Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano kujikita katika: Upendo; Ushuhuda na Ukweli wa Kikristo! Papa Francisko anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano kujikita katika: Upendo; Ushuhuda na Ukweli wa Kikristo!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Mawasiliano: Upendo, Ushuhuda & Ukweli

Mawasiliano katika maisha na utume wa Kanisa yanafumbatwa katika ushuhuda; ukweli, uzuri na wema. Huu ndio ushuhuda wa wafiadini na waungama imani; watu walioyamimina maisha kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Mawasiliano ndani ya Kanisa ni mchakato unaofumbatwa katika ujasiri pasi ya kukata wala kukatishwa tamaa na hatimaye, kumezwa na malimwengu! Kazi ya Ibilisi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 23 Septemba 2019 amekutana na kuzungumza na wajumbe pamoja na wafanyakazi wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano. Katika hotuba yake aliyoitoa kwa Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano, ili iwasaidie kwa tafakari, amegusia kuhusu: Changamoto za mawasiliano, mawasiliano kama utume wa Kanisa; umuhimu wa kufanya kazi kwa umoja na mshikamano kama timu na kwamba, mfumo wa mawasiliano ya Kanisa unafumbatwa katika ushiriki na kushirikishana kama ushuhuda wa umoja wa Kanisa la Kiulimwengu na Makanisa mahalia na kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro ataendelea kuunga mkono miradi mbali mbali ya ushirikiano kati ya Vatican na Makanisa mahalia. Baba Mtakatifu amesema, “cheche za mageuzi” ya vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican imekuwa ni “shughuli pevu” kutokana na ugumu wa mchakato wenyewe pamoja na hali ya kudhaniana vibaya.

Baba Mtakatifu anaridhishwa na hatua mbali mbali za mageuzi zilizokwisha kufikiwa, kwa kuwa na mikakati ya utekelezaji kwa muda mfupi na mrefu. Lengo ni kuhakikisha kwamba, rasilimali watu, fedha na vitu vinatumika kikamilifu, ili kupunguza pia gharama za uendeshaji wa sekta ya mawasiliano ndani ya Kanisa. Katika hotuba iliyobubujika kutoka katika sakafu wa moyo wake kuhusu umuhimu wa mawasiliano amekazia mambo makuu matatu: Umuhimu wa watu wote kufanya kazi kama kiu ya Mungu ya kutaka kuwasiliana; mawasiliano yanayofumbatwa katika ushuhuda na ukweli wa Kikristo. Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu ni chanzo na kilele cha mawasiliano, kwani anataka kuwasiliana na waja wake jinsi alivyo, kutoka katika undani wake. Kumbe, wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii wanapaswa kuwasiliana kwa kutumia akili, moyo na mikono yao; kwa maneno mengine, haya ni mawasiliano yanayomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, kielelezo cha juu kabisa cha mawasiliano ni upendo wa Mungu ambao umemwilishwa kati ya waja wake.

Mawasiliano yanayotekelezwa na Mama Kanisa si matangazo ya biashara wala wongofu wa shuruti. Kanisa linakuwa na kupeta kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Mawasiliano katika maisha na utume wa Kanisa yanafumbatwa katika ushuhuda; ukweli, uzuri na wema. Huu ndio ushuhuda wa wafiadini na waungama imani; watu walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Mawasiliano ndani ya Kanisa ni mchakato unaofumbatwa katika ujasiri pasi ya kukata wala kukatishwa tamaa na hatimaye, kumezwa na malimwengu na hiki ni kishawishi cha Shetani, Ibilisi hata katika karne ya ishirini na moja. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu katika Sala yake ya Kikuhani, aliwaombea wafuasi wake, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwatakasa kwa ile kweli kwani Neno la Mungu ndiyo ile kweli. Wametumwa ulimwenguni lakini wao si wa ulimwengu huu. (Rej. Yoh. 17: 12-19). Wadau wa tasnia ya mawasiliano wasishikwe na kishawishi cha kutaka kujifungia katika upweke wao, kwa kutaka kuendelea kubaki katika udogo wao.

Baba Mtakatifu anasisitiza kwamba, wanahabari ni chumvi na chachu ya kuyatakatifuza malimwengu, kwa kuondokana na utamaduni wa watu kukata tamaa na kulalama kila wakati. Hata katika udogo na uchache wao, bado wanaweza kutenda makubwa kwa njia ya ushuhuda. Huu ni ushuhuda unaotangazwa na kushuhudiwa kwa njia ya tunu msingi za maisha ya Kikristo. Kanisa nchini Ukraine limefumbatwa katika ushuhuda unaohifadhi Mafundisho tanzu ya Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, waandishi wa habari wanapaswa kutangaza ukweli wa Kikristo unaofumbatwa katika ukweli wa mambo, bila kuweka chumvi au kuwabeza wengine. Ndani ya Kanisa, watu wajisikie kuwa ndugu wamoja na watangaze uzuri. Hii ndiyo lugha ya mashuhuda wa imani na wafiadini, waliotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Waandishi wa habari wawe mashuhuda wa Kristo kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu, kama inavyoshuhudiwa katika Kitabu cha Matendo ya Mitume. Waandishi wa habari, wawe ni mashuhuda wa furaha ya Injili, changamoto changamani katika ulimwengu mamboleo. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano!

Papa: Mawasiliano

 

24 September 2019, 15:10