Tafuta

Vatican News
Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko inaongozwa na kauli mbiu: Mpanzi wa amani na matumaini: Baba Mtakatifu anakazia utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko inaongozwa na kauli mbiu: Mpanzi wa amani na matumaini: Baba Mtakatifu anakazia utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!  (AFP or licensors)

Hija ya Papa Francisko nchini Madagascar: Mpanzi wa amani na matumaini! Utunzaji wa Mazingira!

Pamoja na uzuri wa mazingira asilia, lakini kuna uzuri wa pekee ambao umegota katika sakafu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro ambao ni uzuri wa utakatifu wa maisha yao. Ndiyo maana, Baba Mtakatifu anapenda kufanya hija hii ya kitume nchini Madagascar ili kuwaimarisha katika imani na wakati huo huo, hata yeye aweze kuchota imani hii kutoka kwao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia Jumatano tarehe 4-10 Septemba 2019 anafanya hija ya kitume nchini: Msumbiji, Madagascar pamoja na Mauritius. Hii ni fursa kwa Familia ya Mungu Barani Afrika kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu. Kauli mbiu inayoongoza hija ya Baba Mtakatifu nchini Msumbiji ni: matumaini, amani na upatanisho. Kwa upande wa Madagascar ni “Mpanzi wa amani na matumaini na kauli mbiu ya familia ya Mungu nchini Mauritius ni “Hujaji wa amani”. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa njia ya video aliowatumia wananchi wa Madagascar kama sehemu ya maandalizi ya hija yake ya kitume nchini mwao anasema, kwa neema na baraka za Mwenyezi Mungu, baada ya muda si mrefu atakuwa kati yao, lakini tangu wakati huu, anapenda kuwatumia salam na matashi mema; akiwashukuru kwa sadaka na majitoleo yote wanayoendelea kufanya kwa ajili ya kufanikisha hija yake ya kitume nchini Madagascar.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawashukuru kwa sala mbali mbali ambazo watu wa Mungu wanaendelea kusali sehemu mbali mbali za Madagascar. Anasema, haijalishi hata kama atabahatika kutembelea sehemu chache tu za Madagascar, lakini kwa njia ya sala na sadaka yake, ataweza kufanikiwa kuwafikia watu wengi zaidi na kuwapatia baraka zake Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anawakumbusha wananchi wa Madagascar kwamba, nchi yao ni maarufu sana kwa uzuri wa mazingira asilia, kiasi hata cha kuwahamasisha watu wengi kuimba utenzi wa sifa na shukrani kwa kusema, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako”. Ni wajibu wa binadamu kuhakikisha kwamba, analinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Pamoja na uzuri wa mazingira asilia, lakini kuna uzuri wa pekee ambao umegota katika sakafu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro ambao ni uzuri wa utakatifu wa maisha yao.

Ndiyo maana, Baba Mtakatifu anapenda kufanya hija hii ya kitume nchini Madagascar ili kuwaimarisha katika imani na wakati huo huo, hata yeye aweze kuchota imani hii kutoka kwao. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa njia ya video kwa watu wa Mungu nchini Madagascar kwa kuwaombea kwa Bikira Maria ili awawezeshe kuchota zawadi hiyo ya imani! Itakumbukwa kwamba, ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya video kwa watu wa Mungu nchini Msumbiji amekazia kwa namna ya pekee kabisa, mchakato wa upatanisho, udugu na amani Barani Afrika, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ni Baba wa wote. Amewakumbusha kuhusu hija ya kitume iliyofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1998. Hija yake nchini Msumbiji inapania kuwaimarisha ndugu zake katika imani, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya Kristo inayofumbatwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kwa upande wake Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika inakazia: Injili ya amani kama chachu na kikolezo cha maendeleo fungamani ya binadamu. Jambo la pili ni utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kadiri ya Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote”. Dhamana hii, imepewa uzito wa pekee na Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa watu wa Mungu nchini Madagscar. Jambo la tatu anasema Kardinali Pietro Parolin ni mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Kwa ufupi, hija ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika inapania kupyaisha tena misingi ya haki, amani na upatanisho Barani Afrika.

Papa: Ujumbe: Madagascar
02 September 2019, 14:31