Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Mgodi wa Mahatazana amesali kwa ajili ya kuwaombea wafanyakazi wote wanaofanya utume wao katika mazingira magumu na hatarishi. Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Mgodi wa Mahatazana amesali kwa ajili ya kuwaombea wafanyakazi wote wanaofanya utume wao katika mazingira magumu na hatarishi.  (ANSA)

Hija ya Papa Francisko nchini Madagascar: Sala ya matumaini kwa wafanyakazi wote!

Katika Sala yake, Baba Mtakatifu Francisko amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha kusimama mbele ya mwamba huu kwa ajili ya kuwaombea wafanyakazi mahali popote pale walipo. Baba Mtakatifu amewaombea wale wanaofanya kazi za suluba, ili katika hali ya mchoko waweze pia kutoa malezi kwa watoto wao. Wajibu & dhamana ya wafanyakazi katika familia & jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mgodi Mahatazana mjini Antananarivo unamilikiwa na Jumuiya ya Akamasoa, maarufu kama “Mji wa urafiki” unao toa ajira kwa wafanyakazi 700. Mgodi huu umekuwa na mafao na maendeleo makubwa kwa watu wanaouzunguka. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Madagascar, Jumapili tarehe 8 Septemba 2019 baada ya kuzungumza na Jumuiya ya Akamasoa amepata fursa pia ya kusali kwa ajili ya kuombea mgodi huu. Katika Sala yake, Baba Mtakatifu amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha kusimama mbele ya mwamba huu kwa ajili ya kuwaombea wafanyakazi mahali popote pale walipo. Baba Mtakatifu amewaombea wale wanaofanya kazi zinazotumia nguvu nyingi kimwili, ili katika hali ya mchoko waweze pia kutoa malezi na makuzi kwa watoto wao. Mwenyezi Mungu awajalie nguvu na afya njema, ili waweze kukabiliana vyema na kazi nzito wanazozitekeleza kila kukicha. Matunda ya kazi ya mikono yao, yasaidie kuboresha maisha ya familia zao, ili wanaporejea nyumbani jioni, waweze kupokelewa kwa upendo, faraja na kupata furaha ya kweli!

Familia zitambue kwamba, kushirikishana matunda ya kazi ya mikono yao, kunawaletea furaha kubwa zaidi. Baba Mtakatifu anawaombea watoto na vijana wasilazimike na hatimaye kufanyishwa kazi za suluba, bali wapate fursa na hatimaye, kuendelea na masomo yao. Walimu wajisadake bila ya kujibakiza katika shughuli zao, bila kutafuta kazi mbadala ya kusaidia kuboresha maisha yao. Mwenyezi Mungu, chemchemi ya haki aguse nyoyo za wamiliki na viongozi wa mgodi, ili waweze kuhakikisha kwamba, wafanyakazi wanapata mshahara wa haki pamoja na kufurahia mazingira mazuri ya kazi yanayo heshimu utu na heshima yao kama binadamu. Mwenyezi Mungu asili ya huruma, awaonee huruma wale wote wasiokuwa na fursa za ajira, ili kweli ukosefu wa ajira unaosababisha kiwango kikubwa cha umaskini, uweze kutoweka katika jamii. Watu watambue na kufurahia heshima ya kujipatia mahitaji msingi kwa ajili ya kusaidia familia na wapendwa wao.

Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kujenga ari na moyo wa mshikamano, ili wafanyakazi waweze kusaidiana na kusumbukiana katika shida na changamoto za maisha; wawe tayari kuwasaidia wale “walioteleza na kuanguka”. Nyoyo zao zisielemewe na chuki pamoja na hasira wanapokabiliana na ukosefu wa haki msingi za binadamu; kwa pamoja waweze kuwa na ujasiri wa kusimamia na kulinda haki zao. Mwenyezi Mungu awasaidie viongozi kusikiliza na kujibu kilio na maombi yao. Mtakatifu Yosefu, Baba Mlishi wa Yesu na Mchumba mwaminifu na jasiri wa Bikira Maria, awalinde wafanyakazi wote duniani. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amewaweka wafanyakazi wa Akamasoa pamoja na wafanyakazi wote wa Madagascar, hasa wale wenye wasi wasi na wanaokabiliana na kazi ngumu, chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu, ili aweze kuwaweka chini ya upendo wa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, ili aweze kuwainua katika maisha na katika matumaini yao!

Papa: Mgodi

 

09 September 2019, 17:15