Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru sana watu wa Mungu nchini Mauritius kwa wema na ukarimu wao kwake! Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru sana watu wa Mungu nchini Mauritius kwa wema na ukarimu wao kwake!  (Vatican Media)

Hija ya kitume ya Papa Francisko Mauritius: Salam kwa wafungwa

Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwasilimia wafungwa wanaofuata “Mfumo wa Alpha” unaowawezesha kupata majiundo makini kuhusu maana ya maisha pamoja na kusaidia kutambua umuhimu wa imani katika maisha ya kila siku. Hii ni huduma inayotolewa na wahudumu wa maisha ya kiroho kwa wafungwa gerezani nchini Mauritius. Amewashukuru wote kwa ukarimu wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 9 Septemba 2019 mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa heshima ya Mwenyeheri Jacques Dèsirè Laval kwenye Mnara wa Bikira Maria Malkia wa amani, ametoa shukrani zake za dhati kwa sadaka na majitoleo makubwa yaliyofanywa na familia ya Mungu nchini Mauritius. Ameonesha uwepo wake wa karibu kwa viongozi mbali mbali wa Serikali ambao amepata bahati ya kukutana na kuzungumza nao jioni tarehe 9 Septemba 2019. Baba Mtakatifu anawashukuru watu wa Mungu nchini Mauritius kwa mapokezi mazito na ukarimu wa hali ya juu. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii pia kuwashukuru wakleri, watawa pamoja na watu wa kujitolea kwa sadaka na majitoleo yao. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwasilimia wafungwa wanaofuata “Mfumo wa Alpha” unaowawezesha kupata majiundo makini kuhusu maana ya maisha pamoja na kusaidia kutambua umuhimu wa imani katika maisha ya kila siku.

Hii ni huduma inayotolewa na wahudumu wa maisha ya kiroho kwa wafungwa gerezani nchini Mauritius. Wafungwa hawa wamemwandikia barua Baba Mtakatifu Francisko. Ametumia fursa hii kuwapatia baraka zake za kitume. Baba Mtakatifu ametambua pia uwepo wa watu wa Mungu kutoka Visiwa vya Shelisheli, Rèunion, Comoro, Chagos, Agalega, Rodriguez bila kuwasahau wenyeji wa Mauritius. Baba Mtakatifu amewahakikishia uwepo wake wa karibu, sala na sadaka zake. Baba Mtakatifu amewaombea kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia yale mema wanayo tamani kutoka katika sakafu ya maisha yao! Kwa upande wake, Kardinali Maurice Piat, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Port Lous nchini Mauritius, amemshukuru Baba Mtakatifu kwa kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa ajili ya watu wa Mungu ndani na nje ya Mauritius, visiwa ambavyo viko pembezoni mwa vipaumbele vya wengi. Ujio wa Baba Mtakatifu Francisko umewasha moto wa majadiliano ya kidini na kiekumene.

Ujumbe wake wa kitume, umekuwa ni faraja sana kwa watu wa Mungu nchini Mauritius, katika utume wa Kanisa na uinjilishaji wa kina. Familia ya Mungu nchini Mauritius inamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu kwa kuwa kweli ni shuhuhuda na mjenzi wa amani katika mustakabali wa kimataifa. Visiwa vilivyo kwenye Bahari ya Hindi vinataka kujizatiti katika ujenzi wa amani ya kudumu inayokita mizizi yake katika haki jamii pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Familia ya Mungu nchini Mauritius inatambua na kuthamini mchango wa Baba Mtakatifu Francisko kama hujaji wa amani, chapa inayoacha kumbu kumbu ya kudumu katika akili na nyoyo za watu wengi. Kama sehemu ya kumbu kumbu ya ujio wa Baba Mtakatifu Francisko nchini Mauritius, waamini wamepanda miti 100, 000, kama kielelezo makini cha ushiriki wao katika ekolojia fungamani. Hiki ni kielelezo na mwaliko kwa waamini kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na Dunia Mama.

Mara baada ya maadhimisho ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu amepata chakula cha mchana na Baraza la Maaskofu Katoliki Bahari ya Hindi, “CEDOI” lililoanzishwa kunako mwaka 1985 na kwa sasa linaundwa na Maaskofu watano ambao ni wajumbe wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar. Amepata pia fursa ya kutembelea na kusali kwenye Madhabahu ya Père Laval, iliyozinduliwa kunako mwaka 2014 wakati wa Jubilei ya Miaka 150 tangu alipofariki dunia Mwenyeheri Jacques Dèsirè Laval, aliyejisadaka kwa ajili ya uinjilishaji wa kina nchini humo. Kila mwaka ifikapo tarehe 9 Septemba anakumbukwa na Kanisa mahalia. Baba Mtakatifu Francisko amepata pia nafasi ya kukutana na kusalimiana na wagonjwa pamoja na ndugu na jamaa zao.

Papa: Wafungwa
09 September 2019, 19:18