi Orizzonti: Injili ya matumaini

Mwenyezi Mungu anajishusha na kuinama hadi chini kabisa, ili kuwainua wale wanaoelemewa na uzito na ugumu wa maisha. Ushuhuda wao ni mbegu ya imani, matumaini na mapendo, ambayo wamepandikiza katika maisha na utume wa Papa. Haya yamekuwa ni majadiliano ya kina, yaliyoboreshwa kwa muziki mwororo ulioporomoshwa na vijana wa wa Jumuiya ya “Nuovi Orizzonti”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 24 Septemba, 2019 amepata bahati ya kutembelea na kuzungumza na Jumuiya ya “Nuovi Orizzonti”, iliyoko Frosinone, nje kidogo ya mji wa Roma. Baba Mtakatifu amepata fursa ya kusikiliza hotuba ya kumkaribisha kutoka kwa Chiara Amirante, Muasisi wa Jumuiya hii, ambaye amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu kwa kuwatembelea, kuwafariji na hatimaye, kuadhimisha nao mafumbo ya Kanisa. Chiara Amirante amesimulia kwa ufupi historia na utume wa Jumuiya ya “Nuovi Orizzonti” katika ulimwengu mamboleo. Wamejitahidi katika kipindi cha miaka 25 iliyopita kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo na matumaini. Vijana wengi wamethubutu kutoka katika minyororo ya biashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Leo hii wameonja huruma na upendo wa Mungu unaoendelea kupyaisha maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko katika hali ya unyenyekvu mkuu, amesikiliza shuhuda za watu waliokuwa wamekufa na sasa wamefufuka; wasichana wanaotafuta kuonja tena huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Vijana hawa wamemuuliza maswali tete Baba Mtakatifu, lakini amekataa kuwajibu, kwani kwa kufanya hivyo angechafua utakatifu wa ushuhuda wa maisha yao. Ni ushuhuda ambao unamwilishwa katika uhalisia na safari ya maisha. Ni watu walionja huruma na upendo wa Kristo Yesu katika maisha yao, aliyewashika mkono na kuwaokoa kutoka katika shimo la uharibifu, dhambi na utupu! Wasichana hawa wameguswa na Uso wa huruma ya Mungu na katika uhuru wao kamili, wakaamua kupyaisha tena maisha yao. Huyu ndiye yule Mwenyezi Mungu anayejishusha na kuinama hadi chini kabisa, ili kuwainua wale wanaoelemewa na uzito na ugumu wa maisha. Ushuhuda wao ni mbegu ya imani, matumaini na mapendo, ambayo wamepandikiza katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Haya yamekuwa ni majadiliano ya kina, yaliyoboreshwa kwa muziki mwororo ulioporomoshwa na vijana wa Jumuiya ya “Nuovi Orizzonti”.

Baba Mtakatifu amewashukuru vijana walioshirikisha historia za maisha yao na kwamba, wayatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, tayari kuanza mchakato wa upyaisho wa maisha kadiri ya neema ya Mungu. Binadamu ni mavumbi yanayoonesha udhaifu na mapungufu yake, lakini wamekombolewa kwa huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba. Baba Mtakatifu anasema, amesikiliza kwa makini sauti zao katika hali ya ukimya, kama wao walivyo fanya na hatimaye, wakaweza kusikiliza sauti ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Hawa ni vijana waliopambana sana katika maisha, wakapigwa na kugalagazwa, kabla ya kukata tamaa, Kristo Yesu, akwashika mkono na kuwajalia mwanzo mpya wa maisha. Ushuhuda wao, uwe ni kikolezo cha kusonga mbele kwa imani na matumaini mapya. Huu ni mwaliko wa kuthamini, kuheshimu na kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, hakuna nafasi ya kuwadharau wengine.

Watu washikamane na kusaidiana katika maisha! Mwenyezi Mungu daima anajishusha, kama ilivyokuwa kwenye Fumbo la Umwilisho; anaamua kuambatana na wafuasi wake, kama alivyofanya kwa wale Wafuasi wa Emmau, akwafafanulia Maandiko Matakatifu na kumtambua wakati wa kuumega Mkate, tangu wakati ule wakageuka na kuwa watu wapya zaidi. Huu ni mwaliko wa kumwachia Mungu nafasi ili aweze kuwakomboa. Mwenyezi Mungu, daima yuko pembeni mwao kwa njia ya Kristo Yesu, anapenda kuambatana nao katika hija ya maisha yao, ili kuwasaidia katika mapambano ya maisha. Baba Mtakatifu amewakumbusha kwamba, Mwenyezi Mungu anaheshimu sana uhuru wao. Msalaba wa Yesu uwakumbushe: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Wajitahidi kuwa huru kutoka katika undani wa maisha yao, ili wasitumbukie tena katika ukale wa maisha! Vijana hawa wanapaswa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kupyaisha maisha yao, kwa kujiaminisha kwake.

Tabia ya dhambi ni kutaka kujirudia rudia, ili kujenga mazoea! Vijana hawa wajitahidi baada ya kusafisha nyumba ya maisha yao, wasimruhusu tena Shetani, Ibilisi kurudi na kuwachafulia maisha. Katika maisha yao waendelee kujifunza unyenyekevu wa Mtakatifu Petro aliyemkana Kristo Yesu mara tatu, lakini baadaye, akatubu na kumwongokea Kristo Yesu ambaye alimkabidhi dhamana na utume wa kuliongoza Kanisa. Upendo wa Mungu uwalinde na kuwaongoza katika hija ya maisha yao. Uhuru wao unapaswa kujikita katika upendo na huruma ya Mungu. Kila mwanadamu ataendelea kubaki kuwa ni fumbo ambalo limewakutanisha na Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anawakumbusha kuhusu upendo wa Mungu katika maisha yao ni neema inayokuwa na kuchanua kama mtende wa Lebanon. Maisha ni zawadi ya Mungu inayopaswa kulindwa na kuendelezwa ili izae matunda yanayokusudiwa, yaani wawe na ujasiri wa kutoka kifua mbele kwenda kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha yao.

Wawe ni watu wa “Magnificat” tayari kushirikiana na Bikira Maria, kumwimbia Mwenyezi Mungu matendo makuu aliyowatendea katika maisha. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru vijana wote hawa kwa ushuhuda wenye mvuto na mashiko na mbegu ya imani na matumaini, waliyopandikiza katika maisha yake!

Orizzonti: Shuhuda

 

 

25 September 2019, 15:54