Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kuwekeza zaidi kwa utume miongoni mwa vijana. Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kuwekeza zaidi kwa utume miongoni mwa vijana.  (© Vatican Media)

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Mauritius: Ushuhuda & Uinjilishaji mpya!

Kutokana na utume wake Padre Laval, Kanisa limehuishwa na hivyo linahitaji kutumia fursa ya kimisionari ili kuepuka vishawishi vya kupoteza ari na moyo wa uinjilishaji kwa kujitumbukiza katika malimwengu. Kanisa halina budi kujipyaisha ili libaki na uzuri wake na kuwa na nguvu ya kupambana na changamoto mamboleo. Hii inahitaji kuwapokea vijana na kuwashirikisha katika utume wake

Na Padre Angelo Shikombe, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, katika ziara yake huko nchini Mauritius inayoongozwa na kauli mbiu “hujaji wa amani” Jumatatu tarehe, 9 septemba 2019  katika mahubiri yake amewaalika Taifa la Mungu kumsikiliza Yasu Kristo anayehubiri  kusanyiko la watu wa Mauritius kama vile kristo  alivyowahubiria heri za mlimani wakati wa kipindi cha Mitume miaka elfu mbili iliyopita. Akihubiria katika kilima cha sanamu ya Bikira Maria Malkia wa amani, Port –Louis, Mauritius, amesema, katika unyofu wa mioyo, waamini wanaweza kuangazwa tena na imani iliyohubiriwa na manabii, inayotangaza amani na ukombozi katika ufalme wa Mungu. Heri hizo ni kitambulisho cha Mkristo ambazo zinamtaka kila mtu kufanya kile ambacho Kristo anataka. Katika heri hizo tunakutana na Kristo kiongozi wetu na huyo ndiye anayeongoza utume wa umoja wa Mauritius. 

Mwenye heri Jacque – Desire Laval anayeheshimiwa katika visiwa hivyo, akiongozwa na upendo wa Kristo na huruma kwa maskini, aliweka alama isiyofutika  katika maisha yake yanayofungamana na mafundisho ya Injili. Alitambua wazi kuwa uinjilishaji unahitaji kujitoa kikamilifu kwa Mwenyezi Mungu na kujifunza lugha ya watumwa aliowafundisha habari njema ya wokovu katika lugha rahisi. Aliweza kuunda Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ambazo leo hii zimekuwa Parokia. Majitoleo yake yaliwavutia watu kujiunga na ukristo na kuwaimarisha katika mateso yao. Kutokana na utume wake Padre Laval, Kanisa limehuishwa na hivyo  linahitaji kutumia fursa ya kimisionari ili kuepuka vishawishi vya kupoteza ari na moyo wa uinjilishaji kwa kujiaminisha katika malimwengu katika kupyaisha huko, ndipo Kanisa linabaki na uzuri wake na kuwa na nguvu ya kupambana na changamoto za wakati wetu.

Hii inahitaji kuwapokea vijana na kuwashirikisha katika shughuli za jamii. Pamoja na jitihada za kiuchumi wanazo chukuwa nchini Mauritius lakini bado vijana ndiyo kundi linaloteseka zaidi. Hawana ajira jambo linaloghubika maisha yao endelevu, na kuwazuia kuona mchango wao katika jamii. Wanahisi kutupwa pembezoni mwa jamii. Hii nayo ni aina nyingine ya utumwa mamboleo wa Karne ya ishirini na moja. Katika mahubiri  hayo Baba Mtakatifu anawaalika vijana wote kushiriki furaha ya Kristo si katika kushiriki maongezi yao tu, bali kujifunza lugha yao, masimulizi yao, na kushinda nao ili nao waonje kuwa wamebarikiwa na Mwenyezi Mungu. Hii ndiyo sura mpya ya Kanisa.

Akiwapa ushauri wa kutoruhusu kupokonywa kwa hazina hii ya vijana, Baba Mtakatifu amewaomba watu wote kushirikiana kupambana na utamaduni wa kifo. Akitumia mfano wa mwenye heri Padre Laval, Baba Mtakatifu amesema, mwenyeheri aliwapa vijana muda wa kuimba, na kutoa sauti zao hivyo tumaini letu kwa Kristo linajikita katika ushindi wa Mungu. Aidha Baba Mtakatifu amesema, ujumbe wa Injili haumanishi kuwa hakutakuwa na magumu katika maisha bali, watu wanapaswa kupambana na tamaa hasi zinazopelekea kuwekwa kwa sheria na taratibu zinazokinzana na mapendo ya kweli ya kushirikishana rasilimali Katika kuhitimisha, Baba Mtakatifu amewaasa taifa la Mungu kusikiliza tena heri za mlimani, huku akiwafundisha kuwa ni wakristo wenye furaha wanaoshirikisha furaha yao kwa wengine. Neno “Heri” lenye maana ya “furaha” linajidhihirisha katika kujitoa kwa ukamilifu.

Aidha Baba Mtakatifu amewataka taifa la Mungu kutambua kuwa, kiini cha utume siyo suala la ongezeko la idadi, bali katika kuwashiana moto wa upendo katika jamii ya watu. Hivyo kila mmoja anapaswa kujibidisha na mahitaji ya mwenzake. Jambo hili huwavuta vijana wengi kushiriki utume wa Kristo. Katika utashi wake, Baba Mtakatifu angependa kuupanda mlima huo mtakatifu akifurahia sura ya Kristo na kujifunza kutoka kwake furaha ya kweli. Baba Mtakatifu amewaomba taifa la Mungu kusali kwa pamoja, kuziombea jumuiya mbalimbali ili ziweze kutoa ushuhuda wa furaha ya Kristo. Akizikabidhi mikononi mwa mwenye heri Padre Laval, amewaombea taifa la Mungu baraka na neema ili ziweze kuwalinda. Na pia kwa maombezi ya Mama Bikira Maria wa mateso ameomba Mungu Roho Mtakatifu awaongoze katika furaha ya maisha mapya. 

Papa: Bikira Maria: Amani

 

09 September 2019, 19:31